LIFAHAMU GUGU KAROTI NA MADHARA YAKE
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Gugu karoti ambalo kisayansi linatambuliwa kama “Parthenium weed” ni gugu vamizi ambalo majani yake hufanana sana majani ya zao la karoti ambapo kwa hapa nchini Tanzania gugu hili limeonekana kwenye maeneo mbali mbali ikiwemo hapa wilayani Karagwe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoandaliwa na Ramadhani Kilewa, Mtafiti katika Kitengo cha Kuzuia Visumbufu vya Mimea, TPRI, kutoka Arusha, asili ya gugu hili ni Amerika ya kati, kusini na nchi ya Mexico.
Katika kujiridhisha na uwepo wa mmea huu, mwandishi wa makala haya alitembea maeneo kadhaa katika wilaya ya Karagwe ikiwemo ukanda wa Bushangaro hasa katika Kata za Tarafa za Nyabiyonza na Nyakakika hali kadhalika maeneo ya Tarafa za Nyaishozi na Bugene ambapo kwa kiasi kikbwa gugu hili limetamalaki katika maeneo hayo bila wananchi wengi kutokulijua na kutambua madhara yake.
Kwa hiyo makala hii inapenda kuangazia baadhi ya madhara ya gugu hili ambapo kwa mujibu wa Mtafiti ndugu Kilewa, anautaja mmea huu kuwa na sumu aina ya Parthenium. Sumu hii inatajwa kwamba inaweza kusababisha ugonjwa wa ngozi unaoitwa Parthenium allergic demartitis ambapo inakadiriwa watu karibu na asilimia 73 wanaoishi karibu na gugu hili wanaweza kupata ugonjwa wa ngozi iwapo watagusa mmea huu huku wanawake wakitajwa kuwa ndio waathirika zaidi kuliko wanawake.
“Baadhi ya dalili za ugonjwa wa ngozi unaosababishwa na gugu karoti ni pamoja na kuwashwa kwa ngozi, hasa katika maeneo ya uso na mikono, macho kutokwa na machozi, kuvimba na kuchomachoma katika utando wa ngozi yam domo na pua, kukuhoa mfululizo muda wa usiku, pua kupumua kwa sauti pamoja na kuchomachoma katika ukuta wa juu wa mdomo na uchovu”, imenukuliwa taarifa ya mtafiti huyo.
Aidha kupitia andiko hilo yanatajwa baadhi ya madhara ya gugu karoti kwa wanyama ikiwemo kusababisha manyonya kunyonyoka, midomo kuvimba na kupasukapasuka na hupunguza ladha ya nyama.
Kwa upande mwingine sumu aina ya parthenin iliyopo katika gugu karoti husababisha maziwa kuwa na uchungu.
Kadhalika madhara mengine mmea huu hupunguza kiwango cha uzalishaji wa maziwa na wakati mwingine mnyama akila gugu karoti kati ya asilimia 30 na 50 anaweza kufa.
Kwa upande wa mimea mingine ya asili, gugu karoti linatajwa kuwa na uwezo wa kuzuia kuota kwa mbegu na ukuaji wa mimea ya asili, kupunguza malisho ya wanyama na kuleta athali ya virutubisho katika udongo.
Kuhusu madhara kwa mazao, gugu karoti linatajwa ya kwamba linaweza kuzuia mbegu kuota, kupunguza ukuaji wa mazao, kuzuia uchavushaji wa maua ya mazao mfano nyanya, maharage, pilipili na biringanya.
Madhara mengine kwa mazao ni kupunguza mazao na kuhifadhi wadudu mfano mdudu aitwaye “meal bugs whiteflies na vimelea vya magonjwa ya fangasi kwa mazao.
Hata hivyo zipo jinsi mbalimbali ambazo wananchi wa Karagwe na menegine hapa nchini wanaweza kuzichukua ili kukabiliana na gugu karoti. Nazo ni kama vile kung’oa gugu karoti kabla halijatoa maua na mbegu.
Jinsi jingine ni kama vile kuhakikisha mizizi inang’olewa ili kuepuka kuacha shina ambalo litaota na kutoa mbegu baada ya wiki mbili.
Aidha inashauriwa baada ya kung’oa mmea huu ukusanywe na kuchomwa kwa moto.
Pia ni vizuri kukinga ngozi kwa kuvaa nguo nyepesi ambayo ni ndefu itakayofunika sehemu za mwili. Hali Kadhalika ni muhimu wananchi wakavaa ‘gloves’ au mifuko ya nailoni katika mikono na viatu vinavyofunika miguu.
Na wakati mwingine, ni muhimu kuvaa ‘masks’ kuzuia vumbi la kwenye maua kuingia puani na mdomoni na kama wananchi wakahisi ngozi inawasha na kuchomachoma wanashauriwa kutokujikuna na kujifuta badala yake wanapaswa kuosha sehemu inayowasha au kuchomachoma kwa maji baridi haraka iwezekanavyo.
Kadhalika inasisitizwa kutumia Viuagugu ‘Herbicides’ ili kuangamiza gugu karoti.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.