Mamia wafurika mkutano wa Mbunge wa Karagwe
Na Innocent E. Mwalo, Kayanga
Katika hali isiyo ya kawaida wananchi wa Kata ya Kayanga na maeneo yote ya Wilaya Karagwe jumapili ya tarehe 09/07/2017 walijitokeza kwa wingi kumsikiliza mbunge wao wa Karagwe Mh. Innocent Lugha Bashungwa katika mkutano unaotajwa kuwa wa aina yake uliofanyika katika uwanja wa changarawe katika kata ya Kayanga alimaarufu kama uwanja wa “Push –Up”
Mkutano huo wa mbunge ulioanza majira ya saa kumi jioni ulidumu kwa takribani kwa masaa matatu huku mbunge huyo akitumia wasaa huo kutoa mrejesho wa mambo kadhaa yaliyofanywa na serikali kwa muda wa mwaka mmoja na miezi saba na yale yaliyojiri kwenye bunge la bajeti lilimalizika Julai 06, 2017 mjini Dodoma ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea kufanya hvyo kwa wananchi wake kila unapomalizika mkutano wa bunge .
Mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa serikali, Chama cha Mapinduzi na viongozi mbalimbali wa vyama vingine vya siasa, ulipambwa na vijana wa Skauti ambao ni mkusanyiko wa wanafunzi mbalimbali wa shule za msingi zilizopo wilayani Karagwe na burudani ya muziki iliyoonekana kukonga nyoyo za viongozi na wananchi waliohudhuria kusanyiko hilo la mbunge.
Wanafunzi toka shule ya Sekondari Kayanga walipata nafasi ya kutumbuiza kupitia shairi lao la zaidi ya beti tano ambalo pamoja na mambo mengine liligusia changamoto kubwa wanayokutana nayo katika mazingira ya kujifunza ambayo ni shida ya maji na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi.
Awali, Diwani wa Kata ya Kayanga yalipo makao makuu ya Wilaya, Mh. Bi. Adventina Kahatano alipopata fursa ya kusalimia wananchi alimpongeza mbunge kwa jitihada kadhaa anazozifanya katika kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya Karagwe bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa.
Katika risala iliyosomwa na Benjamini Mazimba kwa niaba ya Mtendaji wa Kata ya Kayanga iligusia mafanikio kadhaa yaliyofikiwa katika kata hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara za lami katika njia kadhaa za mitaa ya Kayanga pamoja na ujenzi wa wodi ya wanaume unaendelea katika kituo cha Afya Kayanga.
Naye Mh. Wallace Mashanda, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Karagwe alipopata nafasi ya kuwasalimia wananchi alijaribu kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari kupitia shairi lao iliyokuwa inahusu tatizo la maji shuleni hapo.
Mh. Mashanda aliwataka wanafunzi hao na wananchi hao kuwa na subira kwani suala hilo litapatiwa ufumbuzi kupitia mikakati ya muda mrefu na ile ya muda wa kati.
Alisema serikali inao mkakati wa muda mfupi wa kuhakikisha maji yanapatikana katika maeneo ya mji wa Kayanga akiyataja baadhi ya maeneo kuwa ni maeneo yote ya Kayanga Shule ya Sekondari, maeneo ya Bomani, baadhi ya maeneo ya Katoma Ruzinga na maeneo mengine yanaozunguka mji wa Kayanga.
Aliwahakikishia wananchi hao kuwa tayari serikali imeshatoa kiasi cha bilioni 1.8 kupitia BUWASA kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji unatarajiwa kakamilika kabla ya mwaka wa fedha 2018/2019 lengo likiwa kuwapunguzia wananchi kero ya maji.
Nje ya mkakati huo wa muda mfupi Mh. Mashanda aliutaja mkakati wa muda mrefu wa shilingi bilioni 60 wa kutoa maji toka ziwa Rwakajunju kuwa ni mkakati unaolenga kumaliza kabisa tatizo la maji na kulifanya kuwa historia kabisa katika wilaya ya Karagwe siku za usoni.
