WANANCHI KARAGWE WATAKIWA KUHAKIKISHA WATOTO WAO WANAHUDHURIA CHANJO
Na, Geofrey A.Kazaula Karagwe
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Ndg, Godwin M.Kitonka amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la chanjo ili kuhakikisha watoto wao wanapatiwa kinga ya magonjwa mbalimbali.
Hayo yamebainika katika kikao kazi kilicho washirikisha Viongozi na wataalam mbalimbali chini ya Shirika la USAID Mradi wa MCSP.
Ndugu Kitonka amesisitiza kuwa zoezi la chanjo ni muhimu na inabidi lifanyike kwa ushirikiano Mkubwa kwa kuwashirikisha Wah, Madiwani, wananchi pamoja na wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii yaani – WAJA.
“Kuna haja ya kuendesha zoezi hili kwa ushirikiano Mkubwa sana ili kuhakikisha Wilaya ya Karagwe inafikia malengo ya Wizara ya Afya ifikapo Desemba 2018’’ alifafanua Kiongozi huyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mh, Godfrey Mheluka ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao kazi hicho, alisisitiza juu ya kuwashirikisha viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ofisi yake ili kuhakikisha zoezi la chanjo linaendeshwa kwa ufanisi na kufikia malengo ya Taifa.
Aidha kiongozi huyo aliwataka watumishi wanao husika na kuratibu zoezi la chanjo kuhakikisha wanawasiliana na Ofisi yake moja kwa moja hasa pale wanapo kutana na changamoto mbalimbali ili awasaidie kupata utatuzi wa changamoto hizo ambazo zingeweza kukwamisha zoezi la chanjo.
‘’Natoa wito kwa watumishi wanaohusika na zoezi la chanjo kuacha tabia ya kujifungia na changamoto mbalimbali na badala yake wafike fisini kwangu ili kwa pamoja tutatue changamoto hizo na kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma kama yalivyo malengo ya Serikali ya awamu ya tano’’ Alisisitiza kiongozi huyo.
Kwa upande wake Afisa Chanjo Kutoka Shirika la USAI – MCSP Ndg, Raphael Nshunju alifafanua kuwa lengo la kukutanisha wataalam pamoja na viongozi ni kutaka kusisitiza juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto hasa Katika Wilaya ya Karagwe ili kuhakikisha Wilaya inafikia malengo ya Wizara katika utoaji wa chanjo.
Bwana Nshunju aliongeza kuwa ili kuhakikisha zoezi la chanjo linafanyika kwa ufanisi inabidi Halmashauri kushirikiana na Kamati za Maendeleo za Kata ili kupata takwimu sahihi za watoto ambao hawajapatiwa chanjo mbalimbali na kuhakikisha wanapatiwa ikiwa ni pamoja nakutumia vyombo vya Habari kutoa elimu kwa uuma juu yya umuhimu wa chanjo kwa watoto.
Halmashauri ya Wilaya ya Karawge inaundwa na Kata 23 ambapo zoezi la chanjo linaloendelea linatarajiwa kufanyika katika Kata zote baada ya viongozi na wataalam kukubaliana kutatua changamoto mbalimbali ambazo zingezorotesha zoezi la chanjo kwa watoto katika maeneo hayo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.