Kikao cha Baraza la Madiwani Chaanza.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Kikao cha Baraza la Madiwani katika Halmashuri ya Wilaya Karagwe kwa robo ya kwanza kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 kimeanza mnamo Novemba 29, 2017 katika Ukumbi wa Angaza ambapo kinatarajiwa kudumu kwa takribani siku mbili (02) huku kikitarajiwa kuangazia mambo kadhaa wa kadhaa yahusuyo maendeleo ya wananchi wilayani hapa.
Mapema kikao hiki kilifunguliwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Wallace Mashanda ambapo pamoja na mengi mengine aliwaongoza wajumbe wa kikao hicho kuthibitisha dondoo zitakazojadiwa katika kikao hicho ambapo wajumbe hao kwa sauti moja waliafiki ajenda zote zilizoletwa kwenye kikao hicho; baadhi zikiwa kupokea taarifa ya serikali iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka.
Katika kikao hicho taarifa ya Mwenyekiti wa Halmashauri pia ilipata kutolewa kwa wajumbe wa kikao hicho.
Mambo mengine yaliyojadiliwa katika siku hiyo ya kwanza ya kikao hiki ambacho ndicho kikao kikubwa cha maamuzi katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ilikuwa ni taarifa kutoka kwa wenyeviti wa Kamati za Maendeleo ya Kata kwa Kata zote 23 zilizopo katika Wilaya hii.
Katika taarifa yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya alisisitiza mambo kadhaa ambayo Halmashauri inatakiwa kuyapa msukumo katika kipindi hiki.
Mosi lilikuwa ni suala la upimaji wa ardhi na utoaji wa hati, ambapo Halmashauri ilitakiwa kuwa na mikakati madhubuti kwenye jambo hilo ili kutokukwamisha jitihada za wawekezaji ambao wameonesha nia ya kuwa tayari kuwekeza kwenye kiwanda cha vigae kinachotajiwa kujengwa kwenye Kata ya Kihanga na uwekezaji mwingine ni ule wa kiwanda cha nyama ambapo kiwanda hicho kimependekezwa na mkoa wa Kagera kujengwa wilayani hapa.
“Halmashauri kupitia menejimenti inapaswa kukimbizana ili kutokukwaza jitihada hizi za uwekezaji katika wilaya yetu”, alisema Mh. Mashanda.
Suala jingine lililogusiwa na Mh. Mashanda lilikuwa ni changamoto inayojitokeza wakati wa upigaji wa chapa mifugo, zoezi linaloendela wilayani hapa kwa sasa, ambapo alionya na kuwatahadharisha baadhi ya watendaji wa serikali za mitaa na serikali kuu kutokutumia zoezi hili kama njia ya kujipatia fedha badala yake wafanye kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa.
“Ni lazima zoezi hili lizingatie pia suala la gharama na ushirikishwaji wa wananchi ili kusiwepo na dhana ya kuongezwa muda uliopangwa katika kufanyika kwa kazi hii hali itakayoweza kukwamisha zoezi hili lisifanikiwe kutokana na kukosekana kwa fedha pindi zoezi hilo litakaporefushwa muda wake uliopangwa”, alisisitiza Mh. Mashanda.
Maelezo yote ya Mh. Mashanda yaliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ambaye nae katika taarifa ya Serikali aliweka mkazo katika mambo hayo.
Kadhalika kupitia kikao hicho, Mh. Mheluka aliiagiza Idara ya Ardhi na Maliasili wilayani hapa kutenga siku ya Jumatano ya kila juma kama mahususi kwa ajili kusikiliza migogoro ya ardhi huku akiwatangazia wajumbe wa Baraza hilo kupitia mkutano huo kwamba ofisi yake imetenga siku ya Alhamisi maalum kwa ajili ya kusikiliza migogoro hiyo ya ardhi ili ofisi yake iwe kama rufaa ya mashauri hayo kutoka ofisi ya Halmashauri ya Wilaya.
Aidha katika hatua ya kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na baadhi ya madiwani kupitia maswali yao kwake hasa kuhusiana na masuala ya uvamizi wa ardhi, Mkuu wa Wilaya na wajumbe wote wa kikao hicho kwa kauli moja walikubaliana kuungana katika kushughulikia mambo ya ardhi wilayani hapa ambapo itaundwa timu kutoka ofisi Halmashauri na ofisi ya Mkuu wa wilaya kwa ajili ya kushughulikia masuala ya ardhi.
Katika taarifa karibu zote za wenyeviti wa Kamati za Maendeleo ya Kata, changamoto ya kucheleweshwa kwa ruzuku iliibuliwa na katika kulitolea ufafanuzi jambo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasahuri ya Wilaya ndugu Godwin Kitonka aliweza kuwasisitiza wajumbe hao kuhakikisha akaunti za benki zinakuwa hai muda wote kwani kwa sasa kuna changamoto kwa baadhi ya vijiji na kata akaunti zake sio hai.
Kikao hicho kinatarajiwa kuendelea mnamo Novemba 30, 2017 ambapo baadhi ya ajenda zinazotajwa kutawala zitakuwa ni maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Madiwani, Kusoma na kuthibitisha Muhtasari wa Kikao cha Baraza la Madiwani cha 03- 04 Mei, 2017, Kupokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita.
Jingine ni kupokea taarifa za utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri kupitia kamati za kudumu za Fedha, Mipango na Uchumi.
Kamati nyingine ambazo taarifa zake zitawasilishwa ni za Elimu, Afya na Maji, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira na ile ya UKIMWI.
Aidha ajenda nyingine zitamulika maeneo ya mapato na matumizi kwa robo ya kwanza 2017/2018, taarifa ya Bodi ya zabuni, Taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Julai – Septemba 2017.
Ajenda nyingine zitahusu taarifa ya Ukaguzi wa Ndani kwa robo ya kwanza 2017/2018, taarifa ya Idara ya Utumishi ba Utawala kwa kipindi hicho pamoja na masuala ya kiutumishi.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.