Maandalizi ya Mwenge wa Uhuru 2018 ‘Yapamba Moto’ Karagwe.
Na Innocent Mwalo, KARAGWE
Maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 unaotarajiwa kuwasili wilayani Karagwe mnamo 13 Aprili, 2018 yamepamba moto.
Hayo yamejidhihirisha kupitia kikao cha kamati ya mwenge wilayani hapa kilichoketi hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hii chini ya uenyekiti wa Katibu Tawala wa wilaya, Mh. Innocent Nsena.
Aidha katika kikao hicho wajumbe waliweza kujadili miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu ikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 1,654,900,000.00 ikitarajiwa kuzinduliwa.
“Miradi ni mizuri isipokuwa nashauri kwa wataalam kwenda mbali zaidi kwa kuongeza vitu kadhaa ili Wilaya yetu iweze kufanya vizuri zaidi katika ratiba ya mwenge wa uhuru kwa mwaka huu”, alisisitiza Benneth Ruhinda mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Katika hatua nyingine kikao hicho kilipokea na kujadili kauli mbiu ya mwenge huo wa uhuru kwa mwaka huu inayosema, “Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Wekeza Sasa”.
Ujumbe wa kudumu katika ratiba ya mwenge huu wa uhuru inatajiwa kubaki kama mika mingine ikiangazia katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ile ya UKIMWI/VVU inayosema “Mwananchi jitambue, pima afya yako sasa” na ile ya Malaria inayosema “Shiriki kutokomeza Malaria kwa manufaa ya jamii”.
Aidha ujumbe mwingine utaangazia dawa za kulevya chini ya kauli isemayo “Tuwasikilize na kuwashauri watoto ili wasitumie dawa za kulevya” pamoja na ile inayohusu Rushwa chini ya kauli mbiu isemayo “Kataa rushwa jenga Tanzania”
Mwenge wa Uhuru utawashwa mkoani Geita mnamo tarehe 2/04/2018 na unatajiwa kuzunguka katika Halmashauri zote 195 zilizopo Tanzania Bara na Visiwani kabla ya kufikia kilele chake mapema 14/10/2018.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.