Na, Geofrey A.Kazaula
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco E. Gaguti amefanya ziara ya Siku moja Wilayani Karagwe ili kujionea miundombinu ya Shule mbalimbali na uwezo wa Shule hizo kuwapokea wanafunzi wa Kidato cha kwanza mwakani.
Akiwa Wilayani Karagwe, Kiongozi huyo ameitembelea Shule ya Sekondari inayojengwa kwa nguvu za wananchi katika Kata ya Rugera na kujionea jitihada kubwa zilizofanywa na wananchi katika ujenzi wa Shule hiyo ambapo kwa sasa tayari majengo mawili yenye jumla ya vyumba sita yapo katika hatua ya uezekaji.
Awali akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa Sekondari hiyo, Diwani wa Kata ya Rugera Mh, Dawson P.Byamanyirwohi, alifafanua kuwa ujenzi huo ulianza zikiwa ni nguvu za wananchi baada ya watoto kukosa Shule ya Sekondari kwa muda mrefu na kusababisha Kata hiyo kukosa wataalam wazawa kwa muda mrefu.
‘‘Baada ya kuona watoto wetu wanateseka kwa muda mrefu tuliamua kuunganisha nguvu na kuhakikisha Kata yetu inakuwa na Sekondari kwani kwa sasa watoto wanalazimika kwenda Kata ya Ndama ambapo nimbali sana hivyo wachache humudu kwenda huko nabado huishia kufanya vibaya’’ alisema kiongozi huyo.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Ndg, Godwin M.Kitonka alieleza kuwa nguvu hizo za wananchi zilizokwisha tumika ni kubwa na Halmashauri kupitia Mapato yake ya ndani lazima iangalie namna ya kuwezesha ili kufanikisha ujenzi huo.
‘‘ Nguvu hizi ni kubwa sana na lengo la wananchi ni kusaidia watoto wetu kupata haki yao ya elimu kwa urahisi, sisi kama Halmashauri lazima tuangalie kupitia Mapato yetu ya ndani na mna ya kuwezesha wananchi hawa kufikia lengo lao la kuwa na Shule ya Sekondari katika Kata yao’’ alisema Kiongozi huyo.
Baada ya kukagua na kusikiliza taarifa mbalimbali, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco E. Gaguti alieleza kuridhishwa na ubora wa ujenzi uliokwisha fanyika na kuahidi kuwa atakuwa mlezi wa Shule hiyo na kuhakikisha inaanza mwakani ili kuwasaidia watoto kupata elimu karibu.
‘‘ Ujenzi uliofanyika ni wa kiwango cha juu na mimi najipa ulezi wa Shule hii ili niisimamie na kuhakikisha mwakani inaanza, nitakuwa tayari kutoa ushirikiano wangu kwenu na pale mnapo nihitaji nijulishe, nitafika ili tufanye kazi kwa pamoja’’ alisema kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa aliutaka uongozi wa Wilaya kuhakikisha mazingira bora kwa wanafunzi wanaotarajia kuanza kidato cha kwanza mwakani.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Kayanga, kiongozi huyo aliagiza kuwa hatua za haraka zifanyike ikiwa ni pamoja na kuendesha harambee ili kuhakikisha miundombinu ya shule hiyo inakuwa rafiki kabla ya watoto kuanza mwakani na alisisitiza kuwa ashirikishwe katika kila hatua kwani atakuwa tayari na atatoa ushirikiano kwa kuwashirikisha pia wadau mbalimbali wa maendeleo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.