Karagwe yapendekeza kujenga Kiwanda cha Nyama
Na, Geofrey A.Kazaula – Karagwe
Kufuatia mapendekezo ya Mkoa wa Kagera ya kila Wilaya kuwa na kiwanda kimoja na bidhaa moja, Wilaya ya Karagwe imefikia makubaliano ya kujenga kiwanda cha nyama ili kuendana na Mapendekezo ya Mkoa pamoja na kutekeleza Sera ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwa na Uchumi wa viwanda.
Awali akifungua kikao cha wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe , Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mh, Godfrey Mheluka amesisitiza kuwa wadau hao wahakikishe wanapendekeza kiwanda ambacho kitawanufaisha wananchi wote bila kujali hali zao za kiuchumi
Kwa upande wake , Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi, Ashura Kajuna ameeleza kuwa tayari Halmashauri imetenga eneo la viwanda lililopo katika Kata ya Kihanga.
Aidha, ame eleza kuwa eneo hilo lina sifa ya kuwa eneo la viwanda kwani tayari lina umeme, lina maji na lina barabara ya lami na hivyo lina fikika kwa urahisi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mh, Wallace Mashanda ameeleza kuwa wafugaji kwa sasa wanapaswa kujiunga katika ushirika kama lilivyo agizo la serikali na kueleza kuwa Serikali itawawezesha wafugaji hao ikiwa watakuwa katika ushirika huku akifafanua kuwa kigezo kimoja wapo cha kuunda ushirika ni kuhakikisha wahusika wote ni wale wenye mifugo tu.
Kikao hicho kilihusisha pia wananchi na wadau mbalimbali ambao nao walitoa mapendekezo juu ya sababu muhimu za kuwa na kiwanda cha nyama badala ya zao lingine.
Baadhi ya sababu zilizotolewa na wadau juu ya kutakiwa kujenga kiwanda cha nyama ni pamoja na kwamba mazao mengine kama matunda, mahindi, ndizi, Arizeti, maharage na kahawa tayari yana viwanda vyake na kwamba kiwanda cha nyama bado hakijajengwa.
Aidha wameeleza kuwa Wilaya ya Karagwe ina ng’ombe wengi watakao uzwa katika kiwanda hicho na kuwapatia wananchi kipato tofauti na hivi sasa ambapo bei ya ng’ombe ipo chini kutokana na umbali wa kuwafikisha sokoni .
Sababu nyingine zilizo pelekea kufikia makubaliano hayo ni kwamba mapendekezo ya Mkoa yaliyotolewa kwa kila Wilaya, hakuna Wilaya iliyopendekezwa kujenga kiwanda cha nyama na kwamba kwasababu Wilaya ya Karagwe inao uwezo wa kuingiza ng’ombe 1500-2000 sokoni kila mwezi uwezo wa kuendesha kiwanda cha nyama ni mkubwa ambapo ng’ombe wote wa ukanda huu wanaweza kupata soko .
Licha ya ng’ombe wadau hao wameeleza kuwa kuna mifugo mingine kama mbuzi ambayo pia inaweza kuchakatwa katika kiwanda hicho na kuwaingizia wananchi kipato
Ili kufikia lengo hilo la kujenga kwanda cha nyama, wadau hao wamependekeza kuwa elimu iendelee kutolewa kwa wafugaji ili kuhakikisha wanafuga kisasa kwa maana ya kuwa na mifugo kidogo yenye tija, kuwa hamasisha wakulima kulima mazao ya kutosha ikiwa ni pamoja na kulima chakula cha mifugo, kutafuta madume bora ya ng’ombe ili kupata ng’ombe wakubwa na wenye tija, kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima, na kwamba wazo hilo la ujenzi wa kiwanda cha nyama liendane sambamba na ujenzi wa kiwanda cha ngozi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mh, Wallace Mashanda ametoa wito kwa wadau mbalimbali ambao tayari wanatengeneza bidhaa hasa zinazotokana na ndizi kuhakikisha bidhaa hizo zinawekewa mkakati endelevu ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ulimaji wa mazao husika.
Aidha amesisitiza kuwa mazao hayo yaongezwe ubora kwa kushirikisha vyombo kama TBS na TFDA ili kuyawezesha kupata soko na kuondoa hofu kwa walaji jambo ambalo amesema lifanyiwe kazi kwa wakati.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.