Kikao cha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango chaweka Mikakati mizito Kufikia Vipaumbele vya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019.
Na Innocent E. Mwalo, Karagwe.
Katika hali ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli ili kutimiza azima ya kukusanya mapato kwa lengo la kutoa huduma muhimu kwa wananchi wanyonge, Halmashauri ya Wilaya hii kupitia kikao chake cha Bajeti cha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kilichoketi Januari 24,2018 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hii kimejadili kwa kina Bajeti ya kiasi cha Tsh. 42,465,119,022.94 iliyotengwa kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 kwa ajili ya kufikia vipaumbele kadhaa vilivyowekwa katika mpango wa Bajeti kwa mwaka wa huo wa Fedha.
Kikao hiki pamoja na mambo mengine kilipitia na kujadili ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na vikao vilivyotangulia kikiwemo kile cha kamati ya Elimu, Afya na Maji na Ujenzi, Uchumi na Mazingira ambavyo kwa pamoja viliketi mnamo tarehe 22/01/2018 na kile cha Baraza la Wafanyakazi kilichoketi Januari 23,2018 mahusisi kwa ajili ya kujadili Bajeti hiyo.
Awali wajumbe walihoja kupungua kiasi cha Bajeti kwa Mwaka huu wa Fedha ambapo kiasi hicho kimepungua kutoka kiasi cha Tsh. 47,713,731,279.27 Hadi Tsh.42,465,111,022.94 ambapo Timu ya Menejimenti kupitia kwa Mtakwimu ndugu Morice Muliro waliweza kutaja sababu kadhaa zilizopelea jambo hilo ikiwemo suala la baadhi ya miradi kama vile miradi ya kunusuru kaya maskini (TASAF), miradi ya sekta ya ya Afya (HBF), miradi ya kilimo(ASDP), baadhi ya mishahara, miradi ya UKIMWI pamoja na miradi ya barabara kutokuhusishwa kwenye Bajeti hiyo kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ile ya kusubiri maelekezo kutoka serikali kuu na kadhalika na miradi mingine kuondolewa kwenye Halmashauri ikiwemo suala la barabara lililokabidhiwa kwa wakala wa Barabara Mjini na Vijijini, TARURA.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye kikao hiki na Timu ya Menejimenti, makadirio haya ya Fedha hizo za Maendeleo yanatokana na Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo(LGCDG), Program ya Maji(WSDP), Mfuko wa Jimbo, Programu ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP), Mapato ya Ndani kwa 40% na Elimu bila Malipo.
Aidha makadirio mengine yanahusisha matumizi ya kawaida(OC Proper), matumizi ya kawaida (Own Source Reccurent), michango ya wananchi, michango ya NGOs zote kwa pamoja zikiifanya Bajeti hii kufikia kiasi cha 42,465,111,022.94.
Kabla ya kuweka mikakati, wajumbe waliweza kujadili kwa kina changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mpango wa Bajeti kwa Mwaka 2017/2018 ikiwemo suala la kuchelewa kupokea fedha za miradi ya maendeleo na hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi na uendeshaji wa shughuli za Halmashauri.
Changamoto nyingine iliyojadiliwa ilikuwa ni upungufu wa vitendea kazi hasa magari jambo lililotajwa kukwaza usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za kuwahudumia wananchi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Wajumbe walijadili kwa kina na kuafikiana kwamba Halmasahuri pamoja na mambo mengine inapaswa kufuatilia kwa karibu ngazi ya mkoa na kitaifa juu ya kuiomba Serikali kuleta fedha mapema ili shughuli zilizokusudiwa ziweze kutekelezwa kikamilifu.
Mikakati mingine ilikuwa ni kuendelea kutengwa kwa kiasi cha Fedha kwa ajili ya ununuzi wa gari moja kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa magari.
Baadhi ya vipaumbe vya mpango wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha huu vinahusisha kuendeleza sekta ya kilimo hasa mnyororo wa thamani kwa zao la kahawa ambapo Halmashauri imeshauriwa kutengwa hadi kiasi cha sh. 80,000,000 kwa ajili ya kuboreshwa kwa zao hili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kipaumbele kingine ni ujenzi wa soko la Kayanga baada ya kuungua moto mara mbili mnamo mwaka 2016 ambapo ili kufikia kipaumbele hiki Halmashauri imetenga kiasi cha Tsh.190,000,000 kwa ajili ya kuanza shughuli hiyo.
Halmashauri imetenga pia kiasi cha Tsh.80,000,000 kwa ajili ya kusaidia kukuza na kuendeleza viwanda vidogo vidogo wilayani hapa.
Hali kadhalika Halmashauri imetenga kiasi cha Tsh.90,000,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi ya mabasi Kishao.
Kipaumbele kingine ni kuendeleza na kukuza uchumi wa makundi mbali ya wanawake na vijana kwa kutenga jumla ya Sh. 182,487,552 kwa shughuli hiyo.
Pia, Halmashauri imeendelea kutenga Fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi, wazabuni mbalimbali na watumishi ambapo kiasi cha Tsh.235,092,111.90 kimetengwa kwa shughuli hiyo.
Vipaumbele vingine ni pamoja na Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi kuendelea kukamilisha maabara za Sayansi katika Shule 19 za sekondari za serikali ambapo kiasi cha Tsh.200,000,000 zimetengwa kwa shughuli hiyo.
Kikao hicho pia kilikubaliana kuimarisha mifumo mbalimbali ya kukusanyia mapato na ile ya kibajeti kuimarishwa ambapo mkazo uliwekwa kuimarisha mfumo kibajeti yaani PlanRep, mfumo wa kiutumishi(HCMIS), mifumo ya kutolea taarifa yaani CDR na CFR pamoja na ile ya kiuhasibu ya IPSAS na EPICOR ambapo kiasi cha 19,960,000 kimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
Kujengwa kwa Hospitali ya Wilaya ni kipaumbele kingine ambapo jumla ya Tsh.100,000,000 kimetengwa ili kuruhusu kuanza kwa shughuli hiyo.
Bajeti hii inatarajiwa kuendelea kujadiliwa katika vikao mbalimbali vya ngazi ya wilaya na mkoa kabla ya kupitishwa rasmi na Bunge na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye kikao chake cha Bajeti kinachotarajiwa kuketi mapema kuanzia mwezi Aprili mwaka huu mjini Dodoma. Vikao vingine vinavyotajiwa kujadili mapendekezo ya Mpango huu wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 pamoja na Mapitio ya Mpango huo wa Bajeti ni Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) cha tarehe 26/01/2018, kikao cha Baraza la Madiwani cha tarehe 29/30 Januari, 2018 pamoja na kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) kinachotarajiwa kukutana mjini Bukoba mnamo Februari Mosi, 2018.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.