MRADI WA KIHISTORIA KUMALIZA KERO YA MAJI KATA YA IHANDA NA CHONYONYO
Na Innocent E. Mwalo.
Mradi wa kihistoria wenye uwezo wa kuzalisha kiasi cha lita 60,000 za maji ya bomba kwa siku moja na kuhudumia kaya takribani 5,000 katika vituo vinne kwenye kata za Ihanda na Chonyonyo umezinduliwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya, Mh. Godfrey Mheluka huku ukielezwa kuwa utapunguza ukali wa tatizo la maji katika kata hizo.
Mradi huu ambao upo katika utekelezaji wa awamu ya kwanza umejengwa na Shirika la Mavuno linalofanya kazi zake Wilayani hapa kwa ushirikiano na Wahandisi wasio na Mipaka kutoka katika nchi za Sweden na Ujerumani.
Mradi huu unaotarajiwa kuwahudumia wananchi katika vituo vinne ambavyo ni Rukole, Ihanda, Chonyonyo na Kakoma na umeelezwa kujengwa kwa jumla kiasi cha fedha cha zaidi ya Tsh. 627,000,000/= ikiwa ni msaada kutoka kwa wahisani, shirika la mavuno na michango mingine kutoka serikalini, kwa wadau wa maendeleo na Jamii kwa ujumla.
Awali, Meneja Mradi huu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mavuno Project, Charles Bahati alibainisha baadhi ya faida watakazopata wananchi wa maeneo haya ya kata za Ihanda na Chonyonyo ambapo mradi huu unatekelezwa; kubwa ikiwa ni kuwapunguzia wananchi kero ya kutumia muda mwingi kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kwa ajili ya kutafuta huduma ya maji lakini pia kuwa na uhakika wa kupata maji kwenye maeneo hayo muda wote.
“Katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huu, shughuli zilipangwa kufanyika ni pamoja na kujenga maabara ya kisasa kwa ajili ya shughuli za upimaji wa maji, kujenga mtambo wa kuchuja maji, kujenga vituo vya kuchotea maji na kujenga mtandao wa kuchotea maji”, ilisisitizwa na Bahati kupitia taarifa yake.
Mhandisi Anders Ijungman, mhandisi kiongozi kutoka katika kundi la Wahandisi wasio na mipaka ambao ndio watekelezaji wa mradi huu aliwaambia wananchi wa Karagwe kupitia umati wa watu na viongozi waliokuwa wamekusanyika katika viwanja vya Shule ya Shule Sekondari ya Mfano ya Mavuno juu ya dhamira yao ya kuendelea kufanya ufadhili zaidi katika miradi ya maji wilayani hapa ambapo kwa namna moja alisifu jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza kwa vitendo sera ya viwanda iliyopelekea upatikanaji wa malighali zote zilizohitajika wakati wa utekelezaji wa mradi huu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Wallace Mashanda licha ya kuwashukuru wote waliofadhili ujenzi wa mradi huu huku akieleza kwamba mradi huu umetekelezwa kwenye maeneo ambayo ni sahihi kutokana na shida kubwa wanayopata wananchi wa vijiji vya Ihanda na Chonyonyo juu ya kero ya maji; alitoa wito kwa wananchi juu ya kuitunza miundombinu ya maji iliyojengwa kwenye maeno hayo na kusisitiza kwamba ni lazima wananchi wajue kuwa suala la matengenezo na uendeshaji wa mradi kwa ujumla kuwa litakuwa ni jukumu la wananchi wenyewe wanaonufaika na mradi huu.
Shirika la Mavuno ni moja kati ya taasisi zinazofadhili juhudi za ujenzi wa miundombinu ya maji kuanzia mwaka 1995 ambapo licha ya kuanza kama mpango wa kuvuna maji kwenye familia 582 kwa sasa umekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuzisaidia takribani taasisi 33 katika kuzijengea visima vinavyozalisha wastani wa lita za maji 45,000 – 100,000 wananchi 3700 wakitajwa kunufaika na mradi huo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.