Mkurugenzi Mtendaji afanya Ukaguzi kwenye vituo vya Afya, atoa Maigizo.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, ndugu Godwin M. Kitonka Jumatatu ya tarehe 18 Septemba, 2017 kwa kushirikiana na timu ya wataalamu wa Idara ya Afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa wilaya Karagwe Dkt. Libamba Sobo walifanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye zahanati na vituo kadhaa vya Afya lengo likiwa ni kukagua hali ya usafi, namna ya utoaji wa huduma, upatikanaji wa dawa kwenye vituo na zahanati hizo na kusikiliza kero za watumishi wa kada ya Afya zinazowakabili katika utekelezaji wao wa majukumu.
Shughuli za ukaguzi kwa siku ya kwanza ya tarehe hiyo ulifanyika katika zahanati ya Kakiro, Katwe, Kanoni pamoja na kituo cha Afya Rwambaizi ambapo timu hiyo ya ukaguzi ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya waliweza kupata taarifa kadhaa kutoka kituoni hapo.
Changamoto kubwa katika kila kituo kiklichotembelewa ilikuwa ni upungufu wa watumishi ambapo kwa kiasi kikubwa jambo hili linachangiwa na matokeo ya uhakiki wa watumishi wa umma uliofanywa na serikali na kisha kuwaondoa watumishi wasiokuwa na sifa na hivyo kupelekea suala hili la upungufu wa watumishi kwenye baadhi ya ofisi kujitokeza.
Suala jingine lililoibuliwa na watumishi lilikuwa lilikuwa ni motisha kwa watumishi ambao kimsingi wapo wachache na wanafanya kazi usiku na mchana.
Kupitia changamoto hizi ambazo ziliibuliwa karibu katika zahanati zote zilizotembelewa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Godwin M. Kitonka aliwatia moyo watumishi hao wanaofanya kazi usiku na mchana na kuwasihi waendelee na moyo huo huo wa kuwahudumia watanzania wanyonge kwani mipango ya serikali ni kuajiri watumishi wenye sifa stahiki na akaahidi kwamba watumishi wa kada za afya wataajiriwa mapema kama ilivyoahidiwa mara kadhaa na watendaji wakuu wa serikali ambao kimsingi ndio wasaidizi wakuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
“ Kuhusu suala la motisha kwa watumishi nakuagiza wewe Mganga Mkuu wa Wilaya kutoa maelekezo kwa vituo vyote vya Afya na zahanati zilizopo wilayani hapa ili watumishi hawa wanaofanya kazi usiku na mchana walipwe posho zao za ziada kwani jambo hili lipo ndani ya uwezo wetu”, alisema Kitonka akishangiliwa na watumishi hao.
Kupitia ukaguzi huo Mkurugenzi Mtendaji alitoa maelekezo mengine yaliyotokana na mapungufu aliyoyabaini kwenye baadhi ya vituo.
Agizo la kwanza ilikuwa kwamba matangazo yote ya muhimu (yasiyokuwa ya siri) yabandikwe kwenye mbao za matangazo.
“Nasisitiza matangazo yasibandikwe ukutani kama mnavyofanya bali yabandikwe kwenye mbao za matangazo ili kuepuka uharibifu wa kuta kama ambavyo mnafanya”, alisisitiza Kitonka kwenye kituo cha Afya Kanoni.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji alisisitiza kukamilishwa kwa ujenzi wa nyumba ya watumishi katika kituo cha Afya Kanoni kwani watumishi wanapata adha ya sehemu ya kuishi kungali nyumba ambayo ukamilishwaji wake wa ukarabati unahitaji gharama kidogo ili kuwapunguziwa watumishi hao adha ya kukaa mbali na zahanati hiyo.
Katika baadhi ya vituo kulikuwa na changamoto ya kubandika mawasiliano ya wahudumu kwenye mbao za matangazo ambapo Mkurugenzi Mtendaji alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya kutoa maelekezo upya ya kusisitiza jambo hilo kwa wasimamizi hao wa vituo.
Tarehe 19.09.2017 ukaguzi kama huu unatarajiwa kuendelea katika zahanati na vituo vingine vya Afya lengo likiwa kubaini mapungufu yanayoikabili sekta ya afya katika Halmashauri ya Wilaya Karagwe lengo likiwa kuyatafutia ufumbuzi baadhi ya mambo yanayokwaza utoaji wa Huduma.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.