MWENGE WA UHURU WAZINDUA MIRADI YA MABILIONI WILAYANI KARAGWE
Na Innocent Mwalo, KARAGWE.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, mwaka 2018, ndugu Charles Kabeho, hivi karibuni, amefanya shughuli za ukaguzi pamoja na uzinduzi wa jumla ya miradi 12 ya maendeleo yenye thamani ya Tsh. 3,175,124,660 wilayani hapa.
Miradi hiyo ilikuwa ni Klabu ya Wapinga rushwa iliyopo katika Shule ya Sekondari Rwambaizi kwenye Kata ya Kanoni, Shamba la migomba la Kituntu- Katembe la ndugu Mtawajibu Kajoki, miundombinu ya madarasa pamoja na bweni la wavulana kwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita katika shule ya sekondari Kituntu.
Kadhalika, miradi mingine ilikuwa ni ile ya mapambano dhidi ya malaria na huduma kwa mama wajawazito, watoto na wazee katika zahanati ya Kakiro, miradi ya mapambano dhidi ya dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI/VVU katika kata ya Ndama pamoja mradi wa kiwanda cha kusaga na kusindika unga wa mahindi cha Karimu Amri kilichopo mjini Kayanga.
Aidha, ratiba hiyo ilihusisha ukaguzi wa chuo cha kuzalisha mafundi stadi cha KDVTC, barabara za lami Mjini Kayanga, shule ya Msingi Kazoba, kikundi cha wanawake cha NDAWOSA, kikundi cha vijana cha Kihanga na maonesho ya mabanda ya UKIMWI, Malaria, Kupinga Rushwa na Madawa ya kulevya katika uwanja wa mkesha, Kayanga.
“Miradi yenu ni mizuri ila kwa upande wa mradi huu wa barabara za mjini Kayanga, Meneja wa TARURA hakikisha unawasiliana na mkandarasi ili katika kipindi hiki cha uangazi wa mradi huu, aweze kufanyia kazi changamoto ya maji kutuama katika barabara kwani maji ni adui mkubwa wa barabara”, aliagiza kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Katika mradi huo, wa ukaguzi wa barabara za mjini Kayanga, kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru, alionekana kumkaba koo fundi sanifu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini, TARURA ndugu Liberatus Rwazo kuhusu vipimo na mambo mengine katika ujenzi wa barabara hizo.
Kadhalika kiongozi huyo hakusita kuonesha furaha yake pamoja na kutoa pongezi kutokana na ufafanuzi mzuri na wa kitaalam uliotolewa na mtaalam huyo wa barabara wa TARURA.
Katika hatua nyingine, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru na ujumbe wake wa wakimbiza mwenge kitaifa waliweza kukagua na kupokea taarifa ya uendelevu wa Mradi wa Maji katika Kata ya Bugene katika kitongoji cha Rukajange uliwekewa jiwe la msingi mwaka 2017.
“Kwa mujibu wa maelezo yenu mradi huu unatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili na kwa mujibu wa taarifa yenu inaonesha kwamba shughuli za ujenzi wa mradi huu zimekamilika kwa 65% mpaka sasa jambo linalotia shaka kama mradi huu utakamilika kwa wakati, kwa hiyo nakuagiza Mkuu wa Wilaya kusimamia kikamilifu mradi huu na tupate taarifa ya kukamilika kwake mwishoni mwa mwezi”, aliagiza ndugu Kabeho.
Mradi mwingine ambao ujumbe huo uliukagua ni kikundi cha vijana selemala cha Kayanga uliozinduliwa mwaka 2017 ambapo baada ya hapo msafara ulielekea katika katika eneo la mkesha uwanja wa mpira wa Kayanga ambapo utambulisho ulifanyika.
Matukio mengine katika eneo hilo la uwanja wa mkesha yalikuwa ni kusomwa kwa risala ya utii, kukadhiwa kwa zawadi kwa timu bingwa Ligi ndogo ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu pamoja na kusomwa kwa Risala ya Utii.
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Elimu ni Ufungu wa Maisha; Wekeza Sasa kwa Manufaa ya Taifa Letu” yenye lengo la kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa Elimu kwa Taifa letu kuelekea Tanzania ya viwanda na uchumi wa kipato cha kufikia mwaka 2025.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.