Maadhimisho ya upandaji miti ‘yafunika’ Wilayani Karagwe.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali (Mst.) Salum Mustafa Kijuu ameagiza Halmashauri zote katika mkoa wa huu kutekeleza kwa vitendo agizo lake la upandaji wa miti kwa kupanda miti milioni moja na laki tano (1,500,000) au zaidi kila mwaka.
Haya yamesemwa hivi karibuni na Mh. Godfrey Mheluka ambaye ni Mkuu wa Wilaya Karagwe na ambaye kwenye maadhimisho hayo alimwakilisha Mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera.
Maadhimisho haya ambayo kitaifa yatafanyika Aprili 05, 2018 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, katika mkoa wa Kagera yamefanyika katika Wilaya ya Karagwe huku yakipambwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania ya Kijani Inawezekana Panda Mti kwa Maendeleo ya Viwanda”.
“Mkoa wa Kagera unakabiliwa na tatizo la utapiamlo,udumavu na upunguvu wa vitamini hususani kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, miongoni mwa sababu ni kutozingatia matumizi ya lishe bora na ulaji wa matunda. Kwa sasa Mkoa wa Kagera unaendeleza kampeni ya upandaji miti ya matunda kampeni iliyozinduliwa tarehe 26/1/2018 kwa lengo la kuhamasiha na utoaji wa elimu ya umuhimu wa lishe bora na ulaji wa matunda”, alisisitiza Mkuu wa Mkoa kupitia hotuba yake.
Aidha kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo kila Halmashauri za Wilaya , taasisi za Serikali na Binafsi Mkoani Kagera zimeagizwa kuhakikisha zinapanda miti ya matunda mbalimbali kuzunguka maeneo yao.
“Pia Halmashauri za Wilaya Mkoani Kagera zihakikishe kila Kaya inapanda angalau miti ya matunda kuanzia mitano kuzunguka maeneo yao ya makazi na ikumbukwe pia kama hatua ya kuanzia katika mwaka wa fedha unaoendelea tulikubaliana kuanza kupanda miti ya matunda katika taasisi za afya”, aliendelea kusisitiza Mkuu wa Mkoa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ameziagiza mamlaka za Serikali za vijiji , watendaji na Maofisa wote wa Serikali wakiwemo Maafisa wa kada ya misitu kuchukueni hatua kwa Mujibu wa sheria ya Misitu Na.14 ya 2002 pamoja na sheria ya mazingira ya Namba 20 ya Mwaka 2004 kwa wale watakaobainika kuchoma moto ovyo.
Nao uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kupitia risala iliyowasilishwa na Processius Rweyendera kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya Karagwe umebainisha kwamba kwa mwaja jana Halmashauri ya Wilaya Karagwe ilifanya upandaji wa miti 1,862,720 kutoka kiasi ilichojiwekea kupanda ambayo ni miti 1, 500,000 ikiwa ni ongezeko la takribani asilimia 24 ya lengo lililowekwa.
Aidha uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kipekee ulizipongeza Taasisi za kidini zinazofanya kazi kubwa ya kushiriki katika kupanda miti ambapo taasisi kama CHEMA, ELCT, MAVUNO, KARUPOA zikiwa ni baadhi zimetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha jitihada hizi za upandaji wa miti.
Katika shamrashamra hizi jumla ya miti 600 ya matunda imependwa katika maeneo mbalimbali hapa wilayani na kazi hii inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo.
Kwa namna ya pekee Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Mh. Wallace Mashanda ametoa wito kwa Menejimenti kuhakikisha kwamba mkakati unawekwa katika uundwaji wa klabu za Mazingira ili ziwe chachu katika kuhimiza jitihada hizi za upandaji wa miti.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.