“SERIKALI INAZIFANYIA KAZI CHANGAMOTO ZENU”, ASEMA MHELUKA
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka ametumia maadhimisho ya Mei, Mos ambayo kwa mwaka huu, wilayani hapa yamefanyika katika eneo la uwanja wa Changarawe mjini Kayanga, kuwasisitiza wafanyakazi na watumishi wote wa Umma wilayani hapa kwamba serikali inazifanyia kazi changamoto zao zote ili kuboresha maslahi yao.
Mh. Mheluka aliyasema haya wakati alipokuwa akijibu risala iliyosomwa kwake na Katibu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania, TUCTA Wilayani hapa, Edmund Sosteness ambayo pamoja na mambo mengine, risala hiyo iliibua changamoto kadhaa wa kadhaa zinazowakumbwa watumishi wa umma ikiwemo suala la kupoteza ajira alimaarufu ‘kutumbua majipu’ iliyotokana na ajira hewa, vyeti feki, Elimu ya darasa la saba na watendaji wasio waaminifu kuondolewa kazini na kupelekea kuleta adha kwao na familia zao pia.
Aidha risala hiyo iliibua changamoto nyingine kama vile mishahara duni kwa watumishi, malimbikizo ya mishahara/madai na zoezi la uhakiki wa watumishi kuwa la kudumu.
“Ndugu mgeni rasmi ni dhahiri kabisa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kushusha bei za vifaa vya ujenzi ili kumkomboa mtanzania aliye chini kiuchumi ili kuweza kumudu gharama za ujenzi wa nyumba bora na za kisasa lakini ukweli ni kwamba gharama hizo zipo juu, mfano mfuko wa simenti uliouzwa sh.15,000 mwezi Januari mwaka huu, kwa sasa unauzwa kati ya Tsh 19,000/= na 20,000/=”, alisisitiza Sosteness kupitia risala hiyo.
Changamoto nyingine iliyoibuliwa na TUCTA ilikuwa ni suala la malalamiko ya kukataliwa kwa uhamisho kwa watumishi walio chini ya Halmashauri hususani Idara ya Elimu ambapo watumishi hawa wamekuwa wakiruhusiwa kuhama kwa kigezo cha kubadilishana na walimu kwenye maeneo wanayohamia jambo ambalo linaleta changamoto kubwa kwa watumishi wa kada hiyo.
“Serikali inazifanyia kazi changamoto zote zilizotolewa na viongozi wenu kupitia risala hii na naomba ieleweke kwamba Mkuu wa Wilaya hawezi kutangaza kupandishwa kwa mishahara ya watumishi lakini nazidi kuwahakikishia baadhi ya changamoto mlizowasilisha kwangu tayari serikali imezifanyia kazi na nyingine zinafanyiwa kazi na kwa hiyo nitoe wito kwenu nyote kuendelea kuchapa kazi huku mkiamini serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli inazifanyia kazi changamoto zenu zote kama mlivyoeleza kwenye risala yenu”, alisema Mh. Mheluka.
Aidha kuhusu suala la uhamisho wa watumishi, Mh. Mheluka aliwaeleza washerehekeaji kwamba serikali ilisitisha zoezi hilo kwa muda na sasa baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki kwa kiasi kikubwa serikali imewaruhusu watumishi kuendelea kushughulikia masuala ya uhamisho kwa mujibu wa taratibu, kanuni, miongozo na sheria katika utumishi wa umma.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya aliwatunuku zawadi zaidi ya watumishi 20 waliotajwa kuwa watumishi bora kwa mwaka 2018 kwenye maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Kuunganishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Kulenge kuboresha Mafao ya Mfanyakazi”
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.