MRADI WA SAMBAZA MBEGU FASTA WALETA NEEMA WILAYANI KARAGWE
Na Innocent E. Mwalo, Karagwe.
Uongozi na Wananchi Wilayani hapa, wameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Ukiriguru kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kusambaza mbegu bora za marando kwa ajili ya kilimo cha viazi vitamu iliyofanyika kupitia wanafunzi wa shule za msingi maarufu kama “Sambaza mbegu fasta” ambao umedumu kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja ambapo Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Maruku waliufadhili mradi huo.
Pongezi hizo zilitolewa hivi karibuni katika kikao cha pamoja kilichofanyika kwa ajili ya kuukabidhi mradi huu kwa Halmashauri ya Wilaya ambacho kiliwahusisha baadhi ya wakulima walionufaika na mradi huo kutoka katika kijiji cha Bujuruga, viongozi na wataalam kutoka katika Halmashauri ya Wilaya na wataalam kutoka katika taasisi hiyo iyoufadhili mradi huo.
“Napenda kuwakaribisha katika kikao hiki cha kuagana katika kukabidhi mradi huu ulioanza Mwezi Mei, 2017 hadi Mei 2018 na kweli tunawapongeza sana taasisi hii kwa utafiti mliofanya katika kutekeleza mradi huo kupitia wanafunzi wa shule za msingi na kwa kweli kupitia wanafunzi hawa, Elimu hii ilifikika kwa wazazi wao”, alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, ndugu Jackson Mwakisu.
Mapema katika taarifa yake, Mratibu wa Mradi huu ambaye pia ni Afisa Lishe katika Halmashauri hii Bi. Lustica Mgumba aliweza kuainisha faida kadhaa za mradi huu ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya wakulima wanaozalisha mbegu kutoka 87 ya hapo awali hadi kufikia zaidi ya wakulima 500 waliopo sasa huku idadi ya mbegu ikiongezeka kutoka 77400 hadi 300,000 ambavyo vilipandwa katika eneo la ekari 22.5.
Mafanikio mengine ni pamoja na mbegu kuendelea kusambaa wilayani toka kata nne anzilishi ambazo ni Bugene, Kihanga, Nyakakika na Nyakabanaga na kufikia kata 13 ambapo kwa sasa idadi ya kata zinazozalisha mbegu hizi ni kama vile Kanoni, Kituntu, Nyaishozi, Kiruruma, Kayanga, Nyakahanga, Igurwa, Kamagambo na Nyakasimbi.
Naye Emmanuel Kahesi ambaye ni Mkulima kutoka katika kijiji cha Bujuruga aliweza kubainisha mafanikio mengine ya zao hili ikiwemo suala uhakika wa upatikanaji wa chakula.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe Mh. Wallace Mashanda, alimshukuru sana Mtaalam huyo kutoka katika chuo cha Maruku ndugu Baker Chirimi huku akimhakikishia ya kwamba licha ya kwamba mradi huo unakabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya, jitihada zitaendelea kufanyika katika mipango ya Bajeti ya Halmashauri katika kila mwaka wa Fedha kwa ajili ya kuendeleza mradi huo wa muhimu kwa ajili ya usalama wa chakula.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.