WASICHANA 4005 KUPATIWA CHANJO YA KUZUIA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI WILAYANI KARAGWE
Na Innocent Mwalo, KARAGWE.
Uongozi Wilayani Karagwe, kupitia kikao chake cha Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi, PHC kilichofanyika hivi karibuni katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, chini ya Mwenyekiti wake ambaye ndiye Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka, kimeazimia kwa kauli moja kufanya kila linalowezekana ili kuweza kufikia malengo ya kutoa chanjo kuzuia saratani ya mlango wa uzazi kwa jumla ya wasichana 4005 wenye umri wa miaka 14 kwa asilimi 100.
Maazimio hayo yalifikiwa kupitia kikao hicho kilichokubaliana kutumia njia zote ikiwemo vyombo vya habari katika kuhamasisha jamii ya watu wa Karagwe ili kuwezesha wasichana hao waliokusudiwa katika kushiriki chanjo hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Libamba Sobo, kwenye kikao hicho, itafanyika kwa awamu kadha, ambapo kwa awamu ya kwanza, chanjo hii itatekelezwa kwenye wiki ya chanjo kitaifa itakayofanyika kuanzia Aprili 23, 2018 hadi 30 Aprili, 2018.
“Hadi sasa Wilaya imepokea chanjo za kuzuia saratani ya mlango wa kizazi dozi 2000 ambazo hazitoshelezi mahitaji ya walengwa na kwa mantiki hiyo zoezi hili litafantika kwa awamu kadhaa ili tufikie lengo la wasichana waliokusudiwa”, alinukuliwa Dkt. Sobo akifafanua kupitia kikao hicho.
Nae Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Mheluka aliwaahidi wajumbe wa kikao hicho ya kwamba atafanya jitihada zote ili kushirikiana na kitengo cha chanjo na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya kwa ujumla kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa mafanikio makubwa.
Naye Mratibu wa chanjo kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, Modester Kibona alibainisha baadhi ya sababu zinazosababisha saratani ya mlango wa kizazi ikiwa ni pamoja na suala la kuanza kujamiana katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuwa na ndoa za mitala, kuzaa watoto wengi na uvutaji wa sigara.
Aidha, Modester alibainisha dalili za ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kutokwa damu katikati bila mpangilio au kutokwa damu baada ya kujamiana, maumivu ya mgongo, miguu na kiuno.
Dalili nyingine zilizotajwa zilikuwa ni suala la kuchoka, kupungua uzito, kupungikiwa hamu ya kula, kutokwa uchafu kwenye uke wa maji maji, uliopauka, rangi, kahawia au wenye damu pamoja na kuvimba miguu.
Ikumbukwe kwamba chanjo hii ambayo itafanyika bila malipo yoyote itatolewa kwa awamu nne, ambapo awamu ya kwanza ya mwaka 2018 itawahusisha wasichana wenye umri wa miaka kumi na nne, awamu ya pili ya mwaka 2019 itakuwa wa wasichana wa miaka tisa mpaka 14 huku awamu ya tatu na mwisho ya mwaka 2020 na kuendelea itahusisha wasichana waliofikisha umri wa miaka 09.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.