Mkurugenzi Mtendaji awasihi watendaji, watumishi kutokuwa miungu watu
Na. Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karagwe, Godwin Kitonka amewataka watumishi na watendaji wa Halmashauri hiyo kuacha kuwanyanyasa wananchi wanaohitaji kupata huduma kutoka kwao badala yake watumishi na watendaji hao wamepaswa kuwahumia wananchi hao kwa kufuata miongozo na taratibu nyingine za kiutumishi huku akiwasihi kujenga tabia ya kuwa wasikivu.
Kitonka aliyasema hayo mapema tarehe 20/06/2017 alipozindua mafunzo kwa baadhi ya watendaji na watumishi waliohudhuria mafunzo haya yanayotarajiwa kudumu kwa siku mbili katika Shule ya Msingi Kambarage, tarafa ya Bugene kurudia maneno hayo tarehe 21/06/2017 kwenye tarafa ya Nyaishozi kadhalika amefanya hivyo tarehe 22/06/2017 kwenye tarafa ya Kituntu ambapo mafunzo hayo yanaendelea .
Mafunzo haya yaliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwajengea watendaji na watumishi uwezo wa kiuongozi katika Halmashauri hii ni moja ya mikakati ya Halmashauri ya wilaya Karagwe ya kuhakikisha viongozi hawa wanapata uelewa wa mambo kadhaa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Kitonka alisema mafunzo haya ni muafaka kwa ajili kuwaongezea viongozi hao uwezo wa kufanya kazi ikiwa ni pamoja kuwajengea uelewa wa pamoja lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi wanyonge.
Mapema katika Tarafa za Bugene na Kituntu, akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji kufungua mafunzo haya Afisa Utumishi wa Wilaya, Jackson Mwakisu aliyaelezea mafunzo haya kuwa yatafanyika katika tarafa zote za wilaya hii ili kuwawezesha watendaji wa serikali kata na vijiji kupata maarifa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Kitonka amekuwa anatumia fursa ya mafunzo hayo kuwaonya baadhi ya watendaji ambao sio waadilifu kuacha tabia hizo na kufanya kazi kwa uadilifu ili wananchi wanufaike na rasilimali za nchi.
Huku akimiminia sifa kemkem Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, Kitonka alisema watendaji hawa wanapaswa kusoma alama za nyakati kwani serikali ya awamu ya tano inataka watumishi wanaendana na kasi yake katika kuwahudumiwa wananchi wanyonge.
“Rais wetu anafanya mambo makubwa na kwa hiyo basi ni wajibu wetu kama viongozi ambao ndio tunawaohudumia wananchi hao wanyonge katika ngazi za chini tujitahidi sana kuhakikisha tunaendana na kasi hiyo kwa kuwahudumia na kuhakikisha wananchi hawa wananufaika na rasilimali za nchi hii kama ambavyo Mh. Rais anataka” amenukuliwa Kitonka kwenye mafunzo hayo
“Mnapaswa kuwa viongozi na sio watawala katika kuwahudumia wananchi wanyonge” alisisitiza Kitonka
Mafunzo haya yanayotolewa na wakufunzi ambao ni wataalam toka Halmashauri ya wilaya waliopewa mafunzo hapo awali na wakufunzi kutoka chuo cha Utumishi wa Umma, Singida yanapaswa kuendelea kwenye tarafa nyingine za wilaya kama vile Kituntu tarehe 22/06/2017 na 23/06/2017 huku tarafa za Nyakakika na Nyakabanga zikitarajiwa kuwa na mafunzo haya tarehe 28/06/2017 na 29/06/2017.
Mada zinazotarajiwa kutolewa kwenye mafunzo haya zitahusisha Uhamasishaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, Usimamizi wa Fedha za Halmashauri na Umuhimu wa Kusoma Mapato na Matumizi.
Nyingine ni Manunuzi ya Umma Katika Serikali za Mitaa, Uendeshaji wa Mikutano ya Halmashauri na Ngazi za Chini (Kata na vijiji/mitaa), Uongozi na Utawala Bora na Uandikaji na Usimamizi wa Miradi kwa Kushirikiana na Jamii.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.