NEEMA YAWASHUKIA VIJANA, WANAWAKE NA WATU WENYE ULEMAVU.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa mara nyingine tena imeendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli la kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu.
Katika hatua hiyo ya hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Gogfrey Mheluka kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya, chini ya Mwenyekiti wake, Mh. Wallace Mashanda, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Godwin Kitonka pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango na Timu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya walishiriki zoezi la ugawaji wa hicho cha shilingi milioni 79 kwa makundi hayo matatu ambapo jumla ya vikundi 27 viligawiwa kiasi hicho cha fedha.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mgeni rasmi, Mh. Mheluka pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mh. Mashanda walitumia muda mwingi kulieleimisha kundi la vijana ambapo uzoefu unaonesha kuwa limekosa uaminifu katika urejeshaji wa mikopo jambo ambalo mgeni rasmi alilibainisha kwamba limekuwa likikwaza juhudu za utoaji wa mikopo kwa vikundi vingine kwani fedha hizo zinapaswa kutolewa kwa mzunguko.
“Napenda kutumia zoezi hili kuwaagiza mambo mawili; mosi ikiwa ni kuhakikisha fedha hizi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na pili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa kwa wakati”, alisisitiza Mh. Mheluka.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa makundi hiyo ambayo ni Basiliba Kashaya ambaye aliwakislisha kundi la walemavu, Alison Hamphrey kiongozi wa kundi la vijana na Demetria Saulo walimpongeza Mh. Rais Dkt. Magufuli kwa agizo lake hali kadhalika uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Mh. Rais.
Itakumbukwa kwamba mapema alipoingia madarakani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliagiza kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa mwezi na kuyagawa kwa uwiano wa asilimia 4 kwa wenye vijana, asilimia 4 kwa wanawake na asilimia 2 kwa vijana.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.