Karalo Yazizima Ugeni wa Marafiki Kutoka Ujerumani.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya wageni kutoka shule ya Kurt Masur nchini Ujerumani Novemba 21, 2017 walijikuta wakibubujwa na machozi ili kuonesha furaha walikuwa nayo kufuatia shangwe za umati wa wananchi na wanakijiji wakiongozwa na walimu wa shule ya Msingi Karalo waliojipanga barabarani ili kuwapokea wageni hao waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kujitambulisha na kutengeneza urafiki kati ya shule hizo mbili.
Umati huo uliongozwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi hiyo ndugu Elizeus Iromba aliyekuwa akishirikiana kwa karibu na mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo ambaye pia ni mwalimu wa michezo shuleni hapo mwalimu Willium Magesa waliwalaki kwa furaha na bashasha wageni hao.
Baada ya kuwasili katika viwanja vya shule ya Msingi Karalo, kikundi cha ngoma na kwaya ya wanafunzi waliweza kutumbuiza kwa nyimbo za kuvutia zilizowahamasisha wageni hao kwa namna moja kushiriki katika michezo hiyo hasa ngoma.
Awali Mwalimu Iromba aliweza kuwatambusha walimu, wajumbe wa kamati ya shule na viongozi wa serikali ya kijiji waliokuwa wamekusanyika katika hadhara hiyo.
Kisha wageni kutoka katika shirika lisilo la kiserikali la Jambo Bukoba ambao ni Bi. Imani Paulo, Meneja Mradi na Bw. Lameck Kiula, Meneja Mawasiliano nao wakajitambulisha na kuwatambulisha wageni waliokuwa wameambatana nao ambao ni Bi. Heike Henstschel ambaye ni Mkuu wa Shule ya Kurt Masul kutoka Ujerumani aliyeambatana na mwalimu kutoka katika shule hiyo Bi. Katja Wachler, Bi Costanze Meinel ambaye ni mmoja wa wazazi wenye watoto katika shule hiyo ya Kurt Masur na Bi. Manuela Hubner ambaye ni mratibu katika shule hiyo.
Msafara huo pia ulikuwa umeambatana na Afisa Utamaduni wa Wilaya hii ndugu Alloyce Mujungu aliyekwenda kwenye shamrashamra hizo kwa ajili ya kumwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmsahauri ya wilaya aliyeshindwa kufika kutokana na majukumu mengine.
Mapema Bi. Iman Paulo aliieleza hadhara hiyo kwamba tangu kuanzishwa kwa shirika la Jambo Bukoba mnamo mwaka 2008, Taasisi hiyo imekuwa ikisaidia katika shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani hapa.
“Tangu kuanzishwa kwa taasisi yetu tumekuwa tukifundisha vijana wa shule ya msingi usawa wa kijinsia, Elimu ya UKIMWI na ujenzi wa miundombinu ambapo hapa wilayani Karagwe taasisi yetu imeweza kujenga madarasa mawili pamoja na kutoa madawati 20 katika Shule ya Msingi Karalo”, alisema Bi. Imani
Kisha baada ya maelezo hayo Bi. Imani aliieleza hadhara hiyo kwamba lengo la ziara yao ya Novemba 21, 2017 kuwa ilikuwa kwenda Shule ya msingi Karalo kwa ajili ya kwenda kuwatambulisha marafiki wa shule ya msingi Karalo ambao ni shule ya Kurt Masur iliyopo nchini Ujerumani.
Kadhalika Bi. Imani shughuli nyingine kufanywa kupitia mkutano huo kuwa ni kutoa zawadi ya kompyuta mpakato (laptop), kamera na simu ya smart phone zilizotolewa na shule ya Kurt Masur kwa lengo la kurahisisha mawasiliano na shule ya msingi Karalo.
Mwalimu Iromba alitumia muda wake mwingi kuisifu taasisi ya Jambo Bukoba kwa namna ilivyosaidia ujenzi wa madarasa mawili, madawati 20 na ujenzi wa visima viwili vya maji.
“Pia tunawashukuru marafiki zetu shule ya Kurt Masur kwa msaada wa kompyuta, kamera na simu ya smart phone kwa kweli wametusaidia sana maana tulikuwa na jukumu la kununua kompyuta kutokana na uhitaji wake hivi karibuni lakini tunawashukuru sana marafiki zetu”, alisisitiza Mwalimu Iromba.
Pamoja na haya risala iliyosomwa na Mwalimu Iromba ilibainisha changamoto kadhaa zinazoikumba shule hiyo kama vile mapungufu ya matundu ya choo kwa ajili ya wanafunzi, tatizo la nyumba takribani 13 kwa ajili ya walimu.
Changamoto nyingine aliyoiainisha ilikuwa ni suala la wanafunzi kutokunywa uji lakini akasisitiza kwamba tayari suala hilo limewekewa mikakati ya kwamba mara wazazi watakapovuna mwezi Februari 2018 basi kila mzazi analo jukumu la kupeleka mahindi shuleni hapo kwa ajili ya uji wa wanafunzi kwa ajili ya kuimarisha suala la taaluma shuleni hapo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.