“MICHEZO NI AJIRA” – KITONKA
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ndugu Godwin Kitonka hivi karibuni amewataka wanafunzi wanaoshiriki michuano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania, UMISETA kufanya bidii katika mashindano hayo ili kukuza vipaji vyao vya michezo huku akiwaasa watambue ya kwamba kwa sasa michezo ni zaidi ya kujenga urafiki na kuwafanya kuwa na afya njema badala yake wachukulie ya kwamba michezo ni ajira.
Mh. Kitonka aliyasema haya alipowahutubia wanafunzi hao kwenye ufunguzi wa mashindano hayo alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa muda wa siku mbili wilayani hapa kwa ajili ya kupata kikosi kitakachoshiriki kwenye mashindano hayo ya UMISETA ngazi ya mkoa
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, ndugu Upendo Rweyemamu, alimweleza mgeni rasmi ya kwamba katika mashindano hayo kulikuwa na ’Cluster’ nne zilizokuwa zinashiriki katika mashindano hayo ambazo alizitaja kuwa ni Nyaishozi, Nyabiyonza, Nyaishozi na Rwambaizi huku akiitaja baadhi ya michezo itakayofanyika kwa muda wa siku hizo mbili ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa mikono, pete, riadha, kurusha tufe, mikuki n.k
“Nakuagiza Afisa Elimu Sekondari na Wakuu wa Shule wote mnaoratibu mashindano haya kusimamia mashindano haya vizuri ili kusiwepo upendeleo na hatimaye wapatikane washindi wazuri na halali ambao wataweza kushiriki katika mashindano hayo hadi ngazi ya kitaifa wakiiwakilisha wilaya yetu”, alisisitiza Mh. Kitonka.
Huku akiitaja baadhi ya michezo kama mpira wa miguu ambayo mara nyingi waamuzi na waratibu wake huweza kufanya upendeleo kwa timu au washiriki wasiostahili.
Katika hatua nyingine Bi. Upendo pamoja na wakuu wa shule wanaoratibu mashindano hayo walimhakikishia Mgeni rasmi ya kwamba haki itatendeka katika mashindano hayo kwa kupatikana washindi wanaostahili.
Aidha katika hatua nyingine Bi. Upendo aliwaagiza wanafunzi hao kuonesha nidhamu ya hali ya juu katika kipindi hiki huku akibainisha ya kwamba hawatasita kumuondoa mshiriki yeyote atakayeshindwa kuonesha nidhamu katika mashindano hayo.
Ratiba ya mashindano hayo inatarajiwa kuwa ya siku mbili ili kupata timu ya wilaya ambayo baada ya kupatikana kwake itakwenda kambini kwa siku tatu kabla ya kwenda kufuana na timu za wilaya nyingine katika mashindano ngazi ya mkoa yatakayofanyikia katika manispaa ya Bukoba.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.