Idara ya Maji, Maendeleo ya Jamii zaendelea Kuhamasisha Uundwaji wa Jumuiya za Watumiaji Maji.
Na Innocent E. Mwalo, Karagwe
Idara ya Maji Vijijini kwa kushirikiana na ile ya Maendeleeo ya Jamii na Ustawi wa Jamii, zimeendelea kufanya mikutano kadhaa wa kadhaa wilayani hapa kwa lengo la kuhamasisha wananchi juu ya uundwaji wa Jumuiya za watumiaji wa maji katika maeneo yao ikiwa ni kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2009, sheria namba 12 na Sera ya Maji ya Mwaka 2012 kwa pamoja zinatoa nafasi ya uanzishawaji wa jumuiya hiyo.
Haya yalibainishwa mnamo tarehe 19/10/2017 na Bi. Flora Rwetabura, Jackreen Jacob ambao ni mafundi Sanifu toka Idara ya Maji na Bi. Edina Kabyazi, Afisa Maendeleo ya Jamii na msajili wa Jumuiya za watumia maji walipofika katika kijiji cha Kijumbura kilichopo katika kata ya Bweranyange ikiwa ni mwendelezo wa shughuli ya utoaji wa Elimu ya uhamasishaji wa uundwaji wa Jumuiya hizo kama ambavyo imekwisha kufanyika kwenye maeneo mengine katika wilaya hii.
Katika Mkutano huo uliofanyika katika Shule ya Msingi Kijumbura na kuhudhuriwa na wananchi wa kijiji hicho, Elimu kuhusu umuhimu wa uanzishwaji wa Jumuiya hizo ilitolewa pamoja na uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya hiyo uliweza kufanyika.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kijumbura, ndugu Even Eustard katika maneno yake ya ufunguzi aliwashukuru wataalam hawa kutoka Halmashauri ya wilaya kwa kufika katika eneo hilo kwa kazi hiyo ya uhamasishaji huku akikiri kutokuwepo kwa jumuiya hizo kijijini hapo kwa kudai kuwa huenda kumepelekea matatizo mengi ya miundombimu ya maji
“Kati ya mabomba saba ya maji yaliyopo kijijini hapo ni mabomba matatu tu ndiyo yanayofanya kazi chanzo kikiwa ni kukosekana kwa uratibu ambao ungeweza kufanywa kupitia Jumuiya ya watumia maji kama inavyofanywa kwenye maeneo mengine kwenye jumuiya kama hizo”, alikaririwa akisema ndugu Eustard.
Kwa upande wake Bi. Edina Kabyazi, Afisa Maendeleo ya Jamii na Msajili wa Jumuiya za watumiaji wa maji ambaye ndiye alikukuwa mwenzeshaji mkuu katika hadhara hiyo, alitumia muda mwingi kuwaeleza wananchi hao waliokuwa wakimsikiliza kwa makini kuhusu umuhimu wa Jumuiya za watumiaji maji.
“Kama mnavyofahamu umuhimu wa ushiriki wa wanannchi katika shughuli za maendeleo, na huo ndio msingi wa serikali yetu kuanzisha sheria hii kwa ajili kuwawezesha wananchi kuunda Jumuiya hizi zenye jukumu kubwa la kulinda na kukarabati miundombinu ya maji”, alisema Bi. Edina.
Aidha, Bi. Edina alizitaja faida nyingine kadhaa za uanzishwaji wa Jumuiya kama zinavyotajwa kwenye sheria hiyo kwamba jumuiya hiyo inakuwa na nguvu kisheria ya kumiliki mali zote, kutumia miundombinu hiyo ya maji, kutengeneza sheria ikiwemo kuwa na katiba na kanuni kuhusu jumuiya husika, kutengeneza miundombinu hiyo ya maji pindi inapotokea uharibifu pia kukubalina na wanajumuiya juu ya michango ya kuchangia katika kuratibu shughuli za jumuiya hiyo ya maji.
Zaidi ya hayo, Bi. Edina aliitaja kazi nyingine za jumuiya ya maji kwamba ndio itakayokuwa na jukumu kikatiba na kisheria ya kuwasiliana na kuushirikisha uongozi wa serikali ya kijiji au taasisi nyingine zinahusika na masula ya ardhi kwa ajili ya kupanga masuala yanayohusiana na uratibu wa shughuli za jumuiya husika.
Kupitia mkutano huo,Bi. Edina aliendelea, kusisitiza kwamba kwa kuwa Jumuiya hiyo ndiyo yenye jukumu kisheria la kukarabati miradi ya miundombinu ya maji, mkutano mkuu wa kijiji ndio wenye jukumu la kuchagua wajumbe 13 wa jumuiya hiyo akiwemo fundi huku kwa suala la jinsia likipaswa kuzingatiwa katika uchaguzi huo.
“Pia mkutano mkuu wa kijiji unapaswa kuchagua jina la kikundi ambalo halipaswi kuwa jina la mahala popote na kupitisha katiba na kanuni kwa ajili ya jumuiya husika”, alisisitiza Bi. Edina.
“Na kwa kuwa mwamko wa watu juu ya jambi hili bado ni mdogo nawaomba ninyi wenyeviti wa vitongoji kwenda kuhamasisha watu kwenye vitongoji vyenu ili waweze kupata elimu juu ya jambo hili kwani uundaji wa jumuiya hii una faida kubwa wananchi hawa kama tulivyotangulia kusema”, aliongeza Bi. Edina.
Katika mkutano huu masuala kadhaa yalisisitizwa ambapo wananchi walipata ufafanuzi kutoka kwa wataalam hawa kutoka Halmashauri ya wilaya hasa juu ya kuwa na fundi katika kila jumuiya kwani wananchi hao walihoji kama mafundi wao katika jumuiya wakishindwa kupata ufumbuzi wa tatizo fulani kuhusiana na tatizo la miundombinu ya maji ambapo walijibiwa kwamba mafundi hawa ambao mbeleni hujengewa uwezo wa kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao lakini wanaposhindwa kulipatia ufumbuzi jambo fulani basi uongozi wa jumuiya unao wajibu na jukumu la kumtafuta Mhandisi wa maji wa wilaya kwa ajili ya ufumbuzi wa tatizo hilo.
Kupitia mkutano huu wananchi wa Kijiji cha Kijumbura waliweza ,kuchagua uongozi watu kumi na mbili wakiongozwa na Amos Rumanyika aliyechaguliwa Mwenyekiti, Jackson Rweyabura, Katibu na Bi. Editha Pius akichaguliwa Mweka Hazina.
Wajumbe wengine waliochaguliwa walikuwa Albert Kagande, Jackson Kabonga, Justa Medard, Malius Medard, Fumacut Eustard, Gipson Wilson, Saraphina Dioniz, Flora Joas, Severine Jurinary, na Joas Byakubana huku jumuiya saba zinazohusisha vitongoji vya Mujunju, Kijumbura, Kazingaina, Kikonje, Kashasha, Bweranyange, Kashebe zikitarajiwa kuundwa.
Halmashauri ya wilaya Karagwe kupitia Idara ya Maji Vijijini na Idara ya Maendeleo ya Jamii inayo mikakati kabambe inayolenga kuimarisha shughuli za upatikanaji wa maji safi na salama kwani itakumbukwa kwamba tatizo la matumizi ya maji safi na salama bado ni kubwa hapa nchini kwani ni asilimia 49 tu ndio inayosemekana kupata na kutumia maji safi na salama.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.