Jambo Bukoba Wapiga Hodi kwa Mkuu wa Wilaya Karagwe.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka, Novemba 21, 2017 alipokea ugeni wa wa wajumbe sita (06) kutoka katika shirika lisilokuwa la kiserikali lijulikanalo kama Jambo Bukoba lenye makao makuu mjini Bukoba na wengine wakitoka katika shule ya Kurt Masur iliyopo nchini Ujerumani.
Kutoka katika ofisi za Jambo Bukoba walikuwepo Bi. Iman Paulo ambaye ni Meneja Mradi na Bw. Lameck Kiula, Meneja Mawasiliano.
Aidha kutoka Ujerumani walikuwepo Bi Heike Henstschel ambaye ni Mkuu wa Shule hiyo ya Kurt Masul.
Wengine katika msafara walikuwa ni mwalimu katika shule hiyo Bi. Katja Wachler, Bi Costanze Meinel ambaye ni mmoja wa wazazi wenye watoto katika shule hiyo ya Kurt Masur pia alikuwepo Bi. Manuela Hubner ambaye ni mratibu katika shule hiyo.
Msafara huo uliambatana ndugu Alloyce Mujungu aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe ndg. Godwin Kitonka aliyekuwa na majukumu mengine.
Kadhalika walikuwepo mwalimu Elizeus Iromba, mwalimu Willium Magesa na wanafunzi wao wawili wa darasa la sita ambao ni Eliya Petro na Asimwe Karugendo kutoka katika shule ya Msingi Karalo.
Walipowasili katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya Karagwe wageni hawa walitambulishwa kwa Mkuu wa Wilaya Karagwe na ndugu Mujungu ambaye alimweleza Mkuu wa Wilaya Karagwe Mh. Mheluka kwamba ugeni huo ulikuwa mahususi kwa ajili ya kwenda Shule ya Msingi Karalo, Kata ya Ihanda kwa ajili ya shirika la Jambo Bukoba kuutambulisha urafiki kati ya Shule ya Msingi Karalo na Shule ya Kurt Masur.
“Mh. Mkuu wa Wilaya pamoja na kwamba ugeni huu unakwenda kufanya utambulisho wa ugeni huu kule shule ya msingi Karalo tayari wageni wetu hawa wameandaa zawadi watakazokwenda kuwapa marafiki zao hao ambazo ni kompyuta mpakato (laptop), kamera na simu aina ya Smart phone”, alisema ndugu Mujungu.
Aidha ndugu Mujungu aliweza kumweleza Mh. Mheluka sababu iliyowafanya Jambo Bukoba kuichagua shule ya msingi Karalo kwamba ni moja kati ya shule zilizoshinda vigezo vya kufadhiliwa na shirika la Jambo Bukoba ikiwemo kufanya vizuri katika shughuli za michezo moja kati ya vipaumbele vya shirika hilo.
Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Mheluka alilishukuru sana shirika la Jambo Bukoba kwa kazi nzuri wanayoifanya wilayani hapa huku pamoja na mambo mengine akiwaomba kukuza wigo kwa kusaidia shule nyingi zaidi.
Ombi jingine alilolitoa Mh. Mheluka lilikuwa ni suala la jambo Bukoba kusaidia katika ukamishwaji wa ujenzi wa miundombinu ya tenki la maji kwa ajili ya kuhifadhi maji yatayotumika katika shughuli za uokozi katika majanga ya moto ambayo kwa mujibu wa Mh. Mheluka aliyataja kutokea mara mbili kwa mwaka 2016.
“Najua kuna masuala ya bajeti katika taasisi yenu lakini kwa kweli tatizo hilo ni kubwa na ningeliomba mlichukue na kutusaidia kadri mtakavyoweza”, alisisitiza Mh. Mheluka.
Meneja Mradi kutoka Jambo Bukoba, ndugu Iman Paulo, akijibu ombi hilo alimuomba Mkuu wa Wilaya kufanya andiko la mradi huo ili ofisi yake iweze kupitia na kuona kipi ofisi hiyo inaweza kufanya katika kutekeleza ombi hilo ambapo Mkuu wa Wilaya alimwagiza ndugu Alloyce Mujungu kuwasiliana na Mkuu wa Idara ya Kikosi cha Zimamoto wilayani hapa ndugu Peter Mmbare kwa ajili ya kuandaa taarifa hiyo na kuituma kwenye ofisi za Jambo Bukoba.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.