Rais Museveni Kujenga Makumbusho ya Kihistoria Bweranyange, Karagwe.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, ameahidi kutoa kiasi cha Tsh. 258,289,135 ili kufadhili wa Ujenzi wa Makumbusho ya Omukama Rumanyika I Orugundu, Bweranyange Wilayani Karagwe lengo likiwa ni kuyaendeleza Makumbusho hayo na kuyafanya kuwa kivutio cha utalii na utamaduni Wilayani Karagwe na Tanzania kwa ujumla.
Wakati ombi hilo la ufadhili likiwa limekubaliwa na Rais Museveni kupitia kwa timu ya watu wanne waliotoka Wilayani Karagwe kwa minajili ya kumwona Rais huyo iliyokuwa inawahusisha Mchungaji Dkt. Geofrey Aligawesa, Bi. Georgia Ruhinda, ndugu Alloyce Mujungu, ndugu Theonest Kishenyi na Bi.Bahati Rumanyika ambaye ni mtoto wa David Rumanyika.
Rais Museveni aliahidi kumshirikisha kwanza kwa namna ya pekee , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa Tanzania na kazi hiyo inatarajiwa kufanywa hivi karibuni wakati viongozi wetu hawa wawili watakapokutana mjini Hoima nchini Uganda kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la msingi Bomba la mafuta.
Ili kukamilisha hatua muhimu za kufikia hatua hiyo ya ujenzi wa Makumbusho ya Bweranyange wilayani hapa, uongozi wa Wilaya Karagwe ukiwahusisha Mh. Innocent Lugha Bashungwa, Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Karagwe, Mh. Wallace Mashanda na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, ndugu Godwin M. Kitonka tayari wameshaanza utekelezaji wa baadhi ya ushauri uliotolewa na Rais Museveni ili viongozi hawa wawili (Rais Museveni na Rais Magufuli) watakapokubaliana kupitia mazungumzo yao haya yatakayofanyika mjini Hoima.
Itazingatiwa kwamba Rais Museveni alishauri mambo kadhaa yafanyiwe kazi ili makumbusho hayo yatakapokamilika basi yafanane na makumbusho mengine ya kisasa.
Baadhi ya ushauri wa Rais Museveni ilikuwa kwamba rejea ifanywe katika maandishi mbalimbali ya kihistoria yaliyowahi kufanyika kabla na baada ya ukoloni hadi sasa kama vile ujio wa wamisionari Afrika ya Mashariki juu ya utawala wa jadi wa Karagwe ili historia hiyo iweze kuwekwa kwenye Makumbusho haya ya Bweranyange ili kukuza utalii na utamaduni.
Wakati huo huo utekelezaji wa baadhi ya mambo umeshaanza kufanyika wilayani hapa ambapo mapema tarehe 09/10/2017, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe Mh. Dawson Paulo Byamanyirwohi akiambatana na timu ya wataalamu toka Halmashauri ya Wilaya wakiwemo Afisa Ardhi wa Wilaya ndugu Essau Bernard, Afisa Kilimo wa Wilaya ndugu Adam Salamu, Afisa Mazingira wa Wilaya ndugu Procesius Rweyendera, Fundi sanifu wa Majengo ndugu Raphael Tibaijuka Mudogo na Afisa Utamaduni wa wilaya ndugu Alloyce Mujungu.
Msafara huo uliambatana pia na Mwenyekiti wa Mpango Mkakati wa Wilaya Karagwe, Mchungaji Dkt. Godfrey Aligawesa na baadhi ya wanafamilia wa Omukama Rumanyika I Orugundu akiwemo ndugu Georgia Ruhinda.
Baada ya kuwasili Bweranyange, ujumbe huo ulizuru maeneo hayo ya makazi ya Rumanyika I Orugundu kisha wakaelekea katika kijiji cha Kijumbura ambapo Mkutano wa Hadhara ulikuwa umeitishwa kwa lengo la kujadili matumizi bora ya ardhi na ujenzi wa makumbusho ya Omukama Rumanyika I Orugundu.
