Kiama cha Majangili Chanukia Wilayani Karagwe.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Wananchi Wilayani Karagwe hasa Kata zile zinazopakana na Mapori ya Akiba (Game reserves) za Burigi na Kimisi wanaendelea kupewa Elimu ya Uhifadhi wa mazingira ili kutokomeza ujangili unaotajwa kuikosesha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapato.
Elimu hiyo inatolewa na maafisa kutoka Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania, TAWA; Mamlaka yenye jukumu la kusimamia jumla ya mapori ya akiba 28 hapa nchini.
Aidha TAWA wanaifanya kazi hiyo kwa kushirikiana Halmashauri ya Wilaya Karagwe kupitia Idara ya Maliasili na Utalii, Kitengo cha Maliasili.
Kazi hii ilianza mnamo Novemba 14, 2017 ambapo timu hii ya wataalam ikiwahusisha ndugu Mohammed Mpita, ndugu David Gunda, ndugu Winifrida Mkenda (Maafisa wanyamapori/wahifadhi kutoka Club ya Malihai Tanzania, Kanda ya Mwanza), ndugu Winnie Kweka ambaye ni Afisa Wanyamapori kutoka katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi makao yake makuu ya ofisi zake yakiwa Biharamulo pamoja na dereva wao ndugu Rashid George waliambatana na mafiasa maliasili/ wanyamapori kutoka katika Halmashauri ya wilaya Karagwe akiwemo ndugu Rama Masele na ndugu Everyln Swai walifanya uhamasishaji wenye lengo la kutoa Elimu kwa wananchi ili wananchi waweze kushiriki katika uhifadhi wa mapori ya akiba kama ilivyo dhamira ya serikali.
Katika siku hiyo ya kwanza, Elimu ilianza kutolewa katika Kata ya Rugu kwenye vijiji vya Rugu, Kasheshe na Ruhita hali kadhalika kwenye Shule za Msingi za Ruhita, Kasheshe na Rugu na Shule ya Sekondari ya Rugu ambapo katika maeneo yote shule wanafunzi na walimu walijitokeza kwa wingi kupata Elimu hiyo.
Kadhalika katika vijiji hivyo vya kata ya Rugu wananchi nao walijitokeza kwa wingi kusilikiza ujumbe huo ambapo wote kwa pamoja walipata kushiriki na kuuliza maswali kadhaa kuhusiana na masuala ya uhifadhi wa mapori ya akiba ya wanyamapori.
Aidha kazi hii imeendelea Novemba 15, 2017 katika kata ya Nyakasimbi kwenye Shule za msingi za Kabale, Kahanga, Muungano, Kyanyamisa na Shule ya sekondali ya Nyakasimbi huku Elimu hiyo ikitolewa kwa walimu na wanafunzi katika shule hizo.
Hali kadhalika Elimu hiyo imeweza kutolewa kupitia Mkutano wa Hadhara kwa vijiji vya Kahanga, Muungano na Nyakasimbi, mkutano uliofanyika katika soko la Kahanga na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi na viongozi wote wa maeneo hayo.
Pia katika mikutano yote kwa kata za Rugu na Nyakasimbi alikuwepo Afisa Misitu kutoka Wakala wa Misitu Tanzania, TFS hapa Wilayani Karagwe ndugu Sunday John ambaye nae aliungana na kundi hilo katika kutoa Elimu ya uhifadhi wa mazingira hasa misitu.
Awali ndugu Winnie Kweka alitambulisha dhima ya Elimu hii, pamoja na mambo mengine aliwasihi wananchi katika Kata ya Rugu na Nyakasimbi na maeneo mengine ambapo mapori haya yanapita kuacha kuyaona mapori haya na rasilimali zote zilizomo kwenye maeneo haya kama ni mali ya wahifadhi badala yake jamii hiyo ilikumbushwa kuyathamini na kuyaona maeneo hayo kama rasilimali ambayo jamii inao wajibu mkubwa wa kuwa sehemu yake na kushiriki kikamilifu katika kuilinda.
“Mnalo jukumu la msingi katika kushiriki shughuli hizi za uhifadhi kwani kwa sasa Mamlaka ya Wanyama pori na serikali kwa ujumla inataka kufanya uhifadhi wa pamoja kwa kuwashirikisha kikamilifu ninyi wananchi”, alinukuliwa ndugu Kweka katika moja ya mikutano hiyo.
