Kamati ya Lishe Yazinduliwa Wilayani Karagwe.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Kikao cha kwanza cha Kamati ya Lishe Wilayani hapa kimefanyika mnamo Januari 30, 2018 katika Ukumbi wa ELCT kwa kuzinduliwa Kamati hiyo inayomjumuisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Katibu wake atakuwa Mratibu wa Lishe katika Halmashauri.
Wajumbe walikuwa ni Mganga mkuu wilaya, Afisa mipango, Afisa Habari, Afisa Elimu msingi, Afisa Elimu sekondari, Afisa kilimo, umwagiliaji na ushirika, Afisa mifugo na uvuvi, Afisa maendeleo ya Jamii, Mhandisi wa maji, Wawakilishi wa dini (Wakristo na Waislamu), wawakilishi wa Asasi za kijamii, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wawakilishi wa sekta binafsi, wawakilishi kutoka vyuo vya afya na wawakilishi wa vyombo vya habari.
Aidha baadhi ya wajumbe wataalikwa endapo kuna uhitaji wa maelezo ya kitaalamu katika kamati ya Lishe, kama Afisa biashara, Afisa Afya, Mratibu wa afya ya baba, mama na mtoto n.k
Kwa mujibu wa mwongozo kamati hiyo itakuwa na majukumu ya kusimamia, kuongoza, kutathmini na kufuatilia utekelezaji wa shughuli mtambuka za lishe katika halmashauri.
“Mtatakiwa Kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa kamati ya lishe kwenye mikutano muhimu, kuandaa na kutekeleza maadhimisho ya kidunia au kitaifa yanayohusika na masuala ya lishe mfano; wiki ya unyonyeshaji n.k”, alisisitiza Gisela Richard, Afisa Lishe.
Bi Gisela alisisitiza kwamba kamati hii itakuwa na jukumu la kuhamasisha jamii juu ya masuala ya lishe mfano suala la watoto kupata chanjo na matone ya Vitamin A.
Nae Mgeni rasmi, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bi. Adeodatha Peter ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii aliweza kuwasisitiza wajumbe hao kukubali kufanya kazi katika mazingira ya changamoto lengo ni kuondokana na matatizo yanayoweza kwakumba watoto ikiwemo kuepuka suala la utapiamlo linaweza kuchochea udumavu wa akili.
Kamati hii ya lishe itatakiwa kukutana mara moja katika kipindi cha miezi mitatu kwa lengo la kujadili utekelezaji wa majukumu yao.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.