Na, Geofrey Archard Kazaula.
Wananchi Katika Wilaya ya Karagwe wamehimizwa kujenga vyoo bora na imara kama sehemu ya kinga kwa afya zao.
Akizungumza na wananchi Katika Kata ya Nyakabanga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Karagwe ndg, Innocent Nsena amesisitiza juu ya uwepo wa vyoo bora na imara kwani hadi sasa kuna takribani Kaya 619 ambazo hazina vyoo kabisa huku baadhi ya Kaya zikiwa na vyoo ambavyo si bora.
Kiongozi huyo amesisitiza juu ya kila Kaya kuwa na choo bora ikiwa ni pamoja na miundombinu ya maji kwa ajili ya kunawa mikono na kwamba kwa kutofanya hivyo, wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwani sheria ipo wazi kuwa kwa atakaye kutwa bila choo bora atatozwa faini isiyopungua laki moja ( 100,000) au kifungo cha miezi sita.
‘‘ Niwaombe wananchi mtambue wazi kuwa sheria ipo na si kwa matakwa yangu bali ni kwa mujibu wa sheria na tukifanya ukaguzi tukabaini mtu ambaye hana choo bora sheria itachukua mkondo wake ikiwa ni pamoja na kulipa faini isiyopungua T.Sh 100,000 au kifungo cha miezi Sita’’alifafanua kiongozi huyo.
Kwaupande wake Afisa Afya wa Wilaya ya Karagwe Ndg, Beatrice Laurent ame eleza kuwa Idara ya Afya kupitia Afisa Afya imekuwa ikitoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuwa na choo bora na imara licha ya baadhi ya wananchi kutotilia maanani maagizo yanayotolewa na kusisitiza kuwa hatua za kisheria kwa wanao kaidi zitaanza kuchukuliwa .
‘‘ Tumekuwa tukitoa elimu mara kwa mara lakini wapo watu ambao bado wana kaidi, sisi tutachukua hatua za kisheria kwani kutokuwa na choo bora kunaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya mlipuko ambayo yata athiri jamii yetu’’ alisema afisa huyo.
Wilaya ya Karagwe inendelea na zoezi la kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuwa na choo bora kama sehemu ya kinga ya magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.