MADIWANI WAWILI WA CHADEMA WAHAMIA CCM
Geofrey A. Kazaula, KARAGWE
Madiwani wawili kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamejiuzulu nafasi zao za udiwani pamoja na kuachia nyadhifa nyingine ndani ya chama chao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ndugu Godwin M. Kitonka amefafanua kuwa amepokea barua za kujiuzulu udiwani na nyadhifa zao madiwani hao wawili ambao ni Mh. January Joachim wa Kata ya Ihanda pamoja na Mh. Norvart Kishenyi wa Kata ya Chonyonyo.
“Ni kweli nimepokea barua za kujiuzulu kwa madiwani hao na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo tarehe 7/9/2018 majira ya saa 4:00 asubuhi”, alisema ndugu Kitonka.
Aidha amefafanua kuwa baada ya kupokea barua hiyo, ametoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Wallace Mashanda ili kwa mujibu wa kanuni, Mwenyekiti huyo amwandikie barua Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kumjulisha juu ya jambo hilo.
Kwa maelezo ya ndugu Kitonka tayari nakala ya barua hiyo imetumwa kwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza uwepo wa nafasi wazi katika kata hizo.
Kuhusu nafasi zao za udiwani kwa sasa, ndugu Kitonka amefafanua kuwa mara baada ya kujiuzulu nafasi zao za udiwani na majukumu yao katika chama chao cha awali tayari wamepoteza sifa ya kuwa madiwani.
“Ili kuwa Diwani ni lazima mtu atokane na chama cha siasa na hivyo mtu kuhama chama anapoteza sifa ya kuwa diwani na kwamba suala la kuhama chama ni la kikatiba kwani mtu anaruhusiwa kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa”, alifafanua kiongozi huyo ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi kwa ngazi ya Halmashauri.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.