MAELEKEZO YA BARAZA LA MADIWANI KWA WATENDAJI NA WANANCHI.
Na Innocent E. Mwalo,KARAGWE.
Kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichodumu kwa takribani siku mbili kimemalizika kwa kutoa maagizo na maelekezo kadhaa kwa watendaji na wananchi wa Wilaya ya Karagwe kwa ajili ya kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi wa hao.
Ikiwa ni muendelezo wa siku ya kwanza, kikao hiki kiliweza kupokea taarifa ya serikali iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka ambapo licha ya kuwashukuru viongozi wilayani hapa kwa kujitokeza kwa wingi kwenye masuala kadhaa wa kadhaa ikiwemo ziara za viongozi wa kitaifa, alitoa maagizo kadhaa ikiwemo kukemea suala la rushwa lililojitokeza katika zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya taifa linaloendelea katika kata za Wilaya ya Karagwe.
“Napenda kukuagiza Meneja wa TANESCO Wilaya kuwaagiza watu wako watoke ofisini mara moja muda huu na kwenda eneo la Nyakagoyegoye kata ya Kiruruma kwa ajili ya kwenda kurekebibisha nguzo ya umeme na transfoma iliyoathiriwa na mvua kwa takribani majuma matatu sasa”, alisikika Mh. Mheluka alipokuwa akijibu hoja ya Diwani wa Kiruruma Mh. Silvester Evarista.
Aidha katika hatua nyingine, Meneja wa Barabara Mjini na Vijini, TARURA, Mhandisi Peter Mikimba aliweza kuwaeleza wajumbe wa kikao hicho ya kwamba serikali imewaagiza TARURA kupitia barabara zote kwa ajili ya kubaini barabara zilizoathiriwa kutokana na athali za mvua na kwamba mara baada ya kazi hiyo kutafanyika matengenezo ya barabara hizo yatafanyika kupitia fungu maalum la fedha itakayotolewa na serikali.
Katika hatua nyingine, Baraza hilo liliweza kupitia utekelezaji wa maazimio ya kikao chake cha Machi 01- 02 mwaka, ambacho kiliagiza mambo kadhaa wa kadhaa.
Timu ya wataalam ndio ilikuwa na jukumu la kutoa majibu hayo huku ikianisha taarifa mbalimbali za utekelezaji wa maagizo hayo ambapo kwa kiasi kikubwa kikao hicho kiliweza kuagizwa juu ya utekelezaji wa azimio la watendaji kushirikiana na wananchi kwa kila kijiji kubainisha maeneo ya wafugaji na kuyawekea alama.
Katika hatua nyingine ya utekelezaji wa baadhi ya maazimio, wajumbe walipata nafasi ya kupitisha majina ya wajumbe wapya wa mabaraza ya kata kwa takribani kata 19 huku kata nne ambazo haziwasilisha orodha hiyo ya majina kazi hiyo ikikasimiwa kwa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango.
Aidha, Baraza liliweza kupokea taarifa mbalimbali za utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri kutoka kwa wenyeviti wa kamati za kudumu za Halmashauri ambapo katika Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango iliyowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Mh. Dauson Byamanyirwohi ikiwa ni taarifa ya miezi mitatu yaani Februari, Machi na Aprili ambapo wajumbe kwa kauli moja waliagiza kwamba tax zote zinazofanya kazi ya kuchukua abiria kutoka Kayanga kwenda Omurushaka zifike Nyakahanga Hospitali ambacho ndio kituo cha kugeuzia magari kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Baraza liliagiza kwa yeyote atakyevunja na kukiuka sheria hiyo kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kulipa faini ambayo kwa mujibu wa sheria za Fedha. Faini hiyo ni kuanzia shilingi Laki mbili hadi milioni moja.
Kadhalika kupitia Baraza hilo, wajumbe waliazimia kubainishwa kwa vitabu vyote vilivyochukuliwa na watendaji katika ngazi mbalimbali za Halmashauri kwa muda mrefu huku hatua kali zikiagizwa kuchukuliwa kwa yeyote atayeonekana kutowasilishwa vitabu hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Baraza liliweza kujadili pia Taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira inayoongozwa na Mh. Charles Beichumila ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakahanga.
Katika taarifa hiyo wajumbe waliagiza Idara ya Afya Wilayani hapa kukagua na kujiridhisha na orodha ya maduka ya dawa muhimu yaliyosajiliwa na kuchukua hatua kali ikiwemo ya kuyafungia maduka yale yote yasiyosajiliwa ili wananchi waweze kupata huduma iliyo salama.
Jambo jingine liliagizwa lilikuwa ni suala la kukamilika kwa wakati kwa miradi ya maji na kisha ikabidhiwe kwa wananchi ambapo kwa maelezo yaliyotolewa na Fundi Sanifu kutoka Idara ya Maji Vijijini, Hernam Kigwa, miradi hiyo itakamilika kabla ya Juni, 04 Mwaka huu.
Masuala mengine yalijitokeza katika Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira ambapo wajumbe walikubalina juu ya mambo kadhaa ikiwemo suala la wananchi kuchukua tahadhali katika kupambana na ugonjwa ujulikanao kwa jina la gugu karoti ambao umeenea kwa kasi kubwa na kusababisha madhara makubwa kwa mimea, wanyama na wanadamu na hivyo ikasisitizwa ya kwamba wananchi wote wachukue tahadhali ya kutokushika kwa mkono gugu hili na pia kuchukua tahadahli nyingine ikiwemo kung’oa gugu karoti kabla halijatoa maua na mbegu huku ikishauriwa baada ya kuling’oa kulichoma moto gugu hilo.
Katika hatua nyingine Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika ilielekezwa kubaini ugonjwa wa mibuni na kuchukua hatua kwenye maeneo ambayo ugonjwa huo umeathiri mazao hayo.
Wito mwingine ulitolewa kwa wakulima wa mahindi na maharage na mazao mengine kuacha kuuza mazao hayo kwa kutumia vipimo vya ndoo na vifaa vingine badala yake wananchi hao wameaswa kutumia mizani katika kuuza mazao hayo.
Aidha kikao hicho, kiliweza kuazimia kwa kauli moja kuhusu wazo la kwenda kupanda miti kwenye mlima Kishoju, eneo lililopo katika kata ya Kihanga kwa ajili ya kupamba mandhari ya eneo hilo na pia kuhamasisha wananchi juu ya uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo yao.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.