“MWAROBAINI WA VYETI VYA KUZALIWA WAPATIKANA” – DED KITONKA
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, ndugu Godwin Kitonka ametoa maelekezo kwa wananchi na watendaji wilayani hapa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi la kuwaandikisha watoto wa umri wa miaka 0 – 5 iliwaweze kupata vyeti vya kuzaliwa.
Ndugu Kitonka aliyasema kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Chanika – Omurulama uliofanyika hivi karibuni ambapo alibainisha ya kwamba zoezi hili linalosimamiwa na Mamlaka ya Usajili na Ufilisi (RITA) kwa kushirikiana na timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya linarajiwa kuanza mnamo Oktoba 1, 2018.
“Zoezi hili litafanyika bila kulipa gharama yoyote hivyo basi viongozi, watendaji na wananchi kwa ujumla mnapaswa kutumia wasaa huu kuhakiksha watoto wetu hao wanapata vyeti hivyo”, alisema ndugu Kitonka.
Kwa upande mwingine ndugu Kitonka alitumia hadhira hiyo kuwakumbusha wanachi juu ya kampeni ya furaha yangu yenye lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao huku akibainisha ya kwamba kampeni hiyo itazinduliwa kwa ngazi ya mkoa hivi karibuni na kutekelezwa kwenye wilaya zote za mkoa wa Kagera kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kwa upande mwingine ndugu Kitonka aliwakumbusha wananchi juu ya suala la kupambana na udumavu wa akili kwa watoto wadogo ambapo alitoa wito kwa wazazi kuepuka kuwalisha watoto chakula cha aina moja ikiwa ni pamoja na kuwalisha matunda na kusisitiza juu ya kutekelezwa kwa agizo la Mkoa wa Kagera la kuhakikisha kila kaya inalima kwa wingi matunda kwa ajili ya lishe ya watoto
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.