Maadhimisho ya Siku ya Unyonyeshaji yafana Wilayani Karagwe
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyesha ambayo huadhimishwa kitaifa kila mwaka kuanzia tarehe 01 Agosti mpaka tarehe 07 Agosti, hapa Wilayani Karagwe yamefikia kilele chake mapema tarehe 08 Agosti, 2017 katika viunga vya kitongoji cha Rwizinga kijiji cha Mguruka katika kata ya Bweranyange huku Elimu kuhusu unyonyeshaji ikitolewa kupitia shamrashamra hizo.
Awali kabla ya ujumbe wa dhana ya unyonyeshaji uliotolewa na wataalam kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, sherehe hizo zilipambwa kupitia utumbuizaji uliofanywa kwa njia mbalimbali zikiwemo ngoma, nyimbo,ngonjera, risala na michezo ya kuigiza.
Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Diwani wa Kata ya Bweranyange, Mh. Fideli B. Mugabo huku kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni “Sote kwa Pamoja Tuendeleze Unyonyeshaji”
Kauli mbiu hii ilikiwa ni mahususi kuwakumbusha wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo kwani ni muhimu sana kwa afya na uhai wa mama na mtoto.
Awali mada kuhusu Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama ilitolewa na Maafisa Lishe kutoka Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ambao walikuwa Bi. Lustica Mgumba na Bi. Gissela Richard.
Katika mada hiyo washiriki walifundishwa umuhimu wa unyonyesha wa maziwa ya mama ambapo wawezeshaji walitaja faida kadhaa kama za kunyonyesha maziwa ya mama vile maziwa ya mama kuwa kuwa na virutubisho vyote muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mtoto kwa muda wa miezi sita.
Umuhimu mwingine uliotajwa kutokana na unyonyeshaji wa maziwa ya mama ulikuwa ni gharama ndogo sana za maziwa hayo ukilinganisha na maziwa ya viwandani na ya wanyama, kuimarisha upendo kati ya mama na mtoto, maziwa haya hutumika kama njia ya uzazi wa mpango kwa muda wa miezi sita endapo mama atamnyonyesha mtoto vizuri mara kwa mara.
“Pia husaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali yake ya mwanzo na wakati mwingine hupunguza mama kuvuja damu nyingi na hivyo husaidia kupunguza upungufu wa damu”, alibainisha Bi. Lustica kupitia mada hiyo.
Pia mada hiyo ilibainisha kuwa ni muhimu ndani ya miezi sita katika ukuaji wa mtoto baada ya kuzaliwa kwa mama kuzingatia kumnyonyesha maziwa ya mama tu mtoto kwani maziwa ya mama yana virutubisho vyote na maji ambayo mtoto anahitaji kwa ajili ya ukuaji katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo.
Pia ilitajwa sababu ya kwamba mtoto ambae amenyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi sita hashambuliwi kirahisi na magonjwa ya kuharisha pamoja na majonjwa mengine kwa sababu maziwa ya mama ni masafi na humlinda mtoto dhidi ya magonjwa.
Kadhalika wataalam hao wa lishe walieleza kwamba mama anapomnyonyesha mtoto mfululizo kwa miezi sita ya mwanzo humsaidia kutopata mtoto mwingine mapema na pia humsaidia mtoto katika kuimarisha hatua mbalimbali za ukuaji.
Elimu hii ya unyonyeshaji iligusia pia mambo ya kuzingatia wakati wa kunyonyesha ambayo yalikuwa ni kwamba mama anatakiwa kuwa msafi (kwa nguo alizovaa na mwili wake) kwani asipozingatia usafi anaweza kumsababishia mtoto magonjwa, mtoto anatakiwa kunyonyeshwa katika hali ya utulivu, mtoto anyonyeshwe angalau mara kumi hadi kumi na mbili katika masaa 24 na mama anatakiwa kufahamu ishara mbalimbali zinazoonesha kwamba mtoto ana njaa ambapo ishara hizo ni kama vile kunyonya vidole na kutoa ulimi.
Mada hii ilisisitiza pia namna ya kumshika mtoto wakati wa kumnyonyesha ili aweze kunyonya vizuri ambapo ilielekezwa na wataalam hao kwamba sehemu nyeusi ya ziwa baada ya chuchu inatakiwa kuwa ndani ya mdomo wa mtoto.
Pia ilielezwa kwamba tumbo la mtoto linatakiwa kugusana na tumbo la mama.
Aidha ilisisitizwa kwamba mama hatakiwi kubana ziwa na vodole kwa kuweka mkasi wakati wa kunyonyesha kwani husababisha mtoto kutopata maziwa ya kutosha kutokana na kuziba kwa vimirija vidogovidogo vinavyopitisha maziwa.
Jambo jingine lililosisitizwa ilikuwa ni kwamba mtoto anatakiwa kunyonya ziwa moja hadi maziwa yote yaishe ndipo ahamishiwe ziwa jingine na zaidi ya hapo uso wa mtoto unatakiwa kutizamana na uso wa mama.
Katika risala iliyosomwa kwa mgeni rasmi na Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Wilaya, ilibainisha kwamba suala la unyonyeshaji sio suala la wanawake pekee yao bali ni jukumu pia la baba na jamii kwa ujumla.
Pia risala hiyo ilianisha changamoto zinazoathiri unyonyesha kama vile jamii kuendelea kutofuata kanuni bora za unyonyeshaji, kutokuwepo kwa ushirikiano na wanafamilia na jamii na wakina mama wanapewa majukumu mengi yanayochangia kutonyonyesha ipasavyo kwa hivyo basi inashauriwa mama apunguziwe majukumu kipindi cha unyonyeshaji.
“Tutaendelea kutoa Elimu ya unyonyeshaji katika maeneo ya vituo vya tiba, vipindi redioni na kwenye mikutano ya jamii”, ilibainisha risala hiyo iliyosomwa na mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Wilaya.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi, Mh. Fideli B. Mugabo aliushukuru uongozi wa Wilaya kwa kufanya maadhimisho haya kwenye kitungoji wa Rwizinga, kijiji cha Mguruka Kata ya Bweranyange huku akinukuliwa kwamba huenda ni mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa Taifa hili la Tanzania kwa maadhimisho ya namna hii kufanyika katika eneo hilo.
Mh. Mugabo alitumia wasaa huu kuiomba ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hii ya Karagwe kutafakari juu ya ombi lao la kujengewa zahanati ya kijiji cha Mguruka huku akibainisha sababu kadhaa ikiwemo ile ya kwamba kijiji hicho ni kipya kwani kimeanzishwa mwaka 2015.
“Wakazi hawa wanasafiri umbali mrefu kutoka eneo hili kufuata huduma ya afya kwenye maeneo mengine husafiri takribani kilomita 30 (kwenda na kurudi) kwa ajili ya kufuata huduma kwenye kijiji cha cha Chamchuzi jambo ambalo linasababisha kero na usumbufu mkubwa kwa wananchi hawa wanaosafiri umbali huo kwenda kutafuta huduma hiyo muhimu”, alikanukuliwa akisema Mh. Mugabo.
Naye Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Wilaya, Bi. Beatrice Laurent alitumia maadhimisho kuungazia umma uliokusanyika katika sherehe hizo kuchukua tahadahali dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu unaoripotiwa kutokea kwenye baadhi ya maeneo ya hapa nchini na kwa hivyo jamii inapswa kuzingatia kanuni za usafi ikiwemo matumizi sahihi ya vyoo pamoja na kunawa mikono kila baada ya kutoka chooni pamoaja na kula vyakula vya moto na vile vilivyochemshwa vizuri.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.