Neema Inakuja kwa Wakulima wa Kahawa Wilayani Karagwe.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mh. Dkt. Charles Tizeba leo tarehe 16/02/2018 amefika wilayani hapa na kutoa maagizo na maelekezo kadhaa kwa uongozi na menejimenti ya Wilaya ya Karagwe kwa ajili ya kutengeneza mikakati yenye lengo la kumuinua mkulima wa zao la kahawa wilayani hapa.
Mapema katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya Mh. Nyangele Makunenge alisoma taarifa kwa Mh. Waziri Dkt. Tizeba iliyoelezea hali ya chakula wilayani hapa ambapo taarifa hiyo ilianisha kwamba katika wilaya ya Karagwe, kwa kipindi hiki cha mwezi Februari 2018 mazao mengi yameanza kuvunwa na hiyo inaashiria hali ya chakula kuwa ni nzuri,maana chakula kipo cha kutosha na chakula cha ziada kinauzwa katika wilaya na mikoa ya jirani,na kadhalika bei za vyakula mbalimbali vijijini na sokoni ziko chini.
Aidha taarifa hiyo ya Kaimu Katibu Tawala Wilaya iliweza kubainisha changamoto ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.
“Kwa Wilaya yetu ya Karagwe mawakala wanaojihusisha na ununuzi na uuzaji wa pembejeo wameshindwa kunufaika na mfumo huu wa (Bulk) na hii imesababishwa na ukosefu wa mitaji na matumizi madogo ya mbolea”, iliainisha taarifa hiyo ya Kaimu Katibu Tawala.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Mh. Dkt. Tizeba alitumia wasaa huu kutoa maelekezo yake kwa wananchi na viongozi ya kuorodhesha mazao yote ya biashara na sio kuorodhesha tu zao la kahawa kama ambavyo imekuwa inafanyika kwa mujibu wa taarifa za viongozi.
Agizo jingine lilikuwa ni suala la kuiondoa miche ya kahawa inayodaiwa kuchokaa na badala yake wananchi wamehamasishwa miti hiyo ikatwe na kupandwa miche mipya ambapo uongozi wa Wilaya kupitia kwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji waliweza kumwahidi Mh. Waziri kwamba mpaka sasa Halmasahuri ya Wilaya Karagwe imeweza kuwekeza katika vitalu saba ambavyo vinatarajiwa kuzalisha miche ya kahawa takribani 1,000,000 kwa ajili ya wakulima wa kahawa.
Aidha Mh. Dkt. Tizeba aliuagiza uongozi wa Wilaya kushirikiana na taasisi ijulikanayo kama OLAM katika uratibu wa shughuli za uzalishaji wa zao la kahawa.
Kupitia kikao hicho Mh. Waziri aliweza kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya kuhakikisha kwamba anashirikiana kikamilifu na Mrajisi wa Kahawa wa mkoa ili kama kuna upungufu wa maafisa ushirika taasisi hiyo iweze kutoa wataalam kwa ajili ya kazi hiyo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.