MKURUGENZI MTENDAJI AWAWEKA “KITI MOTO” WATUMISHI WA MAKAO MAKUU.
Na Innocent E. Mwalo.
Ikiwa zimepita siku chache toka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kufanya uteuzi wa Wakurugenzi wapya 41 kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa nchini na kuwabadilisha baadhi ya vituo vya kazi Wakurugenzi kadhaa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mh. Godwin Kitonka mmoja kati ya Wakurugenzi wachache waliobakizwa katika vituo vyao vya kazi, hivi karibuni aliitisha kikao cha watumishi wote wanaofanya kazi makao Makuu ya Wilaya kwa lengo la kuwapa maagizo na maekelezo kadhaa yenye lengo la kuimarisha uwajibikaji katika majukumu yao na ajenda kuu ikiwa ni suala la ukusanyaji wa mapato.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Kitonka (ambaye wakati wote alipokuwa akizungumza alikuwa akishangiliwa na watumishi hao) alitumia muda mwingi kuwakumbusha na kuwasisitiza watumishi hao majukumu yao ya kila siku huku akiwaasa kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano inayosisitiza juu ya kukusanya mapato kwa ajili ya kufanikisha azma ya serikali ya kuwahudumia wananchi wanyonge.
Katika kusisitiza suala hilo la ukusanyaji wa mapato, Mh. Kitonka aliwaagiza Wakuu wa Idara/Vitengo vyote vya Halmashauri kuondoa dhana ya kwamba suala hilo ni jukumu la Idara ya Fedha na Biashara pekee na kupitia kikao hicho alitoa agizo kwa Idara/Vitengo vyote kuwa na orodha ya vyanzo vya kukusanya mapato kwenye maeneo yao na kukusanya mapato hayo.
“Mambo mengine ambayo tunapaswa kuyatekeleza kwa nguvu zote ni usimamizi na ufuatililiaji wa miradi inayotekelezwa ambapo Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji kwa kushirikiana na Idara yenye mradi husika mnapaswa kuifuatilia kwa karibu miradi ili iweze kutekelezwa kwa kuzingatia ‘value of money’ thamani ya miradi hiyo”, alisema Mh.Kitonka.
Aidha katika kikao hicho, Mh. Kitonka aliwasisitiza Wakuu na Idara/Vitengo na watumishi kwa ujumla juu ya suala la kufuata miongozo katika utekelezaji wa Bajeti.
Maelekezo mengine ilikuwa ni agizo la kuendelea kutenga katika Bajeti ulipwaji wa madeni yote ya wazabuni yanayopaswa kulipwa na Halmashauri na suala la usimamizi wa mikataba.
“Ndugu zangu jambo jingine ambalo ninaona fahari kukiri kuwa tumefanikiwa sana hapa wilayani kwetu ni suala la mahusiano ambapo kwa kweli tunapaswa kuendeleza mashirikiano hayo na wadau wetu wa maendeleo, waheshimiwa madiwani, sisi wenyewe kwenye Idara/Vitengo vyetu na zaidi tuwe na mahusiano mema na Chama Cha Mapinduzi kwani sisi ndio watekelezaji wakuu wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2015- 2020”, alisisitiza Mh. Kitonka.
Hotuba yake pia iliangazia utekelezaji wa masuala ya kiutumishi ikiwemo suala la kupanda vyeo kwa watumishi, Idara ya Utumishi na Utawala kuhakikisha kuwa kunakuwa na taarifa sahihi kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi (LAWSON) pamoja na majalada binafsi ya watumishi na katika hili, Mh. Kitonka alimwagiza Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala ndugu Jackson Mwakisu kuhakiki taarifa za watumishi hao kwenye majalada ya watumishi kazi aliyoagiza ifanywe kwa kushirikiana na watumishi wenyewe.
Katika suala hili la utekelezaji wa masuala ya kiutumishi, Mh. Kitonka alimwagiza pia ndugu Mwakisu na watumishi wote kufuatilia fedha zao zinazokatwa kutoka kwenye mishahara yao ili kupelekwa kwenye Mifuko ya ya Hifadhi ya Jamii, kufuatilia taarifa ya Fedha hizo ili kujiridhisha na usahihi wa taarifa hizo.
Pamoja na kupongeza ushirikiano wa watumishi wote katika kufanikisha upatikanaji wa Hati Safi katika Ukaguzi wa Hesabu uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017, Mh. Kitonka aliwataka watumishi hao kuendelea kuweka mikakati ya kuepuka kutokea kwa Hoja zisizokuwa za lazima ikiwa ni pamoja na kujibu kikamilifu Hoja za Mkaguzi kwa mwaka wa Fedha 2017/2018.
Maagizo mengine yaliyotolewa na kiongozi huyo yalihusu maelekezo ya masuala ya uhamisho wa watumishi na taratibu za uteuzi ambapo alitoa agizo kali kwa wakuu wa Idara/Vitengo kutokusaini barua zozote za uhamisho wawatumishi huku akikisitiza kwamba suala hilo linapaswa kutekelezwa na Mkurugenzi Mtendaji tu na asipokuwepo suala hilo litatekelezwa na yeyote atakayemkaimisha Ofisi hiyo huku akibainisha kwamba suala hilo linalenga kutekeleza kwa umakini agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa kwenye Maadhimisho ya Mei Mosi, 2018 yaliyofanyika mjini Iringa ambapo aliagiza mtumishi asihamishwe pasipo kulipwa stahiki zake za uhamisho.
Agizo la mwisho lilikuwa ni suala la maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2019 ambao alitoa agizo kwa Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi la kuendelea kufanyia kazi maandalizi yote muhimu kuelekea uchaguzi huo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.