Afisa Utamaduni, Aloyce Mujungu aliwakumbusha wanakijiji hao wa Kijumbura juu ya baadhi ya maazimio yaliyofikiwa katika kikao cha Familia ya Marehemu Omukama Rumanyika na serikali ya Halmashauri ya wilaya Karagwe tarehe 05/01/2008 kutokana na ardhi hiyo ya Omukama Rumanyika I Orugundu kuvamiwa na baadhi ya wananchi kwa shughuli za kilimo na wengine wakiwa wamejenga bila idhini yeyote katika maeneo hayo.
Baadhi ya maazio yalikuwa ni kwamba watu wasivamie ardhi ya makumbusho ya Omukama Rumanyika I Orugundu kwa shughuli za kilimo, baadhi ya wanaukoo waliamriwa wasiuze eneo hilo kiholela kwa manufaa yao binafsi, serikali ya Halmashauri ya wilaya iliamriwa itoe Hati miliki ya ardhi na ikabidhiwe kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe ili kuwadhibiti wavamizi wote wasiotakiwa katika eneo hilo.
Maazimio mengine yalikuwa Serikali iendeleze eneo la Makumbusho kwa manufaa ya watanzania wote pia ipandwe miti ya asili katika eneo la makumbusho ili kulinda uoto wa asili na jamii ielimishwe kuheshimu maeneo hayo.
Maazimio mengine yalikuwa ni kwamba maeneo yaliyokuwa ya kuwazika wakama huko Kawela yasivamiwe na wananchi na pia ilishauriwa itungwe sheria ndogo ya kulinda maeneo ya makumbusho ya Halmashauri lakini pia ilishauriwa uwepo ushauri wa kitaalam juu ya ukarabati wa majengo ya kufufua makumbusho hayo.
Kwa hiyo basi kupitia kikao hicho cha tarehe 09/07/2017 wataalam wa Halmashauri ya Wilaya waliweza kutoa majibu ya maazimio hayo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mh. Byamanyirwohi na Mchungaji Aligawesa kwa nyakati tofauti waliwasihi wananchi hao kukubaliana na wazo hilo la kujengwa kwa makumbusho hayo kwani kukamilika kwake wananchi hao watapata faida kadhaa wa kadhaa ikiwemo usogezwaji wa huduma za kijamii kwa wananchi na ujenzi wa miundombinu bora ikiwemo barabara za lami.
Huku wataalamu toka Halmashauri akiwemo ndugu Alloyce Mujungu (Afisa Utamaduni wa wilaya ) ndugu Essau Bernad (Afisa Ardhi wa Wilaya), ndugu Adam Salamu (Afisa Kilimo), ndugu Procesius Rweyendera (Afisa Mazingira) na Fundi Sanifu wa Majengo, ndugu Raphael Mudogo wakisisitiza mambo kadhaa ikiwemo kuwasihi wananchi hao kuridhia mradi huu kwa kujiandaa kupima ardhi yao iliwaweze kuwa na hati miliki zao ambazo pamoja na mambo mengine zitasaidia kupunguza migogoro ya ardhi na kuwafanya kukopesheka kwenye taasisi za kifedha huku Bi. Georgia Ruhinda, mwanafamilia wa omukama akisisitiza azma ya rais Museveni ya kuyajenga makumbusho hayo.
Maoni ya wananchi wengi waliohudhuria Mkutano huo waliridhia kwa kauli moja juu ya ujengwaji wa makumbusho hayo huku baadhi yao akiwemo Pius Rumanyika, Henerico Theonest, Robert Leonard, Philibert Barebe Rwabazingo, Gipson Wilson Rumanyika, Sosteness Paulo Mongelle, Juhudi Theonest, George Chambwala na Janeth Mapinduzi Rumanyika ikiwa ni baadhi ya washiriki waliotoa maoni yao waliridhia juu ya ujengwaji wa makumbusho hayo huku mzee Pius Rumanyika akimshukuru sana Rais Museveni wa Uganda na kumuombea kwa mungu aishi maisha marefu kutokana na mchango wake kwa Tanzania.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.