KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ‘AIFAGILIA’ WILAYA YA KARAGWE
Na Innocent Mwalo, KARAGWE
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2018, ndugu Charles Kabeho ameimwagia sifa kemkem wilaya ya Karagwe kutokana na maandalizi yake mazuri katika mapokezi ya mwenge wa uhuru huku akiitaja shughuli hiyo kufana sana.
Maneno hayo ya shukrani yalitolewa na kiongozi huyo katika viwanja vya Shule ya Msingi Benaco Wilayani Ngara yalipofanyika makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya Wilaya ya Karagwe na Ngara mnamo Aprili 14, 2018.
“Kwa dhati kabisa nakuomba Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mh. Godfrey Mheluka nikupongeze kwa jinsi wewe na viongozi wengine wilayani Karagwe mlivyoweza kuhamasisha wananchi waliojitokeza kwa wingi na kufurika sana katika viwanja vya mkesha wa Mwenge wa Uhuru Mjini Kayanga hapo jana”, alisikika Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Karagwe.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo alitoa wito kwa viongozi wote wilayani Karagwe kuendelea kusimamia kwa vitendo ujumbe wa mwenge wa uhuru kwa mwaka huu unaosema “Elimu ni Ufunguo wa Maisha; Wekeza Sasa kwa Manufaa ya Taifa Letu” pamoja na jumbe nyingine za kudumu katika maeneo ya kupambana na rushwa, ugonjwa wa malaria, maambukizo ya ugonjwa wa UKIMWI na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.
Naye Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Mheluka alimwahidi kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kwamba uongozi wilayani Karagwe utafanyia kazi maelekezo na maagizo yote yalitolewa na kiongozi hususani juu ya miradi ya maendeleo.
Baada ya salam hizo yalifanyika makabidhiano ya mwenge wa uhuru wa uhuru kati ya Mkuu wa Wilaya Karagwe Mh. Godfrey Mheluka na Mkuu wa Wilaya ya Ngara Mh. Luteni Kanali (Mstaafu), Michael Mntenjele yaliyoshuhudiwa na umati mkubwa wa wananchi kutoka pande zote mbili yaani wilayani Karagwe na Ngara.
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2018 uliingia Mkoani Kagera ukitokea mkoa wa Geita mnamo Aprili 08, na kuzungushwa katika Halmashauri zote nane (08) za Mkoa wa Kagera; unatarajiwa kukabidhiwa mkoani Kigoma mnamo Aprili 16.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.