Mafunzo uhamasishaji wa maendeleo endelevu yatolewa wilayani Karagwe
Na INNOCENT MWALO- KARAGWE
Mafunzo maalum yaliyoandaliwa na uongozi wa Halmashauri ya wilaya Karagwe na kutolewa na wataalam wa menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora toka chuo cha utumishi wa umma Singida yenye lengo la kuwaandaa wakufunzi toka hapa Halmashauri ya Wilaya pamoja na kuwajengea uwezo waheshimiwa madiwani kuhusu uhamasishaji wa malengo endelevu yaanza.
Mapema tarehe 12/06/2017, mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Wilaya ndugu Innocent Nsena alifungua mafunzo haya katika ukumbi wa kituo rafiki cha vijana, Angaza, huku akiwahimiza wahudhuriaji wa mafunzo haya kuzingatia maada mbalimbali zitakazotolewa kwenye mafunzo hayo.
Ndugu Nsena aliyataja mafunzo hayo kuwa ni muhimu huku akisema yamekuja kwa muda mwafaka katika kipindi hiki ambapo Halmashauri inakabiliana na changamoto mbalimbali za usimamizi wa miradi kwenye ngazi chini za Halmashauri.
“Matumaini yangu mafunzo haya yatasaidia katika taratibu za udhibiti na usimamizi wa fedha kwenye serikali za mitaa, kuainisha changamoto za usimamizi wa fedha kwenye Halmashauri na kuzitatua pamoja na mafunzo ya utawala bora”, alibainisha Katibu Tawala huyu.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hii, Mh. Wallace Mashanda ambapo pamoja na mambo mengine aliwasisitiza waheshimiwa madiwani kujiandaa kukabiliana na mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kuja katika utendaji wa serikali ambapo aliwasihi kuendana na kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia ikiwa ni nyenzo muhimu katika kufuatilia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Baada ya uzinduzi huu kufanyika kwenye kituo cha Angaza, mafunzo haya yaligawanyika katika makundi mawili; moja likiwa ni lile kundi linalojumuisha waheshimiwa madiwani na jingine likiwa ni lile linalohusisha timu ya wataalam toka Halmashauri wanaotarajiwa kuwa wakufunzi baada ya mafunzo haya kumalizika.
Mafunzo haya yanayotarajiwa kudumu kwa muda wa siku tano yatajumuisha maada kadhaa zitakazotolewa kama vile Uhamasishaji wa malengo ya maendeleo endelevu, usimamizi wa Fedha za Halmashauri na umuhimu wa kusoma mapato na matumizi.
Maada nyingine zitahusisha manunuzi ya umma katika serikali za mitaa, uendeshwaji wa mikutano ya Halmashauri na ngazi za chini yaani vijiji na mitaa, uongozi na utawala bora, uandikaji na usimamizi wa miradi kwa kushirikiana na jamii.
Mafunzo haya yatahitimishwa kwa kutunukiwa kwa vyeti vya mafunzo kwa washiriki wote kabla ya wahitimu hawa kukabiliana na jukumu la kwenda kuuelisha umma wa wananchi wa wilaya Karawe kuhusu uhamasishaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.