MKUU WA MKOA WA KAGERA AFANYA ZIARA YAKE YA KWANZA WILAYANI KARAGWE NA KUTOA MAAGIZO NA MAELEKEZO KWA WANANCHI NA WATENDAJI.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mh. Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, hivi karibuni amefanya ziara yake ya kwanza wilayani hapa yenye lengo la kujitambulisha ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt John Pombe Joseph Magufuli mnamo 28/07/2018 kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Meja Jenerali (Mstaafu) Salim Kijuu ambaye amestaafu.
Katika ziara yake hiyo ambayo imedumu kwa takribani siku moja, Mh. Gaguti amekutana na wakulima wa kahawa na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS), Bodi ya Maendeleo ya Kahawa (KDCU), wadau, watumishi na wananchi kwa ujumla, ziara ambayo imefanyika kwenye maeneo matatu tofauti ikiwemo Ukumbi wa ANGAZA, Kituo cha Afya Kayanga na kiwanda cah kukobolea kahawa cha KADERES.
Akiwa katika Ukumbi wa Angaza, Mh. Gaguti aliwapongeza wakulima wa kahawa kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam wa kilimo na hivyo kuwawezesha kulima kahawa ambayo aliitaja kuwa na ubora wa kimataifa kwa msimu wa kilimo wa 2017/2018 lakini akatoa wito kwa wananchi wote kuunga mkono mfumo uliokubaliwa na serikali katika ununuzi na uuzaji wa kahawa huku akitoa wito kwamba serikali haina lengo la kuwaletea hasara mwananchi katika ununuzi wa kahawa katika msimu huu unaoendelea.
Aidha, Mh. Gaguti alitumia wasaa huo kuwahakikishia wananchi kuwa tayari serikali imeshatoa takribani shilingi bilioni nne zitakazotumika kuwalipa wakulima wa kahawa wanaodai mauzo yao ya kahawa kwa msimu huu huku akisisitiza kwamba kiasi kingine cha shilingi bilioni tatu kitapokelewa hivi karibuni kwa ajili ya kukamilisha malipo ya wakulima hao.
“Aidha naagiza ya kwamba wakati wa kulipa malipo hayo kipaumbele kinapaswa kuwa ni kumlipa mkulima aliyetangulia kupeleka kahawa zake kwenye vyama vya msingi na nitafuatilia kuona kama kuna ukiukwaji wa agiza langu hili na kuchukua hatua stahiki”, alisema Gaguti.
Maagizo mengine aliyoyatoa kwa wanchi na watendaji ilikuwa ni suala la ulinzi na usalama ambapo aliagiza kwamba suala hili ni la kila mmoja ndani ya wilaya hii huku Mh. Gaguti akienda mbali zaidi kwamba wananchi wanapaswa kutoa taarifa juu ya masuala yote yanayohatarisha amani kwenye maeneo kote wilayani hapa.
Aidha, aliagiza suala la wajasiliamali wadogo kuchukuliwa kwa uzito unaostahili huku akiahidi kwamba kwa sasa kuna mkakati wa mkoa wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na kamati usalama na maadili kwa waendesha bodaboda ili iwe rahisi kuwajibishana wao wenyewe pindi linapotokea tatizo miongoni mwao.
Maagizo na maelekezo mengine ilikuwa ni kwamba wananchi wote wilayni hapa an mkoani Kagera kwa ujumla kuchukua tahadhali juu ya ugonjwa wa Ebola unaotajwa kuzuka katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuwataka wanachi kusoma vipeperusha mbali mbali juu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huu ambavyo vipeperushi hivyo vinapatikana katika Hospitali, vituo vya afya na zahanati wilayani kote.
“Mkoa huu ni moja kati ya mikoa mitano ambayo imekumbwa na tatizo la udumavu kwa watoto kutokana na kukosekana kwa lishe bora na hivyo basi nitoe wito kwenu wananchi wenzangu kuzingatia suala la mlo kamili kwa ajili ya kuepuka tatizo hili na siku nyingine ikifanyika tathmini basi mkoa wetu usitajwe tena katika orodha hiyo”, alisisitiza Mh. Gaguti.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huu walimweleza Mh. Gaguti kufurahishwa na ujio wake wilayani hapa ambapo kwa upande wake Bi. Akwilina Francis mbali na kumshukuru kiongozi huyo kwa ufafanuzi wake wa kwamba malipo ya kiasi cha shilingi 1,000/= yanayotolewa sasa na KDCU ni sehemu tu ya gharama ambaza mwananchi atalipwa baada yam nada wa kahawa kufanyika na wanunuzi wa kahawa kununua zao hilo kwenye mnada utakaofanyika mjijni Moshi.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa alifika kwenye kituo cha Afya Kayanga na kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo kuwajulia hali wagonjwa walikuwa wanapata matibabu katika kituo hicho.
Ziara ya Mh. Gaguti ilimalizika kwa kutembelea kiwanda cha kokoboa kahawa cha KADERES ambapo Mkuu wa Mkoa licha ya kusifu jitihada zilizofanywa na mwekezaji katik kiwanda hicho aliahidi kufika tena katika eneo hilo kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa shughulu mbalimbali za maendeleo kwenye eneo hilo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.