Kikao Cha Baraza la Madiwani chafanyika
Na Innocent E. Mwalo
Kikao cha Baraza la Madiwani kwa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kinafanyika kwa muda wa siku mbili yaani tarehe 16/08/2017 na tarehe 17/08/2017 huku mada kadhaa zikitajiwa kujadiliwa katika kikao hicho cha Robo ya Nne ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 ikiwemo ile ya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya na wenyeviti wa kamati za kudumu za Baraza la Madiwani pamoja na kuteua wajumbe wa kamati hizo za kudumu ambao uchaguzi wao hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za mitaa.
Kwa siku ya kwanza yaani tarehe 16/08/2017 kikao kilifunguliwa mapema asubuhi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Mh. Wallace M. Mashanda ambapo kilianza kwa kuthibitiswa kwa dondoo zilitakazotumiwa kama mwongozo kwa mujibu wa kikao hicho cha Baraza hilo la madiwani.
Awali katika taarifa yake kwa Baraza hilo la madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mh. Wallace Mashanda aliwakaribisha wajumbe wa Baraza hilo kujadili kwa umakini mambo yote yaliyoletwa mbele yao kubwa likiwa ni kuja na mikakati mipya ya ukusanyaji wa mapato.
“Mtakumbuka serikali iliagiza Halmashauri kukusanya kwa asilimia themanini la sivyo Halmashauri itakayoshindwa kufanya hivyo itakuwa kwenye hati hati za kutokuwepo”, alisisitiza Mh. Mashanda.
Baadaye taarifa ya serikali ikatolewa kupitia Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey A. Mheluka ambapo katika salamu hizo alisisitiza mambo kadhaa ikiwemo suala la amri ya kuwaondoa wananchi wote waliovamia na kulima kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kusisitiza kwamba ndani ya muda mfupi wananchi hao wanapaswa wawe wameondoka kwenye maeneo hayo vinginevyo watakumbana na nguvu ya dola.
Suala jingina aliloligusia Mh. Mheluka lilikuwa ni pongezi kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kwa kutii agizo la kutokuchoma moto maeneo yao hali aliyoitaja kuwa imekuwa tofauti na miaka mingine kwani maeneo mengi hayachomwa moto ikilinganishwa na vipindi vingine vya nyuma.
Kupitia kikao hicho walitambulishwa pia watumishi wa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) wilayani hapa ambapo Mkuu wa wilaya katika hotuba yake hiyo pia alitumia wasaa huu kusisitiza kuwa kwa kuwa zoezi la kuwaandikisha wananchi limekaribia kuanza basi viongozi hao wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba ni wananchi halali tu ndio wanapata haki hiyo ya kuandikishwa.
Mkuu wa Wilaya Karagwe alitumia hadhara hiyo kuwapa taarifa ya ujio wa boti iliyoletwa na serikali ya Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa ajili ya doria ya kuwaondoa wavamizi kwenye maeneo kadhaa wilayani hapa.
Suala jingine aliloligusia Mkuu wa Wilaya lilikuwa ni agizo la usafi ambapo alitumia jukwaa hilo kuwatangazia wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la usafi na kuagiza kuwa oparesheni kabamba inatajiwa kuanza mapema tarehe 24/08/2017
Akijibu maswali kadhaa yaliyoibuliwa na waheshimiwa madiwani kuhusu masuala kadhaa, Mh. Mkuu wa Wilaya aliendelea kuwasihi wananchi kutumia muda wao mwingi kuendelea kujitafutia mali kwa njia zilizo halali kwa kufanya kazi kwa bidii na kuacha kucheza mchezo uitwao vibonanza kwani mchezo huo hauna tofauti na kamari.
Kikao kiliendelaa kwa ajenda kupokea taarifa kutoka kwa Waheshimiwa madiwani ambao kikanuni ndio wenyeviti wa Kamati za Maendeleo za Kata (WDC), ambapo mambo kadhaa yalijadiliwa ikiwemo faini za moto kwa wale wanaoendelea kukaidi amri hiyo na kuendelea kuchoma moto.
Kilio kikubwa katika taarifa za Kamati hizo za maendeleo ya Kata ilikuwa upungufu wa watumishi hasa watendaji wa kata na vijiji kwenye maeneo yao ambapo azimio liliwekwa kwamba iandaliwe taarifa kwa ajili ya kupelekwa kwenye Mkutano wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa ngazi ya Mkoa (ALAT) ili suala hili hili pamoja na masuala mengine yanayohusu matengenezo ya magari ya serikali yanayofanywa kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) pamoja na ile ianyohusu manunuzi ya vifaa kutoka kwa Wakala wa ununuzi wa vifaa vya Ofisi kutoka Bohari ya Serikali (GPSA) ikitakiwa kuzingatiwa.
Kisha ratiba ikaendea kwa maswali ya papo kwa papo kutoka kwa Wajumbe wa Baraza la Madiwani ambapo agizo lilitolewa na kikao hiki ilikuwa ni kwamba uongozi wa Halmashauri ya wilaya uhakikishe kwamba unazielekeza timu za wataalam za kata kuhakikisha kwamba zinasiziagiza mamlaka za kata kuhakikisha kwamba kikao cha timu ya wataalam kwa nagazi ya kata na vijiji kufanyika kila mara moja kwa mwezi kama ambavyo inafanyika kwa ngazi ya wilaya.
Kikao kiliahirishwa jioni na kinatarajiwa kuendelea mapema tarehe 17/08/2017 kwa ajenda nyingine ambapo ni kwa mujibu wa dondoo zilizothibitishwa kwenye kikao cha tarehe 16/08/2017 ikiwemo kumchagua makamu mwenyekiti pamoja kuteua wajumbe wa kamati za kudumu.
Mada nyingine zitakazowasilishwa zitakuwa nitaarifa ya maazimio ya kikao cha tarehe 03-04/05/2017, Kupokea taarifa ya utendaji za utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri kutoka kwa wenyeviti wa kamati za kudumu na kupokea taarifa za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.