Aligusia suala la ujenzi wa barabara za mjini Kayanga ambapo aliwaambia wananchi hao kuwa Halmashauri ya wilaya imetenga takribani kiasi cha milioni 686 ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa barabara za maeneo hayo.
Kisha baada ya salaam hizo za mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Karagwe, ilifuata zamu ya Mh. Innocent Lugha Bashungwa mbunge wa jimbo la Karagwe ambaye katika hotuba yake ambayo ilikuwa ikikatizwa mara kwa mara na kelele za wananchi waliokuwa wakimshangilia kwa furaha hasa baada ya kugusia maeneo mbalimbali ambayo kimsingi yanatajwa kuwa kero kubwa kwao kwa muda mrefu.
Mh. Bashungwa alianza na maeneo yanayogusa mambo ambayo yeye binafsi na kwa kushirikiana na serikali yameweza kushughulikiwa na serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba kwa ajili ya kuwaletea maendeleo ya wananchi wa Karagwe.
Jambo la kwanza lililotajwa na Mh. Bashungwa lilikuwa ni upatikanaji wa gari la zimamoto wilayani Karagwe, upatikanaji wa gari la wagonjwa lenye viwango kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa pamoja na upatikanaji wa gari la chanjo lililoletwa kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa chanjo vijijini ambapo ndiko wananchi wanyonge wanapatikana.
Mh. Bashungwa alilitaja jambo jingine ambalo amelipigania kufa na kupona kuwa ni kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana katika hospitali, zahanati na vituo vya afya.
“Mnakumbuka mwezi Machi mwaka huu kulitokea upungufu mkubwa wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali yetu ya Nyakahanga, lakini nilipoongea na serikali kupitia vyombo vya habari kwa kweli serikali kupitia MSD (Wakala wa usambazaji wa dawa) waliweza kusambaza dawa hizo kwa kwa wakati na nikiri kwamba kwa kweli kwa sasa hakuna tatizo tena la dawa”, alisema Bashungwa.
“Zaidi ya hapo serikali kwa sasa inatuma moja kwa moja fedha za kununulia dawa kwenye Halmashauri” alisisitiza Mh. Bashungwa huku akishangiliwa na wananchi waliofurika kumsikiliza.
Alianisha jitihada nyingine zilizofanywa na serikali kwa kipindi hiki kuwa ni upatikanaji wa millioni 170 zilizoletwa na serikali kwa kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanaume, ujenzi wa chumba ch kuhifadhia maiti na ujenzi wa chumba cha maabara unaendelea katika kituo cha Afya Kayanga.
Kuhusu sekta ya Nishati, Mh. Bashungwa alitumia hadhara hiyo kuwajulisha wananchi hao juu ya ujio wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Medard Kalemani wilayani Karagwe mnamo tarehe 11/07/2017 ziara inayotarajiwa kuja kuzindua mradi wa usambazaji wa umeme unaotekelezwa na Wakala wa Umeme vijijini (REA) ikiwa ni awamu ya tatu inayotajia kufika katika vijiji kadhaa vya Halmashauri ya wilaya Karagwe.
Katika sekta ya ujenzi, Mh. Bashungwa aliwaambia wananchi hao kuwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa barabara ya Omugakorongo- Murongo unatajia kufanyika katika mwaka wa Fedha 2017/2018 huku upembuzi yakinifu ukiwa umekamilika kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nyakahanga- Benaco na serikali ikiwa katika hatua za kutafuta fedha ili ujenzi wa barabara hiyo uweze kuanza mara moja.
Huku akishangiliwa na wananchi, aliitaja barabara nyingine ambayo imekuwa kero sana kwa wananchi wa wilaya ya Karagwe kuwa ni ile ya Nyakahanga- Nyabiyonza –Kayungu ambapo kwa sasa barabara hiyo inahudumiwa na wakala wa barabara (TANROARD) na kwa hiyo basi fedha ya kuihumia barabara hiyo inatoka moja kwa moja Hazina jambo linaloipunguzia mzigo Halmashauri kwani fedha ambayo ungepangwa na Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya kuhudumia barabara hiyo sasa itaelekezwa katika ujenzi wa barabara nyingine.
