SERIKALI YATOA MSAADA WA PIKIPIKI KWA MAAFISA ELIMU KATA ILI KUBORESHA UTOAJI WA ELIMU
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, hivi karibuni amekabidhi pikipiki 23 ambapo kila Afisa Elimu Kata kutoka katika kata zote 23 za Wilaya ya Karagwe amegawiwa pikipiki moja kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya taaluma na elimu kwa ujumla kwenye eneo lake.
Awali, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Bi. Upendo Rweyemamu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya aliwasilisha taarifa juu ya ugawaji huo wa pikipiki kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambapo pamoja na mambo mengine aliwaagiza Maafisa Elimu Kata hao kuzingatia mambo kadhaa katika matumizi ya pikipiki hizo ikiwemo kwa kila mtumiaji wa pikipiki kuwa na leseni inayomruhusu kutumia chombo hicho cha moto.
Maelekezo mengine kwa mujibu wa Bi. Upendo ni kwamba kila mtumiaji anapaswa kusoma kwa makini maelekezo ya matumizi sahihi ya pikipiki yaliyotolewa kwenye kitini cha maelekezo yalikuja pamoja na pikipiki, pikipiki kutumiwa kwa madhumuni ya kufanya ufuatiliaji katika shule zilizoko katika kata husika ikiwa ni pamoja na pikipiki kutumika ndani ya kata husika tu na ikilazimika kwenda nje ya kata kwa shughuli za kikazi iliamriwa kwamba mtumiaji anapaswa kuomba kibali.
Aidha, Bi. Upendo alisisitiza kwamba pikipiki itumiwe na Afisa Elimu Kata husika tu huku akisisitiza kwamba hairuhusiwi mtu mwingine yeyote kutumia pikipiki hizo.
“Masharti mengine ni kwamba pikipiki itumike muda wa siku za kazi tu na endapo italazimika kutumika muda ambao sio wa kazi mtumiaji anapaswa kuomba kibali kwa Mkurugenzi Mtendaji na sharti jingine ni kwamba pikipiki hizo zinapaswa zisitumike kwa shughuli za biashara”, alisisitiza Bi. Upendo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Mh. Gaguti aliishukuru Serikali Kuu kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hasa katika kuwahudumia wananchi na akawasisitiza watumishi hao waliopatiwa vitendea kazi hivyo kuzingatia masharti yote yaliyotowa na serikali hususani juu ya waraka wa matumizi ya magari na vifaa vya moto vya serikali.
Naye Bi. Rosemary Kisang’a ambaye ni Afisa Elimu kata ya Ndama kwa niaba ya maafisa Elimu wote waliokabidhiwa pikipiki hizo aliishukuru serikali kwa msada huo huku akiahidi ya kwamba wataenda kuzitendea haki pikipiki hizo kwa kuchapa kazi kwenye maeneo yao ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Serikali imetoa jumla ya pikipiki 23 ikiwa ni mpango wake katika kutekeleza mpango wa Serikali kupitia program za EQUIP – T na LANES ambapo lengo la pikipiki hizo ni kwa ajili ya kwenda kusaidia kutekeleza majukumu ya maafisa Elimu Kata katika kusimamia shughuli za kielimu katika kata zao.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.