Miundo Mbinu, Majengo Yazinduliwa KARUCO
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Miundo mbinu na majengo ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Karagwe (KARUCO), Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, inayotajwa kujengwa kwa takribani shilingi bilioni mbili na nusu imezinduliwa Jumapili ya tarehe 29 Oktoba, 2017 katika sherehe zilizoenda sambamba na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Matengenezo ya kanisa hilo.
KARUCO kilichojengwa kwenye eneo la Kishoju, Kata ya Kihanga kikiwa na takribani eneo la ekari zipatazo 912.2 kinatarajiwa kufundisha program za kilimo na stadi za mazingira pindi kitakapo pata Ithibati ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) huku kikielezwa kuwa kukamilika kwake kunakifanya kuwa chuo kikuu cha pili ukiacha kile cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ambacho ndio pekee kinachofundisha stadi hizo za kilimo hapa nchini.
Ujenzi wa Miundo mbinu na majengo ya chuo kikuu hicho ulizinduliwa mnamo Oktoba 11, 2012 na aliyekuwa waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika kwa wakati huo, Mhandisi Chrisopher Chiza.
Sherehe hizi za uzinduzi zilizofanyikia katika viwanja vya chuo kikuu hicho, ambapo zilianza na ibada ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya matengenezo ya kanisa, adhimisho linalotajwa kuwa ni kumbukumbu muhimu ya miaka hiyo tangu kanisa hilo lilipoasisiwa duniani na Mkuu wa kanisa hilo, mchungaji Dkt. Martine Luther.
Baada ya kumalizika kwa sehemu ya kwanza ambayo ni Ibada iliyoongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Mhashamu Dkt. Benson Bagonza, uzinduzi wa majengo na miundombinu ya chuo kikuu hicho ulifanyika.
Sherehe hizo zilizowakusanya mamia ya watu kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Karagwe zilihudhuliwa na viongozi kadhaa wa serikali, viongozi wa dini na wafadhili mbalimbali toka nje ya nchi ambao kwa kiasi kikubwa wamefadhili ujenzi wa chuo kikuu hicho.
Viongozi wa serikali waliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mh. Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Mustapha Kijuu ambaye kipekee alimwakilisha Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyetajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho haya lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake hakuweza kuhudhuria na kumuomba Mkuu wa Mkoa huyo kumwakilisha.
Mkuu wa Mkoa aliambatana na viongozi wote wa kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa, Mh. Diwani Athumani.
Pia alikuwepo Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh.Godfrey Mheluka, wajumbe wa kamati ya usalama ya wilaya, Mkuu wa Wilaya Bukoba, Mh. Deodatus Kinawiro, Mkuu wa Wilaya Kyerwa, Mh. Kanali (Mst.) Shabaan Lissu pamoja na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya Karagwe pindi ujenzi wa miundo mbinu hiyo ulipozinduliwa, Mh. Darry Rwegasira ambaye kwa sasa ni mkuu wa wilaya mstaafu.
Wengine walikuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Mh. Wallace Mashanda pamoja na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya hii huku Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya, ndugu Ashura Kajuna na baadhi ya wakuu wa Idara na Vitengo vya Halmashauri wakishiriki pia.
Sherehe hizi zilihudhuriwa pia na viongozi wa dini toka madhehebu mbalimbali ya ndani na nje ya nchi na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Profesa Joseph Parsalaw, alimpongeza Askofu Dkt. Bagonza kwa juhudi kubwa zilizofanyika katika ujenzi huo huku alitanabaisha kwamba alikuwepo kwenye eneo hilo wakati wa uzinduzi wa ujenzi huo.
Huku akibainisha kwamba ukamilishwaji wa ujenzi wa KARUCO unakifanya chuo kikuu cha Tumaini Makumira kufikisha idadi ya vyuo vikuu vishiriki vitano.
“Naamini hata wachungaji waliokuwepo kwenye eneo hili wakati ule ujenzi wa miundombinu hii ulipozinduliwa walikuwa hawana matumaini ya kufikia hatua hii iliyofikiwa leo lakini kwa sisi tunaomfahamu askofu Dkt. Bagonza tuliamini tutafika hapa tulipofika”, alisema Prof. Parsalaw.
