Mbio za Mwenge wa Uhuru 2017 zafana Wilayani Karagwe
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru 2017, ndugu Amour Hamad Amour ameimwagia sifa Wilaya ya Karagwe wakati wa uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwenye miradi kumi (10 )ya maendeleo yenye thamani ya kiasi cha shilingi 2,694,351,845.98 kwenye ratiba ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Karagwe mnamo Agosti 03,2017 kabla ya kuukabidhi Wilayani Kyerwa mapema Agosti 04,2017.
Ndugu Amour Hamad Amour alianza kuyasema hayo kwenye mradi wa kwanza uliohusu uzinduzi wa Klabu ya wapinga rushwa kwenye Shule ya Sekondari Nyakasimbi ambapo aliipongeza Wilaya ya Karagwe kuuweka mradi huu kuwa wa kwanza katika ratiba ya mwenge wa Uhuru wilayani Karagwe kwa mwaka 2017 kwani kwa kufanya hivyo ni kuonesha kwamba mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda muhimu ya taifa kwa kipindi hiki ambacho rushwa imekithiri katika maeneo mbalimbali ya utoaji wa Haki na kwa kufanya mapambano hayo ya rushwa ni suala muhimu katika kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Dk. John Pombe Joseph Magufuli.
Katika hotuba yake kwenye eneo hili la Shule ya Sekondari Nyakasimbi iliyodumu kwa takribani dakika 15, ndugu Amour alisisitiza kwamba rushwa inatakiwa kupambanwa kwa nguvu zote na kila mwananchi wa Tanzania kwani athali za rushwa ni kubwa katika dhana ya maendeleo na kwa hiyo aliendelea kuusifu uongozi wa Wilaya Karagwe kuuweka mradi wa mapambano ya rushwa kuwa wa kwanza kwani hali hiyo inaakisi kwamba wilaya ya Karagwe inathamini kwamba mapamabano dhidi ya rushwa kuwa ni msingi wa shughuli zote za maendeleo wilayani hapa.
Licha ya kutumbuiza kwa nyimbo mbalimbali, Klabu ya wapinga rushwa, Shule ya Sekondari Nyakasimbi ilipata wasaa wa kumwonesha maandiko mbalimbali kuhusu masuala ya kupambana na rushwa kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2017.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru aliuagiza Uongozi wa Wilaya kuhakikisha kwamba Elimu hiyo ya mapambano dhidi ya rushwa inapaswa kuwa ni ajenda ya kudumu katika wilaya hii huku akikisisitiza wanafunzi hawa ambao wamekwisha kuelewa maana halisi ya mapamabano dhidi ya rushwa kutumika katika makongamano mbalimbali wilayani hapa ili waweze kusambaza Elimu na uelwa huo kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla juu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Mradi wa pili uliokaguliwa ulikuwa unahusu Shamba la miti ya miberiti kiasi cha miti 4,950 lenye urefu wa ekari 04 (nne) mali ya ndugu Jackson Iganiza wa Kata Rugu katika kijiji cha Misha ambapo kiongozi huyo wa mbio za mwenge aliukagua mradi huu na kupongeza serikali ya wilaya kwa jinsi unavyotengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji akitolea mfano wa shamba hili lililokaguliwa na kuuleza mradi huu kwamba utaleta mapinduzi makubwa katika shughuli za maendeleo ya viwanda.
Kisha msafara huu uliekea kwenye mradi wa tatu uliokuwa unahusu uzinduzi wa Barabara ya Katojo Ihembe, Kalehe yenye urefu wa Km. 10 na Box Kalvati moja ambapo kiongozi wa mbio za mwenge na msafara mzima walipata nafasi ya kukagua mradi huu na kisha kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru aliuzindua mradi huu.
Mradi mwingine uliozinduliwa ulikuwa ni ule unaohusu Ujenzi wa mabweni mawili ya wavulana katika Shule ya Sekondari ya Bugene ambapo pia ujumbe wa Mwenge wa Uhuru ulitolewa.
Katika viwanja vya Shule hiyo kiongozi wa Mbio za mwenge aliwaasa walimu kutumia muda wao mwingi kubaki katika vituo vya kazi ili waweze kuwafundisha wanafunzi lakini kubwa wito ulitolewa kwa walimu wa kidato cha tano na sita hasa katika somo la Historia kufundisha wanafunzi namna ambavyo mapinduzi wa viwanda yalitokea huko Ulaya ili Elimu hiyo iwe chachu katika maendeleo ya uchumi wa viwanda kwa taifa letu.
Kisha msafara ukaelekea kwenye eneo la Kishao kijiji cha Rukajange Kata ya Bugene kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa maji.
Mara baada kuweka jiwe la msingi, Msafara ulielekea kata ya Kayanga ambapo ulifanyika uzinduzi wa Kikundi cha Vijana Selemala Kayanga.
Baada ya hapo Msafara ulielekea kwenye Kiwanda cha kumenya kahawa mbivu mali ya KADERES ambapo kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru aliuzindua mradi huu.
Mradi mwingine ulikuwa ni ule uwekaji wa jiwe la msingi wa Kituo cha Afya Kayanga ambapo ujenzi wa wodi ya wanawake na watoto pamoja na kituo cha kuhifadhia maiti ambapo kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru alipata wasaa wa kuweka jiwe hilo la msingi huku akipongeza ujenzi wa mradi huu.
Msafara huu uliekea kwenye eneo la Mkesha Uwanja wa Kayanga ambapo kiongozi wa mbio za mwenge alipata kukagua vibanda vya maonesho vya Vikundi vya wajasiliamali kiitwacho MVIKAKATI cha Kituntu lakini pia kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru alikagua mabanda mbalimbali kama vile banda la UKIMWI, banda la Malaria, Banda la Madawa ya Kulevya pamoja na banda la Rushwa.
Katika eneo hili la mkesha, Uwanja wa mpira Kayanga pia Katibu Tawala wa Wilaya ya Karagwe Mh. Innocent Nsena alisoma risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kisha baada ya risala ya utii Ujumbe wa Mbio za Mwenge ulitolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2017 ndugu Amour Hamad Amour.
Katika ujumbe huo ndipo kiongozi wa Mbio za Mwenge alitumia wasaa huo kupongeza miradi iliyozinduliwa, iliyokaguliwa pamoja na ile iliyowekewa mawe ya msingi huku akiahidi kutoa ushirikiano zaidi hasa Elimu ya ujasirimali kwa miradi miwili aliyoonekana kuvutiwa nayo sana yaani ule wa Vikundi vya Wanawake wajasiliamali cha MVIKAKATI cha Kituntu pamoja na ule wa Kikundi cha Vijana Selemala cha Kayanga kwa ujasiliamali wao wenye tija.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 ukiwa Wilayani Karagwe ulizindua, kukugua na kuweka mawe ya msingi kwa miradi kumi yenye thamani ya kiasi cha shilingi 2,694,351,845.98 ikiwa ni mchango wa wananchi wa wilaya Karagwe, mchango wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na pia mchango kutoka serikali kuu.
Mwenge huu ulikabidhiwa Wilaya Kyerwa mapema asubuhi ya tarehe 04 Agosti, 2017 katika eneo la Chanya makabidhiano yaliyofanywa kati ya Mkuu wa Wilaya Karagwe Mh. Godfrey Mheluka na Mkuu wa Wilaya Kyerwa Mh. Luteni (mstaafu) Shabaan Lissu kwenye eneo la Shule ya Msingi Chanya.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.