KERO YA MAJI YATATULIWA KWENYE BAADHI YA MAENEO WILAYANI KARAGWE.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Serikali Wilayani Karagwe hivi karibuni imezindua miradi miwili ya maji katika maeneo ya Chamchuzi na Chanika- Omurulama lengo likiwa kusogeza kwa wananchi huduma hiyo.
Kukamilika kwa miradi hiyo kunatajwa kwamba kutaleta ahueni ya maisha kwa wananchi wa maeneo hayo na kuwafanya kuwekeza muda wao mwingi katika shughuli nyingine za uzalishaji mali badala ya kuitafuta huduma hiyo umbali mrefu na hivyo kushindwa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji kwenye maeneo yao.
Ziara hii ya siku mbili ilianzia katika eneo la Chamchuzi ambapo mradi huu umetekelezwa na kampuni ya DENIKO CO LTD ya Arusha ukigharimu kiasi cha shilingi 1,614,682,652.50 huku ukilenga kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa umbali usiozidi mita 400 na kuongeza asilimia ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama kutoka asilimia 52 hadi 57 na wananchi wapatao 14,500 wakitarajiwa kunufaika na mradi huo.
Mapema katika taarifa iliyosomwa na Mhandisi wa Maji Wilaya, Mhandisi Magai Kakuru ilibainisha ya kwamba kukamilika kwa mradi huu kutakuwa ni fursa kwa wananchi wa vijiji vya Chamchuzi na Muguluka kufanya shughuli nyingine za maendeleo hususani akina mama na watoto kwani maji kwa sasa kwao sio tatizo tena.
Siku ya pili ya ziara hii ilikuwa ni uzinduzi wa mradi wa Chanika- Omurulama ambapo mradi huu umetumia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 700,000,000.00 na unatajwa kuwa na ujazo wa lita 135,000 ulikenga kuwahudumia wananchi wa vijiji vya Chanika na Omurulama.
Mapema katika taarifa yao kwa Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh.Wallace Mashanda, Mtendaji wa Kijiji cha Chanika alibainisha baadhi ya changamoto kufuatia kukabidhiwa kwa mradi huo ambapo alitaja baadhi ya mambo kama vile chanzo cha maji kutokutoa moshi, tatizo la kukosekana kwa “air valve”, kukosekana kwa nyumba ya mlinzi na kutokukamilika kwa nyumba ya mlinzi.
Kwa upande wake Mh. Mashanda alitumia wasaa huo kumwelekeza Mkandarasi wa kampuni ya Jorena & Matrices TV, ndugu Andrew Kazimili na uongozi wa kata ya Chanika kuzifanyia kazi changamoto zote katika kipindi hiki cha miezi sita ya matazamio na akaagiza kama kuna mambo yapo kwenye mpango wa ujenzi (BOQ) basi mkanadarasi huyo ayatekeleze mara moja na kwa uongozi wa kijiji, kata na Jumuiya watumia maji watekeleze yale yasiyo kuwa kwenye mpango huo ili kuufanya mradi huo kuwa na ufanisi pindi utakapokabidhiwa.
“Aidha, ninauagiza uongozi wa kata kumwandikia barua Meneja wa TANESCO Wilaya ili kuwekwa kwenye mpango wa jazia ya mradi wa usambazaji wa umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme vijijini (REA) maeneo haya ya vyanzo vya maji kutokana na changamoto ya ununuzi wa mafuta mliyoitoa katika risala yenu”, alisema Mh. Mashanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, ndugu Godwin Kitonka aliunga mkono wazo la Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya kuhusu kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji wa mradi huku akiwapa changamoto viongozi ya kuitisha kikao cha kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji hasa posho wanazolipwa viongozi akiwemo Mwenyekiti, Katibu, Fundi na Mweka Hazina.
Agizo jingine lilikuwa ni kwa wananchi hao kutunza vyanzo vya maji huku wito ukitolewa juu ya suala la kulinda vyanzo vya maji ambapo kwa kuanzia iliamriwa ya kwamba kibandikwe kibao katika chanzo cha maji cha Omurulama kwa ajili ya kuzuia wafugaji kunyweshea mifugo katika eneo hilo.
Katika tukio hilo ndugu Abdala Said wa Omurulama na Edelbelt Wilson wa Chanika walikabidhiwa na Mgeni rasmi hati ya kukumilika kwa mradi huo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.