Na Geofrey A.Kazaula
Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) imeendelea kuboresha huduma za misitu na mazingira kwa kusimamia zoezi la uoteshaji wa miti na kuwapatia wananchi kwa ajili ya kupanda.
Akizungumza na wananchi katika Kata ya Nyakasimbi, Meneja wa Misitu kwa Wilaya ya Karagwe Bw. Sunday John Anut amefafanua kuwa zoezi la uoteshaji na upandaji wa miti linafanyika ili kutoa mwelekeo chanya wa Taasisi katika kusaidia jamii ili kuboresha mazingira na kusaidia wananchi kukuza uchumi wao.
Aidha amefafanua kuwa Wakala wa misitu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wamefanya tathmini ya uoteshaji miti katika maeneo mbalimbali kukiwa na lengo la kutathmini idadi ya miche iliyo ota kutokana na mbegu, viriba na elimu iliyotolewa kwa wadau wa upandaji miti ikiwa ni pamoja na kutambua na kubaini changamoto za uoteshaji miti kutoka kwa wadau.
‘‘ Sisi kama taasisi tumefanya tathmini baada ya kutoa elimu ya uoteshaji na upandaji miti kwa wananchi na hata hivo tumebaini kuwa mwitikio ni mkubwa sana kwani maeneo mengi miti imeota na wananchi wanaendelea kupanda hivyo ninona kuwa siku za usoni wananchi wataboresha kipato chao kutokana na faida kubwa watakayopata kutokana na miti’’ alisema mtaalam huyo.
Baada ya kukamilika kwa tathmini, imebainika kuwa takribani miche 83,826 ilioteshwa ambapo ni sawa na asilimia 28% ya lengo la kuotesha miche 300,000 na changamoto zilizojitokeza katika zoezi hilo ni pamoja na uhaba wa maji uliosababishwa na ukame katika baadhi ya Kata kama Chanika zenye uhaba wa maji.
Jumla ya Kg 108 za Viriba ziligawiwa kwa wadau wa upandaji miti katika Kata mbalimbali za Wilaya ya Karagwe na wananchi sasa wanajipanga kuendelea na zoezi la upandaji miti kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kuboresha uchumi wao.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.