MAFUNZO YA UGONJWA WA FISTULA YA UZAZI YATOLEWA KWA BARAZA LA MADIWANI WILAYANI KARAGWE.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Shirika linalojulikana kwa jina la Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT) hivi karibuni limeendesha mafunzo ya ugonjwa Fistula ya uzazi kwa Baraza la Madiwani wilayani hapa ambapo kwa namna moja ama nyingine mafunzo hayo yalikuwa ni mahususi kwa ajili ya kuwafahamisha waheshimiwa madiwani maana, sababu,madhara, tiba na kinga ya fistula ya uzazi huku ikielezwa ya kwamba takwimu zinaonesha ya kwamba mkoa wa Kagera unashika nafasi ya tano kitaifa katika mikoa inayoongozwa kukumbwa na tatizo hili.
Mafunzo haya yaliyowezeshwa na ndugu Clement Ndahani ambaye ni Meneja mradi wa Fistula kutoka katika shirika hilo akishirikiana na daktari wa magonjwa hayo Dkt. Adjustus Haule yalifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ambapo licha ya kuwafamamisha madiwani waheshimiwa ukubwa wa tatizo la fistula duniani, nchini Tanzania, mkoani Kagera na wilayani Karagwe kwa ujumla, wataalam hao waliweza kuelezea nafasi ya waheshimiwa madiwani katika kutokomeza fistula Tanzania na wilayani Karagwe kwa ujumla.
“Fistula ya uzazi ni tundu lisilo la kawaida linalotokea kati ya kibofu cha mkojo na uke au njia ya haja kubwa na uke au vyote kwa pamoja”, alieleza ndugu Ndahani wakati wa uhudhurishaji wa mada hiyo.
Aidha Dkt. Haule alizitaja sababu kuu za ugonjwa huu ikiwemo suala la uchungu pingamizi kwa muda mrefu, upasuaji, mionzi ya matibabu ya saratani sehemu ya nyonga au shingo ya uzazi na saratani ya shingo ya uzazi na ile ya kibofu cha mkojo Uharibifu wa kibofu na mfumo wa njia za mkojo.
Kupitia mafunzo hayo, Dkt. Haule aliweza kuyataja madhara ya ugonjwa huu ikiwemo uharibifu/majeraha kwenye njia ya haja kubwa, kujeruhi/kuumiza mishipa ya fahamu/nerve demage na kuharibu misuri ya njia za uke
Kwa maelezo ya Dkt. Haule, madhara mengine ni pamoja na kutokwa na mkojo au haja kubwa ama vyote kwa pamoja mfululizo bila kuwa na uwezo wa kuzuia Kunyanyapaliwa na kujinyanyapaa, msongo wa mawazo/sonona, kushindwa shiriki vema shughuli za kiuchumi, kuachwa na wanaume na kukosa shughuli za kijamii na kiroho kwa gonjwa hao wa Fistula.
Katika hatua nyingine, wataalam hawa waliweza kugusia namna matibabu ya Fistula yanatolewa kwa njia ya upasuaji ambapo ilielezwa kwamba matibabu ya Fistula nchini Tanzania yanatolewa bure bila malipo huku mgonjwa akilipiwa nauli ya kwenda na kurudi na kwa upande wa gharama zote za kula na kulala mgonjwa awapo hospitali zinalipiwa na tasisi hiyo.
Waheshimiwa madiwani ni lazima tukubaliane juu ya ukubwa wa tatizo hili la Fistula linalosumbua nchi zinazoendelea na ukweli ni kwamba tatizo hili halipo tena kwenye nchi zilizoendelea”, alisisitiza Dkt. Haule.
Huku akirejea baadhi ya takwimu, Dkt. Haule alibainisha ya kwamba takribani wakina mama million mbili wanaishi na fistula duniani huku kila mwaka kati ya wakina mama 50,000 hadi 100000 wanapata fistula na kati ya wakina mama wanaopata fistula ni 20,000 tu ndio wanaotibiwa.
“Fistula ipo nyingi zaidi Asia na Afrika kusini mwa jangwa la sahara na nchini Tanzania takribani wanawake 3000 hupata fistula kila mwaka na kati yao wanaotibiwa hawazidi 1400 hivyo zaidi ya nusu hubaki bila kutibiwa na kwa kweli kuna mrundikano wa wanawake wanaoishi na fistula Tanzania”, alibainisha Dkt. Haule.
Dkt Haule aliendelea kutanabaisha ya kwamba sasa wastani wanawake wanaotibiwa fistula Tanzania wameishi na fistula kwa miaka 8 huku mwanamke aliyeishi na fistula muda mrefu zaidi amekaa na fistula kwa miaka 66 huku akiitaja tasisi ya CCBRT ya kwamba inaendelea kutibu wanawake waliokaa na fistula muda mrefu.
“Hii inaamanisha kuwa bado elimu ya fistula na matibabu yake hayajawafikia watu”, alisisitiza Dkt. Haule.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.