WANANCHI WILAYANI KARAGWE WAONYWA VIKALI UHARIBIFU WA MAZINGIRA.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Wananchi wilayani Karagwe wameonywa vikali kutokujihusisha na masuala ya uhalibifu wa mazingira ili kuepuka athali mbalimbali zinazoweza kutokea kutokana na madhara hayo ya kushindwa kufanya uhifadhi wa mazingira.
Maagizo hayo yalitolewa na Mh. Innocent Nsena, Katibu Tawala wa Wilaya ya Karagwe, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani inayofanyika duniani kila mwaka tarehe 5, June ambapo kwa mwaka huu, hapa wilayani Karagwe maadhimisho haya yamefanyikia katika kata ya Kihanga.
Katika sherehe hizi wananchi waliweza kushirikia katika zoezi la usafi wa mazingira ambapo mgeni rasmi na wageni waalikwa waliweza kukagua na kushiriki katika zoezi la usafi lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya kata ya Kihanga.
Katika maadhimisho hayo, Rama Masele ambaye ni Afisa Misitu katika Halmashauri aliweza kusoma risala kwa mgeni rasmi ambapo pamoja na mambo mengine ilibainisha madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ya kwamba ni kwa ajili ya kuhamasisha jamii duniani kote kuelewa masuala yahusuyo Mazingira na pia kuhamasisha watu wa jamii mbalimbali duniani kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira.
“Tunatumia siku hii kutoa fursa kwa jamii kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi katika Mazingira na kuhamasisha jamii kufanya mazingira yao kuwa salama na masafi ili sote tufurahie hali hiyo katika maisha yetu na vizazi vyetu”, alisisitiza Masele kupitia risala hiyo.
Aidha risala hiyo iliweza kubainisha baadhi ya mikakati ambayo Idara ya Mazingira na Taka ngumu imejiwekea katika kufikia azima ya kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuepukana na uchomaji moto misitu na uoto wa asili, ukataji miti kiholela na uchafuzi wa mazingira yanayowazunguka kwa njia mbalimbali.
Mikakati mingine ni kukusanya takwimu za vyanzo vya maji vilivyoainishwa mipaka yake na vilivyopandwa miti rafiki na mazingira ya vyanzo vya maji, kukagua na kufanya usafi kwa maeneo ya makazi, Taasisi, Masoko/Magulio, minada pamoja na kusafisha na kuzibua mitaro.
Pia mikakati mingine inahusus kuhamasisha wenyeviti wa vijiji na Vitongoji kusimamia sheria za kudhibiti uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa vyanzo vya maji na uchomaji moto hovyo na kuelimisha na kuhamasisha Wananchi juu ya huifadhi ,usimamizi na usafi wa mazingira na matumizi ya majiko banifu kwa njia ya maonyesho, maelezo, hotuba n.k
Kupitia maadhimisho hayo, Mh. Nsena alitoa maagizo yaserikali ikiwemo wananchi kutokujihusisha na masuala ya uchomaji wa moto, kutokulima kwenye vyanzo vya maji na kuepuka kukata miti hovyo.
“Suala la usafi wa kila mwisho wa wiki ambapo kwa wilaya yetu hufanyika kila Alhamisi ya wiki ni kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni lazima liwekewe mkazo na nitoe maagizo kwa watendaji wa serikali kulisimamia jambo hilo kikamilifu”, alisisitiza Mh. Nsena.
Katika hatua nyingine Mh. Nsena aliwaeleza wananchi wa Kihanga na Wilayani Karagwe kwa ujumla kujiepusha na ununuzi wa zao la kahawa kwa mfumo unaojulikana kama butula ambao unatajwa kumnyonya mkulima wa hali ya chini na akaahidi ya kwamba yeyote atakayekiuka agizo hilo atakumbana na mkono wa sheria.
Kila tarehe 5 Juni, ya kila mwaka Watanzania tunaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliamuliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972,wakati wa Mkutano wa kwanzawa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira huko Stockholm, nchini Sweden. Aidha, Azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nations Environment Programme (UNEP) lilipitishwa pia siku hiyo. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kila mwaka tarehe 5 Juni, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.