Mapema Askofu, Dkt. Bagonza, wakati alipokuwa akimkaribisha Mgeni rasmi alielezea furaha yake katika kuona juu ya kukamilika kwa ujenzi wa miundo mbinu na majengo huku akiahidi kukamilika kwa ujenzi wa baadhi ya miundombinu ambayo haijakamilika ili kuwapa nafasi Tume ya Vyuo Vikuu kufanya ukaguzi kwa ajili ya kutoa ithibati na masomo yaweze kuanza kwa mwaka 2018/2019 kama ilivyokusudiwa.
“Hadi sasa tayari miundombinu ya maji imekamilika kwa sehemu kubwa, Bweni la kulala wanafunzi wa kike limekamilika, jengo la utawala limekamilika, maabara zote zinazohitajika zimekamilika pamoja na Maktaba”, alisema askofu Dkt. Bagonza.
“Miundo mbinu nyingine pia imekamilika ikiwemo madarasa na samani mbalimbali zitakazotumiwa na wanafunzi zimewekwa’’, alisema
Akifafanua juu ya program zitakazo fundishwa chuoni hapo, Askofu Dkt. Bagonza alibainisha kuwa wataanza na progranu za Kilimo, Mifugo, Misitu, Mazingira, Nyuki na Teknolojia ya Habari.
Aidha, Askofu Dkt. Bagonza amezitaja baadhi ya fursa ambazo wananchi wa Karagwe watanufaika nazo ikiwemo kupanua soko la mazao yao na mifugo na kuikuza Wilaya kiuchumi baada ya kuwa na wataalam karibu ambao pia watasaidia katika kuongeza thamani katika mazao ya wakulima na kutafuta soko la pamoja.
Faida nyingine ni kwamba uwepo wa chuo kikuu pia utasaidia kupeleka maendeleo vijijini, kuwa chemchem ya ajira, utafiti, uwekezaji, kuchochea mabadiliko katika sekta za afya, huduma nyingine kama kituo cha polisi, mawasiliano n.k
Katika hatua nyingine, Askofu Bagonza ameeleza kufurahishwa na ushirikiano anaopata kutoka kwa viongozi wa wilaya tangu miaka ya 1980 hadi sasa ambapo wanaenda kushuhudia hatua kubwa sana ya maendeleo Karagwe.
Kuhusu umiliki wa chuo, imefafanuliwa kuwa chuo hicho ni mali ya wananchi wa Karagwe bila kujali tofauti zao za kiimani na kwamba kinaendelea kuchangiwa na watu mbalimbali kwani kinalenga kwenye mapinduzi ya kiuchumi na kijamii Wilayani Karagwe.
‘’Licha ya chuo hiki kusajiliwa kwa jina la Kanisa lakini ni mali ya wananchi wote wa Karagwe na kinaendelea kuchangiwana waumini wa dini zote hivyo natoa wito kwa kila mmoja wetu kuunga mkono jitihada hizi ili kuinua maendeleo ya wilaya yetu na taifa kwa ujumla.’’ alisema Askofu Bagonza
Ili kuwezesha wakulima kupata soko nzuri la mazao yao, Askofu Dkt Bagonza amebainisha kuwa mara baada ya chuo kuzinduliwa, upo mpango wa kujenga vituo vya fursa vitano( Opportunity Centers ) ambapo vituo hivyo vitakuwa na miundombinu ya kila aina ikiwemo ya kuhifadhi mazao yasiharibike na kwamba wakulima watakuwa wanauzia mazo yao katika vituo hivyo kwa umoja ili wawe na sauti ya pamoja ya kupanga bei ya mazao tofauti na ilivyo hivi sasa.
Mgeni rasmi, Rais wa Mstaafu wa Awamu Nne, Mh.Dkt. Jakaya Kikwete katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa huu ameahidi kushirikiana na KARUCO kupitia Taasisi yake ya Jakaya Kikwete katika shughuli za kilimo.
“Kiu yangu ni kuona wakulima wadogo wanaongeza tija katika Kilimo”, alisema Dkt. Kikwete kupitia hotuba hiyo.
Katika hatua nyingine askofu Dkt. Bagonza alimwombea heri Rais mstaafu Kikwete ili aweze kufika pindi chuo hicho kitakapozinduliwa baada ya kupata ithibati na TCU) ya kunza kwa mwaka wa masomo 2018/2019 kama ilivyokusudiwa nah ii ni kutokana na kuenzi mchango wake alioutoa katika kufanikisha ujenzi wa chuo kikuu hicho.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.