“Tutaendelea Kuunga Mkono Jitihada za Wafadhili”, asema Kitonka.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe ndugu Godwin Kitonka ameahidi na kusisitiza kwamba serikali ya Halmashauri ya Wilaya hii itaendelea kuunga mkono pamoja na kuthamini juhudi zinazofanywa na wafadhili katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani hapa.
Ndugu Kitonka aliyasema haya Novemba 21, 2017 alipozungumza ofisini kwake na wageni kutoka katika shirika lisilo la kiserikali la Jambo Bukoba ambao ni Bi. Imani Paulo, Meneja Mradi na Bw. Lameck Kiula, Meneja Mawasiliano.
Aidha katika msafara huo alikuwepo Bi Heike Henstschel ambaye ni Mkuu wa Shule ya Kurt Masul kutoka Ujerumani aliyeambatana na mwalimu kutoka katika shule hiyo Bi. Katja Wachler, Bi Costanze Meinel ambaye ni mmoja wa wazazi wenye watoto katika shule hiyo ya Kurt Masur na Bi. Manuela Hubner ambaye ni mratibu katika shule hiyo.
Msafara huo uliokuwa umeambatana na Afisa Utamaduni wa Wilaya hii ndugu Alloyce Mujungu uliwahusisha pia mwalimu Elizeus Iromba, mwalimu Willium Magesa na wanafunzi wawili wa darasa la sita ambao ni Eliya Petro na Asimwe Karugendo wote kutoka katika shule ya Msingi Karalo.
Mapema ujumbe huo ulijitambulisha kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ambapo Mkuu wa msafara Bi. Iman Paulo aliweza kumweleza Mkurugenzi Mtendaji kwamba tangu kuanzishwa kwa shirika la Jambo Bukoba mnamo mwaka 2008, Taasisi hiyo imekuwa ikisaidia katika shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani hapa.
“Tangu kuanzishwa kwa taasisi yetu tumekuwa tukufundisha vijana wa shule ya msingi usawa wa kijinsia, Elimu ya UKIMWI na ujenzi wa miundombinu ambapo hapa wilayani Karagwe taasisi yetu imeweza kujenga madarasa mawili pamoja na kutoa madawati 20 katika Shule ya Msingi Karalo”, alisema Bi. Imani
“Kadhalika taasisi imeweza kujenga kisima cha maji shule ya msingi Maguge pamoja na kujenga matundu ya choo katika shule za msingi za Maguge na Ahakishaka”, alisisitiza Bi. Imani.
Kisha baada ya maelezo hayo Bi. Imani alimweleleza Mkurugenzi Mtendaji kwamba lengo la ziara yao ya Novemba 21, 2017 ilikuwa kwenda Shule ya msingi Karalo kwa ajili ya kwenda kuwatambulisha marafiki wa shule ya msingi Karalo ambao ni shule ya Kurt Masur iliyopo nchini Ujerumani.
Kadhalika Bi. Imani alizitaja zawadi za kompyuta mpakato (laptop), kamera na simu ya smart phone zilizotolewa na shule ya Kurt Masur kwa lengo la kurahisisha mawasiliano na shule ya msingi Karalo.
Huku akionesha furaha kubwa aliyokuwa nayo kwa wageni hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, ndugu Kitonka aliwashukuru sana Jambo Bukoba kwa jinsi ambavyo wamekuwa mstari wa mbele katika kutekeza miradi ya maendeleo Wilayani hapa.
“Kwa kweli Jambo Bukoba mnastahili pongezi kubwa sana mmekuwa msaada mkubwa katika shughuli za maendeleo hapa wilayani kwetu”, alisisitiza ndugu Kitonka.
Na kwa namna ya pekee, ndugu Kitonka aliutaja urafiki unakwenda kuanzishwa kati ya shule ya msingi Karalo na shule ya Kurt Masur ya Ujerumani kuwa utakuwa chachu ya kubadilishana wanafunzi.
Fursa nyingine aliyoitaja ilikuwa ni suala la kushirikiana katika mitaala na maeneo mengine.
“Nipende kuwaomba wenzetu wa shule ya Kurt Masur kuongeza wigo wa maeneo ya kushirikiana lakini niwashukuru sana kwa hatua hii waliyofikia pamoja na zawadi hizo walizozitoa na niagize kwa walimu wa shule ya Msingi Karalo kuvitunza vifaa hivyo.
Shirika la Jambo Bukoba lilianzishwa mwaka 2008 na tangu kuanzishwa kwake limekuwa likitoa huduma mbalimbali hasa kufundisha vijana wa shule za msingi usawa wa kijinsia, kufundisha Elimu ya UKIMWI na ujenzi wa miundombinu.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.