Rais Magufuli atema cheche Uzinduzi wa Barabara ya Kyaka- Bugene
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, mnamo Novemba 07, 2017 amefanya ziara ya kikazi wilayani hapa iliyokuwa mahususi kwa ajili ya kuzindua rasmi barabara ya Kyaka- Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1. ikiwa ni sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene- Kasulo yenye kilometa 183.1
Barabara hiyo iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 81.597 ikiwa na daraja moja lilipo eneo la Mwisa inayo pia box makalavati 11 na makalavati pipe 132 fedha zilizogharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini, TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale alimweleza Rais Dkt. Magufuli kwamba kazi ya ukandarasi ilitekelezwa na kampuni ya CHICO huku mhandisi mshauri akiwa TECU.
“Mh. Rais ujenzi wa barabara hii umesimamiwa na Watanzania baada ya Kampuni kutoka India iliyokuwa imepewa tenda ya kusimamia ujenzi huo kushindwa kazi hali iliyopelekea Serikali kuamua kuifukuza kazi”, alisisitiza Mhandisi Mfugale huku akishangiliwa na Mh.Rais.
Kadhalika Mhandisi Mfugale alibainisha kwamba uamuzi wa kuifukuza kampuni hiyo umeisaidia serikali kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kwani hapo awali kampuni hiyo ilipangwa kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 4 lakini Watanzania ambao wamesimamia kazi hiyo mpaka ujenzi wa barabara hiyo kukamilika wakilipwa shilingi milioni 500 tu.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa(Mb) katika hotuba yake ya kumkaribisha Mh. Rais aliitaja barabara hii kuwa inauunganisha Wilaya ya Missenyi na Karagwe lakini ujenzi wake utakaoendelea kwenye maeneo mengine unalenga kufungua milango ya mawasiliano kati ya Tanzania na nchi jirani kama vile Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
Katika hotuba yake, Rais Magufuli aliwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Karagwe kuwa Serikali tayari imeiweka kwenye mpango wa ujenzi barabara ya Omugakorongo -Mulongo ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Rais Magufuli aliendelea kuwahakikishia wananchi wa Karagwe waliokuwa wakimsikiliza huku wakimshangilia juu ya dhamira ya serikali ya kuendelea kujenga kipande kilichobaki kutoka Bugene hadi Kasulo, Wilayani Ngara chenye urefu wa Km. 124 ili hatimaye kukamilisha jumla ya kilometa 183.1 zilizokusudiwa.
Katika hatua nyingine, mbunge wa Jimbo la Karagwe, Mh. Innocent Lugha Bashungwa alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kuiletea nchi yetu maendeleo lakini akamuomba Mh. Rais kuwasaidia wananchi wilayani hapa katika upatikanaji wa maji kero aliyoitaja kwamba ni kubwa wilayani hapa.
Kabla ya kujibu hoja hiyo Rais Dkt. Magufuli, aliwaagiza viongozi wilayani hapa kukaa na kuona namna wanavyosimamia sheria inayokataza wananchi kulima kwenye vyanzo vya maji kwani kwa mtazamo wake ni kweli wananchi wanapaswa kutokulima kwenye vyanzo vya maji lakini kumekuwa na utekelezaji usiozingatia ubinadamu hasa kwa wananchi wanaolima mazao ya kinga ya njaa kwenye maeneo hayo.
“Jamani najua kuna sheria za mazingira lakini tukiamua kuzisimamia sheria hizo kwa karibu sana wananchi watakosa mahala pa kuishi, kama wananchi wanalima kandokando ya mito pengine wakati wa kiangazi wakitekeleza sera ya hapa kazi tu waacheni walime kwani hawazuii maji yaliyoletwa na Mungu kutiririka.” Alisistiza Rais Magufuli
Katika kujibu hoja ya Mbunge Mh. Bashungwa, Rais Magufuli alisema anaijua vema kero ya maji wilayani hapa kuwa ni ya muda mrefu, ambapo kwa sasa serikali imeainisha miji 17 na Karagwe ikiwemo na tayari Serikali imepata mkopo wa fedha Dola Milioni 500 kutoka nchi ya India na Wilaya ya Karagwe imetengewa Dola milioni 70 kwajili ya ujenzi wa mradi wa maji.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Magufuli aliwapongeza Waandishi wa Habari kwa kazi kubwa wanayoifanya pia na vyombo vya habari kwa kufanya kazi kubwa ya kuwahaabarisha wananchi.
Ziara ya Rais, Dkt. Magufuli iliyoanza mnamo Novemba 06, 2017 mkoani wa Kagera, inatarajiwa kudumu kwa takribani siku nne (04) na inatajwa kuendelea Wilayani Missenyi katika kiwanda cha Kagera Sukari mapema kesho Novemba 8, 2017.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.