Naye Mohammed Mpita, awali ya yote, aliwakumbusha wananchi juu ya sheria kadhaa zinazowataka kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
Kwanza, alirejea sheria mama; Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, toleo la 1977 ambapo katika Ibara ya 27 (1) inatamka wazi kwamba kila mtanzania ana wajibu wa kulinda mali asili ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
“Pia tunayo sheria ya Kuhifadhi wanyamapori Namba 05 ya Mwaka 2009 inayotamka wazi kwamba wanyama wote wa Tanzania wataendelea kuwa mali ya umma chini ya mamlaka ya Rais kwa niaba ya watu wote wa Tanzania”, alinukaririwa ndugu Mpita akiwasisitiza wananchi hao.
Aidha kwa kurejea sheria hizi mbili ndipo wataalam hawa wakaeleza dhamira ya Mamlaka ya Wanyamapori, TAWA kutoa Elimu hii kwa wananchi hao ili kuwafanya washiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi.
Katika maeneo yote waliyopita wataalam hawa hwakusita kuelezea faida za uhifadhi wa mazingira.
Faida kadhaa zilizotajwa kusababishwa na uhifadhi zilikuwa ni kwamba shughuli hizi zinasaidia katika kudumisha Ikolojia; ikolojia ikiwa na maana ya uhusiano wa wanyama na binadamu, kudumisha tamaduni za watu, kuongeza pato la taifa kwani sekta ya utalii huchangia pato la taifa kwa asilimia 17 na asilimia 25 ya fedha za kigeni inatokana na sekta hii ya utalii.
Ilitajwa faida nyingine kuwa uhifadhi husaidia katika Elimu na utafiti wa kisayansi huku Tanzania ikitajwa kama nchi pekee duniani ambayo katika eneo la Kihansi kuna chura anayezaa ambaye hutumiwa katika shughuli anuai za utafiti wa kisayansi.
“Msije mkasahau faida nyingine za hifadhi hizi kuwa ni vyanzo vya maji, na ni lazima ijulikane kwamba vyanzo vyote vya maji kama vile mto Kagera, Ziwa Viktoria, mto Simiyu na mto Mara hutokana na hifadhi hizi za mapori ya akiba”, alisema ndugu Mpita katika moja ya mikutano hiyo.
Pia kupitia mikutano hiyo, wataalam hao walipata wasaa wa kuwaelimisha wananchi juu ya matatizo yanayoikumba sekta ya uhifadhi hapa nchini na katika eneo hili wananchi waliaswa kutimiza kwa vitendo ile dhana ya uhifadhi shirikishi kwa kuepuka masuala kadhaa yanayotajwa kuzorotesha sekta ya utalii hapa nchini.
Ilitajwa kwamba, pamoja na mambo mengine tatizo la ujangili ni tishio kubwa katika suala la uhifadhi wa wanyamapori hapa wilayani Karagwe na kupitia mikutano hii elimu juu ya dhana ya ujangili iliweza kutolewa ambapo wananchi waliweza kujua maana halisi ya neno jangili.
“Jangili ni mtu yeyote anayekiuka sheria kwa kuvuna maliasili za hifadhi ya wanyama pori bila kibali cha mamlaka hiyo”, alisema ndugu Kweka.
Ndugu Kweka pamoja na wataalam wote kutoka TAWA, waliendelea kusisitiza kwamba kwa mujibu wa sheria ya kuhifadhi wanyamapori namba 05 ya mwaka 2009, mwananchi yeyote anayekamatwa na kuthibitika kwamba ni jangili anahukumiwa kwa kosa la uhujumu uchumi ambapo adhabu yake inakadiriwa kuwa ni miaka 20.
Matatizo mengine yaliyotajwa na wataalam hao kuwa yanaangamiza sekta ya utalii hapa nchini yalikuwa ni suala la kuingiza mifugo kwenye hifadhi jambo ambalo kwa maelezo ya wataalam hao linasababisha pamoja na mambo mengine kukimbia kwa wanyamapori hao kwenye maeneo yao ya hifadhi na hivyo kuathiri suala nzima la ukusanyaji wa mapato.