Mh. Bashungwa aliainisha eneo jingine alilolishughulikia kuwa ni ujenzi wa kituo cha polisi cha wilaya ambapo kwa kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa wilaya Karagwe wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kituo hicho kinajengwa.
Pamoja na hayo, Mh. Bashingwa huku akiongea kwa tahadhali kubwa alimuomba Mkuu wa Polisi Wilaya, SSP. Mika Makanja kufanyia kazi malalamiko ya wananchi kuhusu askari wa usalama barabarani ambapo kwa maelezo ya Mbunge huyo wananchi wanalalamika sana kunyanyaswa na askari hao hasa kwa wananchi wale wanaoendesha pikipiki.
Katika sekta ya Kilimo, Mh. Bashungwa aliujulisha umma huo ya kwamba serikali imeondoa kodi 17 kwenye zao la kahawa na hivyo basi hata kwa zile 09 zilizobaki ni kusudio la serikali kuziondoa zaidi ili wananchi wanyonge waendelee kunufaika.
Mbunge aliisa Halmashauri ya wilaya kuhakikisha inakuwa na mkakati wa kugawa miche kwa wakulima na wakati huo aliwaambia wananchi hao kwamba serikali imebadili mfumo wa ugawaji wa pembejeo na kwamba kwa sasa wananchi watapaswa kupewa pembejeo miezi miwili kabla ya msimu wa Kilimo.
Pia alisisitiza jukumu la Halmashauri katika kuhakikisha wananchi wanaacha kuuza lumbesa.
Jambo jingine lilikuwa ni ujenzi wa soko la Kayanga ambapo itakumbukwa kwamba soko hilo limepata kuungua mara mbili yaani mwaka jana na mwaka huu kwa hivyo mbunge akitumia fursa hiyo kuomba ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kufanywa kwa ubia kati ya serikali na wananchi kuanza mara moja kwani kwake Mh. Bashungwa soko ni moja kati ya vitambulisho muhimu vya mji wa Kayanga.
Kuhusu suala la Elimu, Mh. Mbunge alitaja malengo yake ya kuhakikisha kila tarafa inakuwa na shule ya Sekondari ya Kidato cha tano huku malengo ya kukifanya chuo cha ualimu cha Ihanda kuwa shule ya sekondari kwa wasichana wa kidato cha tano yakitajwa.
Pia aligusia suala la upungufu wa walimu 100 wa masomo ya sayansi kwenye shule za sekondari na upungufu wa takribani walimu 800 kwa shule za msingi kuwa ni changamoto ambayo tayari ameshamwandikia Katibu Mkuu wizara ya Utumishi kwa ajili ya kulipa msukumo jambo hilo.
Mwishoni wananchi walipata nafasi ya kumuuliza maswali mbunge wao ambapo suala la kununua gloves, daftari na vifaa vingine kwa wananchi wanapoenda kutibiwa lilijitokeza na lilijibiwa na Mganga Mkuu wa wilaya Karagwe, Dkt. Libamba Sobo aliyeitwa na mwenyenyikiti wa Halamshauri kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi jambo hilo ambapo Mganga mkuu huyo alitoa katazo kwa wataalam wa Idara ya Afya wanaofanya jambo hilo kuacha kufanya hivyo huku mbunge akiendelea kuwasisitiza wananchi kuendelea kuweka msisitizo katika suala upimaji wa ardhi pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji kazi aliyoitaja kuwa inafanywa kwa ufanisi mkubwa kwa kipindi hiki tofauti na awali.
Hotuba hii ya Mh. Mbunge ilikuwa inajibu kero mbalimbali zilizotajwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati anazindua Bunge la kumi na moja mjini Dodoma mnamo tarehe 20 Novemba, 2015 hasa kuhusu azima yake ya kuwatua akina mama ndoo kichwani akiwa na kusudi la kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwenye maeneo yote nchini unafanikiwa ambapo kwa wilaya ya Karagwe miradi mbalimbali ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la maji inaendelea.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.