ICAP Kuzuia maambukizi mapya ya UKIMWI.
Na, Geofrey A.Kazaula, KARAGWE
Shirika la kimataifa linalopambana na UKIMWI ambalo ni International Center of AIDS Care and Treatment Programs (ICAP ) kwa sasa limepata mradi mpya utakao dumu kwa muda wa miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2021/2022.
Kwa mujibu wa Manager mradi wa Mkoa wa Kagera Dr, Omar Msumi Shirika hilo limekuwa likifanya kazi ndani ya Mkoa wa Kagera na sasa Shirika limepata mradi mpya uitwao ‘FIKA’ ambao utajikita katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa wasichana walioko katika umri wa barehe na wale wanaofanya biashara ya ngono.
Kwa mujibu wa Utafiti wa viashiria vya UKIMWI na Malaria nchini wa mwaka 2011/2012 wastani wa kiwango cha maambukizi ya VVU miongoni mwa watu wenye umri kati ya miaka 15-49 ni asilimia 5.1, hii ina maana kuwa katika kila watu 100 watu watano (5) wanaishi na maambukizi ya VVU.
Aidha, takwimu zinaonesha kuwa kuna takribani watu 1,325,271 wanao ishi na VVU nchini kwa mujibu wa takwimu kwa kipindi kinachoishia Juni 2016.
Dr Msumi amefafanua kuwa kwa Wilaya ya Karagwe , mradi ulianza tangu April, 2017 kwa baadhi ya Kata na kwamba sasa mradi umepanuka na kuifikia Wilaya nzima.
Aidha, ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa na Shirika kwa kushirikiana na Serikali kupitia mganga mkuu wa Mkoa na Mganga mkuu wa Wilaya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Wilaya ya Karagwe Dr Libamba Sobo ameeleza kuwa mradi unaendelea kutekelezwa wilaya nzima na kwamba lengo la serikali ni kumaliza kabisa maambukizi mapya ya VVU.
”Lengo la Serikali ni kuhakikisha maambukizi ya VVU yanaisha na kubakia 0 ifikapo mwaka 2030.’’, alisema Dkt. Sobo.
Tayari shirika kwa kushirikiana na ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Karagwe limetoa mafunzo kwa wataalam katika ngazi mbalimbali ambao watatekeleza mradi huo na kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanafikia ukomo kama yalivyo malengo ya Serikali .
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.