Hali kadhalika kitendo cha kuingiza mifugo kwenye hifadhi kinasababisha kuambukizwa kwa magonjwa kwa wanyama pori huku wataalam hao wakitaja tofauti kati ya wanyama wanaofugwa na wale walioko kwenye maeneo ya hifadhi kwamba wanyama wanoafugwa wanapuliziwa madawa ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuathiri wanyamapori mara mifugo hiyo itakapoingia kwenye mapori hayo ya akiba.
Aidha lilitajwa tatizo jingine la kuchomwa moto hovyo kwa maeneo ya hifadhi, sambamba na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, mkaa na magogo.
Tatizo jingine lililoainishwa lilikuwa ni suala la uchimbaji wa madini kwenye maeneo hayo ya hifadhi ambapo wataalam hawa walionya wananchi kuepuka kufanya kazi hiyo kwenye maeneo ya hifadhi huku tahadhali ikitolewa kwamba mara baada ya Elimu hii kutolewa utekelezaji wa sheria tajwa kuhusiana na uhifadhi utasimamiwa kikamilifu na wananchi wengi wakaelimishwa kwamba kama hawataitekeleza sheria hii kikamilifu wananweza wakajikuta wakitumikia kifungo cha miaka hiyo 20 na mifugo yao kutaifishwa na serikali kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wao wanafunzi na wananchi waliofikiwa na elimu hii kwenye maeneo yote ya kata za Rugu na Nyakasimbi walikiri kushiriki bila kujua vitendo kadhaa vya ujangili kama vile kula wanyama pori, kuchungia mifugo kwenye maeneo ya hifadhi huku wakiahidi kutokushiriki tena katika vitendo hivyo.
Katika mikutano hiyo, wananchi walipata kuelimishwa juu ya kutoa taarifa kwa watendaj wa vijii na kata juu ya athali za wanyamapori pindi zinapokuwa zimetokea kwenye maeneo yao ambapo viongozi hao wa vijiji na kata wanao wajibu wa kuwasiliana na maafisa wanyama pori kutoka Halmashauri ili tathmini iweze kufanyika kwa kushirikiana na Idara kadhaa za Halmashauri ya wilaya kama vile Idara ya Kilimo kwa ajili ya kupata kifuta jasho au kifuta machozi kutokana na athali inayokuwa imetokea.
Kupitia mikutano hiyo wananchi walipata kuelimishwa kuhusiana na faida watakazozipata pindi watakaposhiriki kikamilifu katika uhifadhi kama vile pato la taifa kuongezeka na hivyo kuiwezesha serikali kutoa huduma muhimu kwa jamii kama maji, shule, huduma za afya, elimu n.k
Ilitajwa faida nyingine kwa Halmshauri husika kwamba, Mamlaka ya Hifadhi itapaswa kuipatia Halmashauri inayozungukwa na pori hilo la hifadhi kiasi cha aaslimia 25 ya faida fedha zinazoingizwa moja kwa moja kwenye mfuko wa Halmashauri ya wilaya na hivyo kuchangia katika uboreshaji wa utoaji wa huduma katika ngazi ya Halmashauri.
Pia, kuna suala la ufadhili wa miradi kadhaa na katika Halmashauri ya Wilaya Karagwe ilitajwa miradi kadhaa iliyotekelezwa kwa ufadhili wa sekta ya utalii kuwa ni ujenzi wa zahanati ya Ruhita, barabara katika kijiji hicho na ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi hiyo iliyopo katika ya Kata ya Rugu.
Elimu nyingine iliyotolewa katika mikutano hiyo ilikuwa ilikuwa ni juu ya mipaka ya wananchi na maeneo ya hifadhi ambapo wananchi walipaswa kuzingatia sheria inayotaka kufanya shughuli zao umbali wa mita 500 kutoka maeneo ya hifadhi na sio vinginevyo.
Elimu hii inaendelea kutolewa katika maneo mengine yanayozungukwa na hifadhi za wanyama pori wilayani hapa huku wito ukiwa ni kuwataka wananchi kutii sheria bila shuruti hali kadhalika kuwahamasisha wananchi kuweza kuanza kubuni miradi kupitia Idara ya Mipango ili maandiko haya yaweze kuwafikia Mamlaka ya wanyama pori Tanzania, TAWA na kisha wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo kama ambavyo inafanywa na Mamlaka ya Mbuga za Wanyama Tanzania, TANAPA katika maeneo yanayopakana na mamlaka hizo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.