Uzinduzi wa Mradi wa “Sambaza Mbegu Fasta” wafana Wilayani Karagwe.
Na Innocent E. Mwalo, Karagwe.
Maadhimisho ya siku ya wakulima(Field Day) yaliyoenda sambamba na uzinduzi wa Mradi wa sambaza Mbegu Fasta pamoja na uzinduzi wa kitabu cha Lishe chenye Maudhui ya Umuhimu na Matumizi ya Viazi Vitamu yamefanyika wilayani Karagwe katika eneo la Shule ya Msingi Bujuruga iliyopo katika kata ya Bugene mnamo tarehe 13/10/2017 huku wito ukiwa ni kuihamasisha jamii ya watu wa maeneo ya wilaya hii kuacha kuwa na fikra za kulima zao moja la migomba na badala yake wajielekeze kulima mazao mengine kama vile viazi vitamu kwa ajili ya kinga ya njaa na lishe kwa watoto wao.
Wito huu ulitolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hii, Mh. Wallace Mashanda katika viwanja vya shule ya msingi Bujuruga alipokuwa mgeni rasmi katika hafla siku ya Wakulima(Field Day) iliyokuwa mahususi kwa ajili ya Uzinduzi wa Sambaza Mbegu Fasta na uzinduzi wa kitabu cha Lishe lakini pia kulijadiliwa Mipango kadhaa ambayo Halmashauri inapaswa kuwa nayo ili itakapofika mei 2018 baada ya mradi kuisha muda wake wa ufadhili basi Halmashauri ya Wilaya iwe na uwezo wa kuendelea nayo.
Mradi huu wa kusambaza marando kwa ajili ya wakulima ukiwa kwa jina maarufu la “Kopa Mbegu na Lipa Mbegu” unaofadhiliwa na Chuo cha Kilimo cha Ukiliguru chenye ofisi zake mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Chuo cha Kilimo cha Maruku kulichopo wilayani Bukoba, Mkoani Kagera ulianza kufanya kazi mapema mwezi Mei 2017 na unatarajia kufika mwisho wa ufadhili mwezi Mei 2018 huku Halmashauri ya Wilaya Karagwe ikipaswa kuchukua jukumu la msingi la kuuendeleza mradi huu.
Itakumbukwa kwamba mradi wa kusambaza mbegu bora za marando uliofanywa kupitia watoto wa shule za msingi ulianza wilayani hapa mwezi Mei, 2017 na ulikuja kutokana na maombi kadhaa ambayo Halmashauri ya Wilaya hii iliyatoa mara kadhaa kupitia serikali kuu na wadau wengine ili kuomba serikali na wadau hao kuingilia kati suala la kuendeleza kilimo cha mazao ya kinga ya njaa kufuatana na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa yanayoambatana na kiangazi cha muda mrefu na hivyo kuathiri mazao muhimu kama vile mahindi na mazao ya jamii ya mikunde ambayo yamezoeleka sana kulimwa wilayani hapa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Mh. Wallace Mashanda ni kwamba kwa miezi mitatu yaani miezi ya (Juni- Septemba 2017) zaidi ya wazalishaji mbegu 88 wamesambaziwa mbegu za kisasa ambapo zaidi ya pingili 74,000 zilizopitia kwa watoto wa shule za Msingi za Bujuruga, Karagwe, Kandegesho na Chabuhora.
Wajasiliamali zaidi ya 100 walipatiwa mafunzo kupitia kwa maafisa Ugani na Halmashauri ilichangia gharama za usafirishaji wa mbegu hizo kutoka Missenyi hadi Karagwe.
“Tunawashukuru waandaaji wa maadhimisho haya kwa kuiweka Halmashauri ya Wilaya Karagwe kati ya wilaya 08 za kanda ya ziwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya”, alisema Mh. Mashanda.
Mh. Mashanda alitoa agizo kwa maafisa ugani wa Halmashauri ya wilaya hii kuhakikisha wananchi wanahamasishwa kikamilifu kwa kuwapa Elimu ya kuongeza thamani ya usindikaji wa viazi lishe ili wananchi hawa wapate kunufaika na uzalishaji wa zao hili la viazi vitamu.
“Nikuombe Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashahuri ya Wilaya kuwaagiza Wakuu wa Idara za Mipango,Kilimo, Sekondari, Msingi, Maendeleo ya Jamii na Afya li wataalam hawa watengeneze mpango mkakati wa Mradi huu ili kuufanya kuwa endelevu hata baada ya kutukabidhi Halmashauri”, alisema Mh. Mashanda.
Mh. Mashanda aliagiza kukamilishwa kwa mpango mkakati huo kabla ya Novemba 2017 ili uweze kuwasilishwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani kitakachofanyika mwezi Novemba kwa ajili ya Baraza kuja na mikakati ya kuendeleza mradi huo utakapokabidhiwa kwa Halmashauri.
“Wito wangu wa pili ni kwamba Idara ya Elimu Msingi isimamie vema ufundishaji wa somo hili la Elimu ya Lishe kupitia kitabu kilichoiandaliwa na Jukwaa la Kilimo lisilokuwa la kiserikali lijulikanalo kama ANSAF ambao kwa kushurikiana na Serikali, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wameweza kuandaa kitubu hicho cha Elimu ya Lishe; Kuhusu umuhimu na matumizi ya viazi vitamu”, alisema Mh. Mashanda.
Kwa upande wake ndugu Beka Chilimu, aliyekuwa akimwakilisha Mkurugenzi kutoka Chuo cha Utafiti cha Kilimo cha Ukiliguru, ndugu Eveline Rukonge aliwasisitiza wananchi waliokusanyika katika maeneo haya kuzingatia kikamilifu ushauri wote unaotolewa na maafisa ugani ili kilimo hicho kiweze kuwaongezea kipato na lishe.
Naye Rehema Msamy aliyekuwa anamwakilisha Mkurugenzi wa ANSAF, alitoa wito kwa walimu kufundisha somo hilo linalohusiana na stadi za Elimu ya Lishe kwani wanafunzi hao wakipata stadi hizo watakuwa mabalozi wazuri na kufanya jitihada za kupambana na udumavu mkoani Kagera mkoa unaotajwa kuwa na udumavu kwa asilimia 42 jambo linalochangiwa na ukosefu wa lishe bora.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Dawson Paulo Bwamanyirwohi aliwashukuru chuo cha Kilimo Ukiliguru kwa kushirikiana na chuo cha Kilimo cha Maruku kwa mradi huo lakini lakini akawaomba wadau hao kuisaidia Halamshauri katika kusambaza mbegu katika maeneo yote ya Halmashauri ya Wilaya Karagwe kabla ya kuukabidhi mradi huo kwa Halmashauri ya wilaya hii mapema mwezi Mei 2018.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.