Mfumo wa “Kielektroniki’ kufungwa Kituo cha Afya Kayanga
Na Innocent Mwalo, KARAGWE.
Serikali kwa kushirikiana na Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya usimamizi wa utoaji wa huduma za afya, MDH wanakusudia kufunga mfumo wa kielekroniki kwenye kituo cha afya cha Kayanga wenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za malipo.
Hayo yalisemwa na timu ya wataalam kutoka MDH, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto walipofika katika kituo cha afya cha Kayanga kwa lengo la kufanya tathmini ya kina na ya mwisho itayowezesha uwekwaji wa miundombinu hiyo kuanzia Aprili 06, 2018.
Timu hiyo iliyowahusisha Daniel Pyuza, Sultana Sief, Restuta Tengio, Manyama Ian, Nassoro Salum, Abdala Liguo na Paulo Bwatihondo waliofika na kufanya ukaguzi huo ambapo kupitia kwa Mganga Mkuu wa Wilaya Karagwe, Dkt. Libamba Sobo aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hii Godwin Kitonka, waliweza kutembelea jumla ya majengo tisa (9) katika kituo cha afya hiki ambapo miundombinu inayohusika na mfumo wa TEHAMA kwa ajili ya kuhifadhia taarifa za wagonjwa inatarajiwa kujengwa.
“Tunapongeza jitihada hizi za ujenzi na kwa kweli shughuli hii ya ujenzi inatia matumaini”, alisema Nassoro Salum ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mradi huu wa ujenzi utadumu kwa takribani majuma sita na unatarajiwa kusimamiwa na Mhandisi Paulo Bwatihondo ambapo mara baada ya kukamilika kwake utasaidia kufanisha utoaji wa huduma za malipo na huduma nyingine za kitabibu kwa njia ya kielekroniki na hivyo kuboresha utoaji wa huduma za matibabu, kusaidia upatikanaji wa dawa na huduma nyingine hali kadhalika kupunguza usumbufu katika ulipaji wa malipo hayo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.