Na Innocent E. Mwalo.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Lishe na wataalam wa Afya wilayani hapa, mnamo tarehe 19/02/2021 wameshiriki ‘Siku ya Afya na Lishe Kijijini’ iliyofanyika katika Kijiji cha Kagutu katika Kata ya Ndama na kufanya mafunzo kwa wananchi wa kijiji hicho juu ya namna bora ya kuandaa chakula cha watoto wa chini ya miaka mitano.
Mafunzo haya ambayo hufanyika kwa kila robo mwaka kwa vjiji vyote wilayani Karagwe yakiwa na lengo la kupambana na utapiamlo unatokana na lishe duni, yalienda sambamba na utoaji wa Elimu ya lishe, namna ya kuandaa au kupika chakula na kupima uzito pamoja na utambuzi wa watoto wenye utapiamlo.
Kwa kupitia mafunzo hayo, Bi Lustica Mgumba, ambae ni Afisa Lishe wilayani hapa, aliyataja makundi matano ambayo ni mlo kamili wa chakula ambapo kundi la kwanza lilikuwa ni vyakula vya protini ambavyo husaidia kukarabati sehemu zilizochakaa, kuimarisha kinga ya mwili, kuzuia upungufu wa damu na kuuwezesha mwili kufanya kazi kwa ufanisi ambapo orodha ya vyakula hivi ilihusisha vyakula vya asili ya wanyama kama vile nyama, samaki, dagaa, maziwa, mayai, maini, figo, senene, kumbikumbi na wadudu wengine
‘’Kundi la pili ni vyakula vya wanga ambavyo hutokana na nafaka, mizizi na ndizi na vyakula hivi ndivyo vinavyochukua sehemu kubwa ya mlo wa kawaida na hivyo basi ndio vyakula vikuu na mfano wake ni mahindi, mchele, mtama, ulezi, ngano, uwele, viazi vitamu, viazi vitamu, muhogo, magimbi, viazi mviringo na ndizi ambapo vyakula vya kundi hili husaidia kuupa mwili nguvu ya kufanya kazi’’, alisisitiza Bi. Lustica.
Bi Lustica alendelea kutaja kundi la tatu, la nne na tano la vyakula hivyo ambapo katika kundi la tatu alitaja vyakula kama vitamini na madini vikijumuisha matunda ya aina zote yaaani yale yale yanayolimwa na yale ya porini huku akitaja mananasi yanalimwa kwa wingi katika eneo la kijiji cha Kagutu kama mfano wa chakula cha kundi hilo na alisisitiza kuwa hili ni kundi la vyakula vinavyopupa mwili uwezo wa kuzuia na kupambana na maradhi ili kuwezesha mwili kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha kupitia mafunzo hayo, Bi Lustica alilitaja kundi la nne kuwa ni vyakula vinavyohusisha mboga mboga za aina zote yaani zile zinazolimwa na zile zisizolimwa ikiwa ni pamoja na mchicha, majani ya maboga, kisamvu, bamia, mnafu, mchunga na ambazo husaidia mwili kupambana na maradhi
Kundi la tano na la mwisho lilihusisha vyakula vya mafuta lakini yakihitajika kwa kiasi kidogo mwilini ambayo hupatikana kutokana na mbegu za mime kama vile alizeti, pamba, korosho, karanga na mawese ambapo alivielezea kama vyakula vya kuupa mwili nguvu kwa kiasi kikubwa.
Nao wananchi waliokuwa wakifuatilia mafunzo hayo kwa umakini mkubwa walionesha shauku kubwa ya kutaka kujua mambo kadhaa wa kadhaa kuhusua masuala ya lishe ambapo Bi. Jesca Phason mkazi wa Kagutu aliwauliza wawezesha wa mafunzo hayo juu ya muda wa kupika mboga za majani ambapo alidai kuwa kumekuwa na madai ya kwamba upikaji wa muda mrefu huharibu ubora wa chakula hicho ambapo Bi Lustica alimweleza kuwa kwa kawaida upikaji wa mboga z majani unapaswa usizidi dakika tano.
Kwa upande Bi. Beatrice Laurent, Afisa Afya wilayani hapa pamoja na mambo mengine aliihamasisha jamii ya Kagutu na wilaya ya Karagwe kwa ujumla juu ya umuhimu wa ujenzi na matumizi bora ya vyoo ambapo alitoa wito kwa wananchi hao kuwa licha ya umuhimu wa mlo kamili katika vyakula wanavyokula, kazi hiyo inawezaisiwe na tija kutokuwa kama hawatazingatia ujenzi na matumizi bora ya vyoo kwani bila kufanya hivyo kinyesi cha binadamu na mkojo vinaweza kuchafua vyakula hivyo na kueneza vidudu na minyoo ambayo husabisha matatizo makubwa kiafya.
Naye Claudia Nkuba ambaye ni Mratibu Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto wilayani hapa aliwasihi akina mama wajawazito kuhakikisha kuwa wanajifungulia katika vituo vya tiba ili kujihakikishia usafi wa usalama wakati wa kujifungua.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.