Na, Geofrey A.Kazaula
Afisa lishe kutoka shirika la IMA World Health anayefanya kazi katika mradi wa mtoto mwelevu Bi. Idda Katigula amesisitiza kuwa Wadau wa Maendeleo pamoja na Serikali wanapaswa kuendelea kutenga Fedha kwaajili ya huduma za lishe ili kuhakikisha Afya ya watoto ina imarika hasa kwa Mkoa wa Kagera.
Hayo yamejiri wakati wa kufanya mapitio ya maoteo ya Bajeti kwa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambapo Halmashauri imesisitizwa kuendelea kutenga fedha katika bajeti ili kuwezesha Shughuli za lishe kufanyika na kumaliza tatizo la udumavu kwa watoto.
‘‘ Najua rasilimali fedha ni kidogo lakini inabidi kuendelea kutenga katika bajeti ya Serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mapambano dhidi ya udumavu yanaendelea hadi tatizo hilo litakapoisha katika Mkoa wa Kagera’’ alisema Afisa huyo.
Kwaupande wake Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mh, Godfrey Mheluka alipongeza Shirika la IMA World Health kwa kuendelea kutoa elimu juu ya masuala ya lishe na kupambana na udumavu ili kuhakikisha tatizo hilo linamalizika katika Mkoa wa Kagera na hususani Wilaya ya Karagwe.
‘‘Nitumie nafasi hii kulipongeza Shirika la IMMA kwa kuendelea kutoa elimu juu ya masuala haya ya lishe kwani tatizo la udumavu ni kubwa na linaweza kuathiri mipango ya Serikali ya kufikia Uchumi wa Viwanda endapo tutaendelea kuwa na watu wenye udumavu’’ alisema kiongozi huyo.
Mh, Mheluka ameongeza kuwa ili kuwa na maendeleo endelevu kama taifa lazima kuhakikisha masuala ya lishe yanatiliwa mkazo kwani bila kuwa na watu wenye afya bora nivigumu kupata nguvukazi ya taifa.
Ame eleza kuwa kuna haja ya kuweka mpango mkakati wa kuwaelekeza watu namna ya kupata mlo kamili kwani tatizo si chakula bali ni namna ya kupangilia mlo.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Ndg, Godwin M.Kitonka amesisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kuzingatia eneo la lishe katika bajeti zake.
‘‘Sisi kama Halmashauri tutaendelea kuhakikisha tunatenga fedha kwaajiliya Shughuli za lishe ili kumaliza tatizo la udumavu katika Wilaya ya Karagwe’’alisema kiongozi huyo
Mkoa wa Kagera ni moja wapo ya Mikoa yenye tatizo la udumavu ambapo kwa Wilaya ya Karagwe tayari jitihada zinafanyika kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo ili kumaliza tatizo hilo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.