‘WORLD VISION’ WAFANYA MAKUBWA SEKTA YA ELIMU WILAYANI KARAGWE
Na Innocent Mwalo, MWALO, KARAGWE.
Wananchi katika maeneo ya Kafunjo, Kilegete na Kajungu yaliyopo katika kata ya Kamagambo wilayani hapa wameushukuru na kuupongeza uongozi wa ‘World Vision’ kwa uamuzi wao wa kuisaidia jamii ya maeneo hayo katika ujenzi wa miundombinu ya Elimu.
Hayo yalisemwa na wananchi hao katika mikutano iliyofanyika kwenye maeneo hayo hivi karibuni, ambapo katika zoezi hilo viongozi wa juu wa Wilayani hapa akiwemo Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mh. Wallace Mashanda, Katibu TAwala wa Wilaya, Mh. Innocent Nsena na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Godwin Kitonka waliweza kukabidhiwa miradi hiyo na Meneja wa World Vision Kanda ya Kagera, Juliana Charles.
Katika maeneo hayo jumla ya Tsh. 305,961,250 zimetumika katika ujenzi wa miundombinu hiyo, ambapo mchanganuo wa gharama unaonesha kwamba jumla ya fedha zilizotolewa na shirika hilo lisilokuwa la kiserikali zilikuwa kiasi chaTsh. 278,768,250 ambazo zilifadhiliwa na Lorenz Honsen raia wa Ujerumani kupitia shirika hilo la ‘World Vision’ huku wananchi wakichangia kiasi cha Tsh. 27,193,000.
Ukaguzi huu uliofanyika katika miradi hiyo mitatu na kwa kiasi kikubwa ulionesha kukamilika kwa zaidi ya asilimia 99.
Kwa upande wa Shule ya Msingi Kajunju, Meneja wa Mradi huo alikabidhi miundombinu ya vyoo vya wavulana na wasichana, tenki la kuvuna maji ya mvua na madawati 100.
Mradi mwingine ambao miundombinu hii imekabidhiwa kwa uongozi wa Wilaya ilikuwa ni madarasa matatu, vyoo vya wavulana na wasichana, tenki la kuvuna maji ya mvua na madawati 150 katika shule ya Msingi Kilegete.
Aidha katika mradi wa tatu ambao ni Shule ya Msingi Kafunjo kumefanyika ujenzi wa madarasa mawili, vyoo vya wavulana na wasichana, tenki la kuvuna maji ya mvua na madawati 100.
Wakizungumza kwa tabasamu, baadhi ya wananchi wa maeneo hayo akiwemo Tauson Steven, aliyehojiwa katika shule ya Msingi Kajunju aliwasihi wananchi wenzake kwenye eneo hilo kuitikia wito wa viongozi wa wilaya waliotoa kwenye eneo hilo ambapo waliwaomba wananchi hao kuendelea kujitoa katika ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo ili kuwapunguzia adha wanafunzi ambao hapo awali kabla ya ujenzi wa shule za msingi za Kilegete na Kajunju walilazimika kutembea umbali mrefu kwwa ajili ya kufuata huduma hiyo ya Elimu kwenye Shule ya Msingi Kafunjo ambayo hata hivyo nayo inatajwa kuelewa na idadi kubwa ya wanafunzi ukilinganisha na miundombinu yake.
“Naagiza zifanyike kila aina ya jitihada ili mwakani (2019) shule hii ya Kajunju iweze kuandikisha wanafunzi”, alisisitiza Mh. Mheluka ambaye wakati wote alionekana kuifurahia kazi hiyo ya ‘World Vision’.
Naye Mkurugenzi Mtendaji, ndugu Kitonka na Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Mashanda kwa nyakati tofauti, waliungana na Mkuu wa Wilaya katika kuhamasisha wananchi hao kuchangia miradi hiyo huku wakisisitiza kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe katika Bajeti yake ya Miradi ya Maendeleo kwa mwaka 2018/2019 imetenga Fedha kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za wananchi katika ujenzi wa madarasa na nyimba za walimu katika Shule ya Msingi Kilegete.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya aliagiza wazazi kufanya jitihada ili watoto wao waweze kunywa uji mashuleni ukiwa ni mkakati wa kupunguza utoro mashuleni.
Historia ianaonesha kwamba ufadhili wa ‘World Vision’ katika ujenzi wa miundombinu hiyo unakuja kufuatia maombi ya mkoa na Wilaya yaliyotolewa mwaka 2016 baada ya serikali ya kutangaza mpango wa Elimu bila malipo, huku katika Shule ya Msingi Kafunjo jumla ya wanafunzi 710 wakiandikishwa kujiunga na darasa la kwanza na wengine 670 waliandikishwa kujiunga na Elimu ya darasa la awali hali iliyohamasisha wananchi na uongozi wa Wilaya kuanza jitihada za kujenga miundombinu ya shule katika maeneo ya Kilegete na Kajunju miradi ambayo kwa sasa imekamilika kwa zaidi ya asilimia 99.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.